Oct 01, 2018 23:03 UTC
  • Jumanne,  Oktoba 2,  2018

Leo ni Jumanne tarehe 22 Muharram 1440 Hijria sawa na Oktoba Pili, 2018.

Siku kama ya leo miaka 980 iliyopita alifariki dunia mmoja wa wasomi wakubwa wa Kiislamu, Sheikh Muhammad bin Hassan Tusi, ambaye ni mashuhuri kwa jina la Sheikhul Twaaifa. Sheikh Tusi alizaliwa katika mji wa Tus kaskazini mwa Iran na akaelekea Iraq kwa ajili ya kutafuta elimu ya juu baada ya kukamilisha elimu ya msingi. Alipata elimu kwa wanazuoni mashuhuri wa Iraq na miaka kadhaa baadaye akaweka msingi wa chuo kikuu cha kidini cha Najaf. Kituo hicho cha kidini kina historia ya miaka elfu moja na ni moja ya vituo muhimu mno vya elimu ya Kiislamu. Sheikh Tusi ameandika vitabu vingi sana katika taaluma mbalimbali. Miongoni mwa vitabu mashuhuri vya mwanazuoni huyo wa Kiislamu ni tafsiri ya Qur'ani tukufu ya al Tibyan na vitabu vya hadithi na fiqhi vya al Istibsar na al Tahdhiib.

Sheikh Muhammad bin Hassan Tusi

Tarehe Pili Oktoba miaka 114 iliyopita alizaliwa Graham Greene mwandishi wa Uingereza. Mwandishi huyo aliakisi matendo mema na mabaya katika athari zake na aliandika kwenye kitabu chake kinachoitwa 'Nguvu na Utukufu' kwamba subira, uvumilivu na mateso ni njia ya wokovu. Graham Greene ameacha vitabu vingi na baadhi ni 'Mtu wa Tatu', 'Utawala Unaotisha' na Muuaji wa Kukodishwa'. Mwandishi huyo Muingereza alifariki dunia mwaka 1991.

Graham Greene

Siku kama ya leo miaka 77 iliyopita sawa na tarehe Pili Oktoba 1941, Adolph Hitler kiongozi wa Ujerumani ya Kinazi alitoa amri ya kuanza kwa shambulizi la pili la jeshi la Ujerumani dhidi ya Urusi ya zamani. Kwenye vita vya kwanza dhidi ya Urusi vilivyoanza tarehe 22 Juni 1941, Ujerumani iliweza kuikalia kwa mabavu sehemu kadhaa za ardhi ya Urusi. Lengo la kufanywa shambulio hilo la Dikteta Hitler, lilikuwa ni kurahisisha operesheni za kijeshi, kudhoofisha nguvu za Jeshi Jekundu na kudhibiti ardhi zaidi za Urusi, na hasa Moscow mji mkuu wa nchi hiyo.

Adolph Hitler

Miaka 60 iliyopita katika siku kama ya leo inayosadifiana na tarehe Pili Oktoba 1958, nchi ya Guinea Conakry ilifanikiwa kujipatia uhuru wake kutoka kwa mkoloni Mfaransa. Wareno walianza kumiminika nchini Guinea mwishoni mwa karne ya 15, na ilipoanza karne ya 19, Wafaransa wakawa na satua zaidi nchini humo na ulipotimia mwaka 1849, nchi hiyo ikakoloniwa rasmi na Ufaransa. Guinea Conakry inapakana na nchi za Senegal, Mali, Ivory Coast, Liberia, Sierra Leone na Guinea Bissau.

Bendera ya Guinea