Jumanne tarehe 10 Julai 2018
Leo ni Jumanne tarehe 26 Shawwal 1439 Hijria sawa na Julai 10, 2018.
Miaka 277 iliyopita katika siku kama hii ya leo ardhi ya Alaska iligunduliwa na mvumbuzi wa Kidenmark kwa jina la Vitus Bering. Mvumbuzi huyo aligundua ardhi ya Alaska inayopatikana kaskazini magharibi mwa Canada akiwa katika safari yake kuelekea Urusi. Hadi kufikia mwaka 1867 eneo tajiri kwa mafuta la Alaska lilikuwa sehemu ya mamlaka ya Urusi ya Kitezari. Hata hivyo mwaka huo Urusi iliiuzia Marekani ardhi ya Alaska kwa kiasi cha dola milioni saba, eneo ambalo leo hii linahesabiwa kuwa jimbo la 49 la Marekani.
Tarehe 26 Shawwal miaka 146 iliyopita alifariki dunia Ayatullah Abdul Majiid al Musawi, faqihi na mrajaa mkubwa wa Waislamu wa Iran katika kipindi hicho. Alihifadhi kichwani Qur'ani nzima akiwa na umri wa miaka saba na kuanza masomo ya dini. Alipata daraja ya juu ya kielimu ya ijtihadi akiwa na umri wa miaka 24 na kuanza kufundisha katika vyuo vikuu vya kidini. Msomi huyo ameandika vitabu kadhaa vikiwemo vile vya Sherhe ya al Urwatul Wuthqaa na Dhakhiratul Ibaad.

Siku kama ya leo miaka 78 iliyopita inayosadifiana na 10 Julai 1940 Jemedari Henri Petain Waziri Mkuu wa muda na afisa wa ngazi ya juu wa jeshi la Ufaransa, alichukua uongozi baada ya Ufaransa kushindwa na Wanazi wa Ujerumani katika Vita vya Pili vya Dunia. Kwa mujibu wa mkataba wa kivita uliosainiwa na nchi mbili hizo tarehe 22 Juni 1940, eneo la kaskazini mwa Ufaransa, ukiwemo mji wa Paris lilibaki chini ya himaya ya jeshi la Manazi wa Ujerumani.
Miaka 45 iliyopita katika siku kama ya leo, visiwa vya Bahamas huko Amerika ya Kati vilipata uhuru kutoka Uingereza na siku kama ya leo hufahamika visiwani humo kama siku ya taifa. Visiwa vya Bahamas viligunduliwa mwaka 1492 na mvumbuzi wa Ulaya Christopher Columbus na kuwa chini ya himaya ya Uhispania. Visiwa vya Bahamas vilipata uhuru mwaka 1973 na kuwa mwanachama wa Umoja wa Mataifa. Visiwa vya Bahamas viko kaskazini mwa Cuba na kusini mashariki mwa Marekani.