Jul 12, 2018 23:42 UTC
  • Ijumaa tarehe 13 Julai 2018

Leo ni Ijumaa tarehe 29 Shawwal 1439 Hijria sawa na 13 Julai 2018.

Siku kama ya leo miaka 1954 iliyopita, moto mkubwa ulitokea huko Roma mji mkuu wa utawala wa kifalme wa Roma. Sehemu kubwa ya mji wa kihistoria na mkongwe wa Roma iliungua na wakazi wengi wa mji huo walipoteza maisha yao kutokana na moto huo. Moto huo ulikuwa kisingizio tosha kwa Nuren mtawala mmwagadamu wa Kirumi ambaye aliwauwa kwa umati watu zaidi ya laki moja na baadaye kuwatuhumu Wakristo kuwa ndio walioanzisha moto huo.

Siku kama ya leo miaka 618 iliyopita liliundwa jeshi la kale zaidi duniani nchini Uswisi. Jeshi hilo la kale zaidi duniani hadi hii leo lemebakia kama lilivyokuwa na hata mavazi ya wanajeshi wake hayajabadilika. Idadi ya wanajeshi wa jeshi hilo dogo lakini lenye nidhamu kubwa ni watu 83. Jeshi hilo ambalo wanachama wake daima huwa raia wa Uswisi, liliundwa kwa ajili ya kulinda viongozi wa Kikatoliki wa wakati huo na hii leo baada ya kupita zaidi ya miaka zaidi ya 600 tangu liundwe, jeshi hilo lina jukumu la kumlinda Papa wa Kanisa Katoliki huko Vatican.

Jeshi la Uswisi

Siku kama ya leo miaka 247 iliyopita, baharia na nahodha mashuhuri wa Kiingereza aliyejulikana kwa jina la James Cook alikamilisha safari yake ya kitafiti na kielimu ya kuelekea The Great Southern Continent. Safari hiyo ilikuwa imeanza tarehe 26 Julai mwaka 1768. Safari hiyo ndefu iliishirikisha pia timu ya watalaamu wa elimu ya Sayansi Asilia au Natural Science kwa kimombo. Wataalamu hao walikuwa na nia ya kufanya utafiti wa kielimu kuhusiana na mimea pamoja na viumbe wanaopatikana katika maeneo hayo.

James Cook

Na siku kama ya leo miaka 47 iliyopita inayosadifiana na 13 Julai 1971, watu wasiopungua 92 waliuawa akiwemo balozi wa Ubelgiji nchini Morocco, baada ya kutokea machafuko nchini humo. Machafuko hayo yalitokea baada ya kundi la waasi wa kijeshi kutoka chuo cha kijeshi cha Ahermoumou nchini Morocco kushambulia sherehe za kutimia miaka 42 ya kuzaliwa Mfalme Hassan wa Pili. Miongoni mwa majeruhi 133, alikuwemo Moulay Abdullah, ndugu wa mfalme wa Morocco.