Nov 24, 2018 02:42 UTC
  • Jumamosi, 24 Novemba, 2018

Leo ni Jumamosi tarehe 16 Mfunguo Sita Rabiul Awwal 1440 Hijria, mwafaka na tarehe 24 Novemba 2018 Miladia.

Siku kama ya leo miaka 1439 iliyopita kwa mujibu wa baadhi ya mapokezi ya historia, Swala ya kwanza ya Ijumaa iliswaliwa na Mtume Muhammad (saw) baada ya mtukufu huyo kuhama kutoka Makka. Baada ya kuwasili katika eneo la Bani Salim bin Auf lililokuwa likijulikana kwa jina la Quba karibu na Madina wakati wa adhuhuri, Mtume (saw) alitoa hotuba na kusimamisha Swala ya Ijumaa mahala hapo. Wanahistoria wanasema  kuwa, hiyo ilikuwa Swala ya kwanza ya Ijumaa katika Uislamu. Hatua hiyo pia inaonesha umuhimu wa ibada hiyo ya kiroho na kisiasa ambayo Bwana Mtume aliamua kuitekeleza mara tu baada ya kuwasili karibu na mji wa Madina.  Aidha inaelezwa kuwa, mahala paliposwaliwa Swala ya kwanza ya Ijumaa na Mtume SAW, baadaye palijengwa msikiti ambao bado upo hadi leo. ***

Swala ya Ijumaa

Miaka 386 iliyopita katika siku kama ya leo, Baruch de Spinoza mwanafalsafa na mtaalamu wa elimu jamii wa Uholanzi alizaliwa. Spinoza alisoma kwa bidii na kukwea daraja za kielimu. Hata hivyo ukosoaji wake kwa dini ya Kiyahudi ulimfanya akabiliwe na chuki na hasama za maulama wa dini hiyo. Njia na fikra za kifalsafa na Spinoza zilikaribiana na itikadi za kisufi. Msomi huyo wa elimu ya falsafa wa Uholanzi ameandika pia vitabu kadhaa kama The Philosophy of Spinoza na The Road to Inner Freedom.***

Baruch de Spinoza

Katika siku kama ya leo miaka 187 iliyopita, Michael Faraday mwanafizikia stadi wa Kiingereza aligundua mkondo wa umeme unaojulikana kitaalamu kama ''Electric Current''. Kwa ugunduzi huo Faraday akawa amefanikiwa kupiga hatua kubwa katika elimu ya fizikia. Faraday alizaliwa mwaka 1791 na awali alikuwa akifanya kazi katika duka la kuuza vitabu. Ni kipindi hicho ndipo taratibu alipoanza kusoma vitabu mbalimbai na kuanza kuvutiwa na masuala ya kielimu. Miaka michache baadaye akawa msaidizi wa maabara. Akiwa katika maabara hiyo Faraday alifanya utafiti mwingi kuhusiana na jinsi ya kutengeneza balbu za umeme. Miongoni mwa mafanikio mengine makubwa yaliyoletwa na mtaalamu huyo ni pale alipogundua mota ya umeme pamoja na kubadilisha nguvu za sumaku kuwa nguvu za umeme. ***

Michael Faraday

Miaka 112 iliyopita katika siku kama ya leo ambayo ni sawa na tarehe 3 Azar mwaka 1285 Hijria Shamsia, gazeti la 'Majlis' lililokuwa na kurasa 8 lilianza kuchapishwa nchini Iran. Mhariri Mkuu wa gazeti hilo alikuwa Adib al-Mamalik Farahani ambaye alikuwa miongoni mwa waandishi mashuhuri wa zama hizo. Mbali na gazeti hilo kuandika habari za ndani na nje ya nchi, liliakisi pia mazungumzo yote ya Majlisi ya Ushauri yaani Bunge la Iran. ***

Gazeti la Majlis

Na miaka mitano iliyopita katika siku kama ya leo ya tarehe 24 Novemba, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ilitiliana saini makubaliano ya muda na nchi tano wanachama wa kudumu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa pamoja na Ujerumani katika uwanja wa miradi ya amani ya nyuklia ya Iran. Makubaliano hayo yalitiwa saini huko Geneva Uswisi. Kutiwa saini makubaliano hayo kulifungua njia ya mazungumzo baina ya Iran na nchi za kundi la 5+1 yaani Marekani, Uingereza, Ufaransa, China, Russia pamoja na Ujerumani kwa ajili ya kutiwa saini makubaliano jumla ya kuondoa suutahafamu zote kuhusu miradi ya nyuklia ya Iran na kuondolewa vikwazo vyote vya kidhalimu vya kimataifa na vya pande kadhaa. Hatimaye  makubaliano ya nyuklia ya Mpango Kamili wa Pamoja wa Utekelezaji (JCPOA) yalitiwa saini Julai 2015 baina ya Iran na kundi la 5+1***

 

Tags