Nov 27, 2018 15:07 UTC

Ni matumaini yangu kuwa hamjambo wapenzi wasikilizaji na karibuni kutegea sikio sehemu ya 10 ya kipindi hiki kipya cha Katika Maktaba ya Imam Khomein (MA) ambacho kinakujieni kwa mnasaba wa miaka 40 ya Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran.

Katika kipindi kilichopita tulisema kuwa, uadilifu katika hukumu una maana kwamba, mtu  anayevirejea vyombo vya mahakama kwa ajili ya kupata haki yake, anapasa kufikia lengo lake hilo bila kusumbuliwa. Kwa ibara nyingine ni kwamba, hali na mazingira ya vyombo vya mahakama, hayapasi kupelekea watu waakose imani ya kupeleka malalamiko yao kwa vyombo hivyo. 

Ndugu wasikilizaji moja ya aina za uadilifu wa kimahkama katika mtazamo wa Imam Khomeini (AS) ni kuchungwa haki za raia na hata watuhumiwa na wahalifu na kadhalika kujiepusha na kufurutu ada na kupoteza haki za wengine. Kwa mfano tu, katika miaka ya mwanzoni mwa Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran, na kama yalivyo mapinduzi mengine duniani, baadhi ya wanamapinduzi waliwafuatilia na kuwaadhibu vibaraka wa utawala uliotangulia na hivyo kuandaliwa uwanja kwa baadhi ya watu wenye misimamo mikali kukiuka haki za baadhi ya watuhumiwa hususan wale waliokuwa wakishirikiana na utawala huo. Katika hilo, baadhi ya majaji ambao waliteuliwa na Imam Khomeini katika wadhifa huo kwa ajili ya kutoa hukumu na kuchunguza mali na fedha za vibaraka wa utawala uliotangulia, sambamba na kutoa hukumu za kifo au adhabu kali na kadhalika kufilisi sehemu ya mali za vibaraka hao, walitumia vibaya nafasi zao hizo kukiuka haki za vibaraka hao, ambapo kutokana na hali hiyo, Imam Khomeini kwa kutumia busara katika kudhibiti hali ya mambo na misimamo hiyo mikali, alitoa radiamali kali na hivyo akazuia mwenendo huo ambao ulionekana kukiuka misingi ya uadilifu ya dini ya Kiislamu. Katika uwanja huo Imam Khomeoni alisema: "Mahakama ni lazima ziwe na vigezo halisi vya Uislamu….Kadhia ya kutaifisha mali za mtu, ni suala ambalo kwa mtazamo wangu lina vigezo ambapo inatakiwa ijulikane wazi kwamba mtuhumiwa alipata mali zake zote kwa njia ya wizi, hiana, utapeli na mfano wa hayo, lakini iwapo mtu kwa mfano alikuwa ni mwanachama wa Shirika la Intelijinsia na Usalama wa Taifa la Iran, SAVAK au wakili wa bunge, ni suala linalofahamika kuwa mtu huyo huenda alikuwa na mali. Katika hali hiyo, haifai kuwanyang'anya mali zao kwa kuwa wana wake na watoto, na pia wana maisha." Mwisho wa kunukuu.

*******

Aina nyingine ya uadilifu na usalama wa mahakama katika mtazamo wa Imam Khomeini (MA) ni kuheshimu mipaka ya mtu binafsi ambapo kwa mtazamo wake, hata kama atakuwa walii mtawala wa sheria, naye hana haki ya kukiuka mipaka ya mtu mwingine na iwapo kwa kibri na matamanio yake ataamua kufanya hivyo, basi atakosa sifa ya kuwa walii mtawala. Hata kama iwapo haki hiyo itagongana na haki nyingine iliyo na umuhimu zaidi nayo ni haki ya kijamii, ni haki hiyo ya kijamii ndiyo inayopasa kupewa kipaumbele cha kwanza, lakini msingi ni kutoingilia masuala ya ndani ya watu binafsi. Imam Khomeini baada ya kufahamu kwamba, baadhi ya watu na asasi zilikuwa zikitekeleza zikikiuka haki za baadhi ya watu kwa kutumia vibaya hisia kali za kimapinduzi, alitoa amri kali ya kukomeshwa hali hiyo kupitia vipengee vinane ambavyo alivitoa mwezi Azar 1361 Hijiria Shamsia, yaani sawa na mwezi Disemba 1982 Miladia, ambavyo msingi wake ulikuwa ni kuheshimiwa haki za raia.

********

Kama kwanza ndio unafungulia redio yako, kipindi kilicho hewani ni sehemu 10 ya mfululizo wa vipindi vinavyozungumzia kiini na kichochezi cha Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran chini ya usimamizi wa Imam Khomeini (MA), kinachokujieni kupitia Idhaa ya Kiswahili Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. 

Aidha kwa mujibu wa amri hiyo, Imam Khomeini aliyasisitizia majeshi yote ya Iran kuwa ni jambo lisiloruhusiwa kukamata na kuwazuia watu bila kuwafikisha mahakamani, kutumia mali zinazohamishika na zisizohamishika za watuhumiwa, kuingia ndani ya nyumba, duka au maeneo yao ya kazi katika kufanya uchunguzi wa kosa bila ya kibali cha mahakama, kusikiliza mawasiliano ya simu ya watu na kufanya ujasusi isipokuwa tu kwa ajili ya kubaini njama za maadui dhidi ya mfumo wa Kiislamu. Yote hayo ni miongoni mwa mambo yaliyosisitizwa na mtukufu huyo katika dikrii ya vipengee vinane kwa lengo la kuhakikisha kwamba uadilifu wa majaji unazingatia haki za wananchi katika mazingira hayo ya kimapinduzi. Ili kutekelezwa amri hiyo muhimu, kuliundwa kitengo maalumu kwa lengo la kushughulikia suala hilo.

******

Kadhalika mwezi mmoja baadaye, yaani mwezi Dei 1361 Hijiria Shamsia, sawa na Januari 1983, Imam Khomeini (MA) alitoa amri mpya ya kuvunjwa kwa bodi za uajiri wa wafanyakazi nchi nzima, kwa kuwa kwa mujibu wa taarifa za kiintelejensia zilizomfikia Imam na kadhalika uchunguzi wa kina na vitabu vilivyoandikwa na bodi hizo, utendajikazi wake ulikuwa ukikiuka mipaka binafsi ya watu katika jamii na hivyo kutia doa usalama wa raia. Katika kipindi chote cha uhai wake, Imam Khomein kwa kutaka kutekelezwa vyema dikri mbili hizo, alikuwa akifuatilia kwa karibu utekelezaji wake na kutoa maelekezo ya lazima kwa viongozi husika. Imam alitoa amri za moja kwa moja kwa vyombo vya mahakama na mihimili mingine ya utekelezaji, kwa ajili ya kuzifanya kuwa za Kiislamu sheria na majukumu ya kiutawala, ambapo aghlabu ya amri hizo zilihusu udharura wa kutoingilia uga wa mtu binafsi na kuhifadhiwa pamoja na kulindwa usalama wa raia na uhuru wao binafsi, hususan usalama na uadilifu wa mahakama. Katika moja ya barua hizo za Imam Khomeini (MA) aliitaka mihimili yote ya serikali kutekeleza sheria za Kiislamu katika sekta zote za serikali hususan vyombo vya mahakama na udharura wa kutumiwa hukumu za Mwenyezi Mungu katika mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu, badala ya hukumu za kitwaghuti za utawala uliopita, hasa katika uga wa kuheshimiwa haki za mtu binafsi.

Wapenzi wasikilizaji sehemu ya 10 ya kipindi hiki cha Katika Maktaba ya Imam Khomeini (MA) ambacho kinakujieni kwa mnasaba wa kutimia miaka 40 ya Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran na kupitia Idhaa ya Kiswahili, Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, inaishia hapa kwa leo. Mimi ni Sudi Jafar, kwaherini.