Jumanne, tarehe 6 Mei, 2025
Leo ni Jumanne tarehe 8 Dhulqaadah 1446 Hijria inayosadifiana na tarehe 6 Mei 2025.
Siku kama ya leo miaka 1098 iliyopita, alifariki dunia mjini Baghdad, Iraq Ibn Zubair, mwandishi mashuhuri wa Kiislamu wa wakati huo.
Katika ujana wake Ibn Zubair alisoma kwa baba yake elimu muhimu tofauti za wakati huo. Baada ya baba yake kufariki dunia aliutumia utajiri wa baba yake katika njia ya kutafuta elimu, kuasisi maktaba na kuwasaidia wanafunzi wa kidini waliokuwa na hali ngumu ya kimaisha. Mbali na uhodari mkubwa katika uandishi, Ibn Zubair alikuwa na kipawa cha kuandika upya baadhi ya vitabu vya wasomi wengine na kuvieneza.

Siku kama ya leo miaka 1067 iliyopita, alifariki dunia Abu Hamid Swaghani, mtaalamu wa nujumu na hesabati wa Iran.
Abu Hamid alizaliwa mjini Khurasan, kaskazini mashariki mwa Iran, na baadaye kuhamia mjini Baghdad Iraq. Msomi huyo alihesabika kuwa mmoja wa wasomi wakubwa katika uga wa elimu ya nujumu na hisabati wa zama zake sanjari na kuasisi kituo cha unajimu mjini Baghdad.
Msomi huyo ameacha vitabu vingi katika taaluma ya nujumu.

Siku kama ya leo miaka 1061 iliyopita, alifariki dunia mjini Baghdad, Ali bin Omar Daraqutni, mwandishi na mtaalamu wa sheria za Kiislamu.
Daraqutni alifanya safari nchini Misri na Sham na kusoma kwa wasomi wakubwa wa zama hizo. Aidha msomi huyo alikuwa hodari pia katika tafsiri ya Qur’ani Tukufu, fiq’hi, mashairi na fasihi ya lugha ya Kiarabu.
Miongoni mwa athari zake ni pamoja na vitabu vya ‘al-Sunan’, ambacho ni mashuhuri kwa jina la ‘Sunan Daraqutni’ na ‘al-Mukhtalif Wal-Mu’talif.’

Katika siku kama ya leo miaka 169 iliyopita, alizaliwa Czechoslovakia, Sigmund Freud daktari wa magonjwa ya akili na raia wa Austria.
Akiwa na umri wa miaka minne alihamia mjini Vienna akiwa na wazazi wake. Alipofikisha umri wa miaka saba alijiandikisha katika chuo kidogo cha udaktari ambapo akiwa na miaka 29 alitokea kuwa tabibu aliyebobea kutibu magonjwa ya akili.
Baada ya kutibu wagonjwa kadhaa wenye matatizo hayo alipata uzoefu mkubwa suala ambalo lilimsukuma kufanya majaribio kadhaa katika uga huo. Daktari huyo alifanya utafiti na kuchunguza matatizo mbalimbali ya kiakili yanayomkumba binadamu na kutoa maoni na nadharia mpya kuhusu chanzo cha magonjwa ya akili. Kwa sababu hiyo anahesabiwa kuwa mwasisi wa elimu ya uchunguzi wa kisaikolojia au Psychoanalysis.
Sigmund Freud alifariki dunia tarehe 23 Septemba 1939 akiwa na umri wa miaka 83 baada ya kupatwa na mshtuko wa moyo.

Siku kama ya leo miaka 166 iliyopita alifariki dunia mtaalamu wa masuala ya kimaumbile na msomi mkubwa wa Kijerumani, Alexander Humboldt.
Alizaliwa mwaka 1769 huko Berlin, Ujerumani. Alifanya safari ndefu katika mabara ya Asia na Amerika kwa ajili ya kufanya utafiti. Tafiti nyingi za msomi huyo zilihusu namna dunia ilivyoumbwa.

Tarehe 6 Mei miaka 143 iliyopita mtaalamu wa Ujerumani, Robert Heinrich Koch alitangaza habari ya kugunduliwa vijidudu maradhi vya ugonjwa wa kifua kikuu (TB).
Mtaalamu huyo wa masuala ya baiolojia alikuwa amegundua vijidudu maradhi hivyo ambavyo vimefupisha umri wa zaidi ya watu bilioni moja.
Baadaye Prf Robert Koch aligundua njia ya kufubaza na kutenga vijidudu maradhi hivyo ambavyo vilikuwa sugu mkabala wa dawa na vilikuwa na uwezo wa kujificha mwilini kwa miaka mingi na kujitokeza wakati mwafaka.
