Jumamosi, 15 Septemba, 2018
Leo ni Jumamosi tarehe 5 Mfunguo Nne Muharram 1440 Hijria mwafaka na tarehe 15 Septemba 2018 Miladia.
Siku kama ya leo miaka 1379 iliyopita sawa na tarehe 5 Mfunguo Nne Muharram mwaka 61 Hijria, Ubeidullah bin Ziyad baada ya kuwa ametuma jeshi la watu elfu moja kuelekea Karbala kwa ajili ya kupigana na Imam Hussein AS, alimtuma bwana mmoja aliyejulikana kwa jina la Zahr bin Qays akiwa na wapiganaji 500 waliopanda farasi na kumpa jukumu la kusimama katika daraja la Sadah katika mji wa Kufa na awazuie kupita hapo watu wote waliokuwa na nia ya kwenda kuungana na Imam Hussein AS. Bwana mmoja aliyejulikana kwa jina la Amir bin Abi Salamah akiwa na lengo la kwenda kuungana na Imam Hussein AS alilishambulia jeshi la Qays na kufanikiwa kupita katika daraja hilo na hakuna mwanajeshi wa Qays aliyekuwa na ujasiri wa kumfuata. Amir akafanikiwa kufikka Karbala na kuungana na Imam Hussein AS. ***

Katika siku kama ya leo miaka 197 iliyopita, nchi za Amerika ya Kati za Nicaragua, Honduras, el-Salvador, Guatemala na Costa Rica zilijitangazia uhuru kutoka kwa Uhispania. Baada ya Napoleone Bonaparte mtawala wa Kifaransa kuikalia kwa mabavu Uhispania na kudhoofika serikali ya kijeshi ya Madrid, nchi kadhaa za Latin America zikiwemo Nicaragua, Honduras, el-Salvador, Guatemala na Costa Rica zilijitangazia uhuru. Baada ya nchi hizo tano kujitangazia uhuru ziliunda Muungano wa Amerika ya Kati. Baada ya muungano huo kuvunjika mwaka 1838, nchi wanachama kila moja ilianza kujitawala na kujiendeshea mambo yake yenyewe. ***

Miaka 60 iliyopita katika siku kama ya leo, kwa mara ya kwanza katika historia ya elimu ya tiba, virusi vinavyosababisha ugonjwa hatari wa trakoma au mtoto wa jicho viligunduliwa. Kugunduliwa virusi hivyo kulienda sambamba na njia za kupambana na ugonjwa huo wa mtoto wa jicho, ambapo maelfu ya watu walikuwa wakiwa vipofu katika pembe mbalimbali duniani kutokana na maradhi hayo. Virusi vya trakoma viligunduliwa na matabibu wawili wa Kiingereza. ***
Na siku kama ya leo miaka 19 iliyopita, sawa na tarehe 24 mwezi Shahrivar mwaka 1378 Hijria shamsiya, alifariki dunia kwa maradhi ya moyo Dakta Abdulhussein Zarinkub mwanahistoria na mtafiti mashuhuri wa Kiirani. Dakta Abdulhussein alizaliwa mwaka 1301 Hijria Shamsiya katika mji wa Borujerd magharibi mwa Iran. Mwaka 1327 Hijria Shamsiya Dakta Zarinkub alitunukiwa shahada ya digrii katika taaluma ya historia na baadae akaendelea na masomo yake katika taaluma hiyo na kutunikiwa shahada ya udaktari. Mbali na historia msomi huyo wa Kiirani alipenda sana masomo ya fasihi ya lugha ya Kifarsi na irfani ya Kiislamu. Aidha aliandika vitabu na makala nyingi na moja kati ya vitabu vyake ni kile alichokiita "Alfajiri ya Uislamu." ***
