Nov 20, 2018 03:41 UTC
  • Jumanne 20 Novemba 2018

leo ni Jumanne 12 Rabiul Awwal 1440 Hijria sawa na tarehe 20 Novemba 2018.

Siku kama ya leo miaka 1493 inayosadifiana na tarehe 12 Mfunguo Sita Rabiul Awwal miaka 53 kabla ya Hijria, kwa kauli ya baadhi ya wanazuoni wa Kiislamu akiwemo Masoudi, alizaliwa Mtume Muhammad SAW. Wanachuoni wengine wa Kiislamu wanaamini kwamba, Mtume Muhammad (saw) alizaliwa tarehe 17 Rabiul Awwal mwaka huohuo. Kwa msingi huo, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ilitangaza kipindi cha kuanzia tarehe 12 hadi 17 Rabiul Awwal kila mwaka kuwa ni Wiki ya Umoja kati ya Waislamu kote duniani. Wiki ya umoja ni fursa nzuri ya kuzikurubisha nyoyo za Waislamu na kuimarisha umoja na mshikamano wao katika kukabiliana na maadui wa ulimwengu wa Kiislamu.

Tarehe 12 Rabiul Awwal mwaka wa kwanza Hijria, Mtume Muhammad (saw) aliweka jiwe la msingi la ujenzi wa msikiti wa kwanza kabisa katika Uislamu katika kijiji cha Quba kilichoko pambizoni mwa Madina. Mtume (saw) aliweka jiwe la msingi la msikiti huo wa kihistoria wakati aliposimama kwa siku chache katika eneo la Quba akiwa njiani kutoka Makka na kuelekea Madina. Mtukufu huyo alisimama kwa muda katika kijiji cha Quba akimsubiri Ali bin Abi Twalib na jamaa wa familia ya Mtume.

Msikiti wa Quba

Katika siku kama ya leo tarehe 12 Rabiul Awwal miaka 1199 iliyopita, alifariki dunia Imam Ahmad bin Hanbal mmoja kati ya maulamaa wakubwa wa Kiislamu katika mji wa Baghdad, Iraq ya leo. Ahmad bin Hanbal alizaliwa mwaka 124 Hijria, katika mji wa Baghdad na kupata elimu ya kidini katika mji huo kutoka kwa maulamaa wakubwa akiwemo Imam Shafii. Imam Hanbal alifanya safari katika miji kadhaa kama vile Kufa, Basra, Makka, Madina, Sham na Yemen kwa minajili ya kukusanya hadithi za Bwana Mtume SAW. Ahmad bin Hanbal ndiye mwasisi wa madhehebu ya Kisuni ya Hanbal na mwandishi wa kitabu mashuhuri cha hadithi cha al Musnad.

Ahmad bin Hanbal

Siku kama ya leo miaka 83 iliyopita, Sheikh Izzuddin Qassam ambaye alikuwa miongoni mwa viongozi wa harakati ya mapambano ya ukombozi wa wananchi wa Palestina dhidi ya uvamizi wa Wazayuni maghasibu na ukoloni wa Uingereza, aliuawa shahidi. Baada ya kukamilisha masomo yake ya awali huko Syria, Sheikh Qassam aliendeleza masomo yake katika Chuo Kikuu cha al Azhar huko Misri. Wananchi wa Palestina walianza mapambana dhidi ya mkoloni Mwingereza mwaka 1930 chini ya uongozi wa Sheikh Izzuddin Qassam. Hata hivyo baada ya kupita miaka kadhaa Wazayuni maghasibu walishirikiana na wakoloni wa Kiingereza na kumuuwa kigaidi kiongozi huyo wa harakati ya mapambano ya Palestina.

Sheikh Izzuddin Qassam

Na siku kama hii la leo miaka 68 iliyopita kwa mara ya kwanza kabisa nchi mbili za Marekani na China zilikabiliana uso kwa uso katika vita vya Korea. Sababu ya mapigano baina ya nchi hizo mbili ilikuwa uungaji mkono wa Marekani kwa Korea Kusini na himaya na uungaji mkono wa China na Urusi kwa Korea Kaskazini. Viya ya Korea ilisababisha hasara kubwa kwa pande zote mbili. hatima vita hiyo ilisimamishwa kwa upatanishi wa Umoja wa Mataifa na peninsula ya Korea iliendelea kugawanywa pande mbili hadi hii leo.