Jul 04, 2019 11:51 UTC

Ni matumaini yangu kuwa hamjambo wapenzi wasikilizaji na karibuni kutegea sikio sehemu ya 30 ya kipindi hiki cha Katika Maktaba ya Imam Khomein (MA) ambacho kinakujieni kupitia Idhaa ya Kiswahili Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Katika kipindi kilichopita tulisema kuwa, moja ya misingi iliyopewa umuhimu na Imam Khomeini (MA) ni suala zima la kuwaunga mkono watu waliofanywa wanyonge na pia kuziunga mkono harakati zinazopigania kujikomboa. Tukasema kuwa suala hilo ni ukamilishaji wa msingi wa kupambana na ubeberu na dhulma. Leo pia tutaendelea kufafanua suala hilo, hivyo endeleeni kuwa pamoja nami hadi mwisho wa kipindi hiki.

Akiendelea kubainisha suala hilo, Imam Khomeini (MA) anasema: “Ni lazima tuwaunge mkono watu walionyongeshwa duniani, kwa kuwa malengo ya Uislamu ni kuwaunga mkono watu wote wanyonge duniani.” Usia wake katika kitabu cha Sahifeh Nur juzu ya 12 ukurasa wa 20. Kwa hakika msingi huo wa kidini ndio ule ule unaosisitizwa na aya ya 75 ya Surat Nisaa inayosema: “Na mna nini msipigane katika njia ya Mwenyezi Mungu na yale ya waoonewa (wanaonyongeshwa) miongoni mwa wanaume na wanawake na watoto ambao wanasema: Mola wetu Mlezi tutoe katika mji huu ambao watu wake ni madhalimu na tujaalie tuwe na mlinzi anayetoka kwako na utujaalie tuwe na wa kutunusuru anayetoka kwako.” 

Serikali ya Iran inawaunga mkono watu madhaifu duniani hususan Wapalestina

Ni kwa kuzingatia jambo hilo, ndipo katiba ya Jamhuri ya Kiislamu ya katika mapambano yake na ubeberu na ukoni, ikaitaka serikali kuwaunga mkono watu dhaifu duniani pamoja na harakati za kupigania uhuru. Kipengee cha 154 cha katiba hiyo kinasema: “Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inaunga mkono mapambano ya wale waliodhoofishwa dhidi ya mabeberu iwe ni katika eneo au duniani.”

******

Kama kwanza ndio unafungulia redio yako, kipindi kilicho hewani ni sehemu ya 30 ya mfululizo wa vipindi vinavyofafanua nadharia ya Imam Khomeini (MA), kuhusu Mapinduzi ya Kiislamu, kinachokujieni kupitia Idhaa ya Kiswahili Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Ndugu wasikilizaji moja ya misingi mingine iliyopewa uzingatiaji na Imam Khomeini katika uga wa siasa za kigeni ni kuwaunga mkono na kuwatetea Waislamu. Katika mtazamo wa mtukufu huyo, kwenye mapambano dhidi ya mabeberu na kuunga mkono juhudi za wanyonge mkabala wa mabeberu, kuna udharura wa uungaji mkono wa utawala wa Kiislamu kwa jamii ya Waislamu na kutetea haki zao kupitia njia chanya. Hii ni kwa kuwa kiuhalisia wa mambo, Waislamu wote na jamii zao zilizotengana za Kiislamu, wanaunda umma mmoja ambao serikali ya Kiislamu ina wajibu wa kuunga mkono umma huo na kuutetea. Kuhusiana na suala hilo, Imam Khomeini (MA) anasema: “Sisi ni ndugu wa Waislamu wote na huo ni moja ya misingi ya Kiislamu ambapo kwayo kila Mwislamu anatakiwa kuwasaidia ndugu zake Waislamu.” Usia wake katika kitabu cha Sahifeye Nusr juzu ya 3 ukurasa wa 31. Na katika sehemu nyingine Imam Khomeini anasema: “Kupitia msingi wa kulinda umoja na kuunga mkono maslahi ya nchi na mataifa ya Kiislamu, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inapendelea kutoa msaada kwa nchi hizo za Kiislamu wakati zinapokuwa katika matatizo.” Usia wake katika kitabu cha Sahifeye Nur juzuu ya 11 ukurasa wa 265.

Harakati za muqawama za Palestina ambazo zinasaidiwa na Iran ya Kiislamu

Kwa hakika mtazamo wa Mwasisi huyo wa Mapinduzi ya Kiislamu juu ya ulazima wa kuwaunga mkono Waislamu duniani unatokana na aya za Qur’an Tukufu na kauli za Mtume na Maimamu watofaharifu (as). Kwa mfano tu aya ya 10 ya Suratul-Hujarat inasema: “Hakika waumini ni ndugu, basi patanisheni baina ya ndgu zenu na mcheni Mwenyezi Mungu ili mrehemewe.” Aidha Mtukufu Mtume (saw) anasema: “Atakayeamka huku akiwa hazingatii masuala ya Waislamu, basi sio Mwislamu na mtu ambaye atasikia sauti ya kuomba msaada ya Mwislamu mwenzake, lakini akaacha kuitikia, basi sio Mwislamu.” Usulul-Kafi juzu ya 3 ukurasa wa 242. Aidha Imam Swadiq (as) amenukuliwa akisema: “Mfano wa muumini kwa ndugu yake muumini ni sawa na mwili mmoja ambao pindi kiungo kimoja kinapopata maumivu, basi viungo vingine vya mwili huhisi maumivu.” Usulul-Kafi juzu ya 3 ukurasa wa 239. Msimamo huo wa kidini wa Imam Khomeini (MA) ndio unaozingatiwa katika katiba ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ambayo inasema: “Kuzingatiwa udugu kati ya Waislamu na kuzingatiwa suala la kutetea haki za Waislamu wote wa dunia, ni mambo ambayo serikali imesisitiziwa kuyatekeleza.”

******

Kwa mtazamo wa Imam Khomeini (MA), uungaji mkono na msaada kwa Waislamu ni mambo ambayo yako katika ngazi tatu za kivitendo na utekelezaji. Mosi ni katika ngazi ya umma wa Kiislamu na ulimwengu wa Kiislamu kwa namna ya kusaidia harakati za mwamko na za kupigiania uhuru wao wa Kiislamu kama vile kuiunga mkono harakati ya Kiislamu ya Hizbullah ya nchini Lebanon dhidi ya utawala haramu wa Kizayuni.

Waislamu duniani wakiwemo wa Myanmar nao wanatetewa na Iran

Na pili ni kuunga mkono na kuwatetea Waislamu ambao wako katika mapambano dhidi ya makafiri katika kutetea haki zao za kimsingi kama vile harakati ya Jihadul-Islami ya wananchi wa Palestina ndani ya ardhi ya nchi yao ya Palestina. Na tatu ni kutetea haki za jamii ya wachache ya Waislamu katika nchi zisizokuwa za Kiislamu ambao nao wanadhulumiwa na kukandamiwa na serikali zao kama vile kusaidia jamii ya wachache ya Kiislamu katika nchi za Ulaya na Marekani. Ndugu wasikilizaji kama mnavyoona, msingi wa siasa za kigeni zilizozingatiwa na Imam Khomeini ulivuka mipaka ya maslahi ya kitaifa na ndani ya nchi tu, na kuchukua upeo mpana  zaidi wa kibinaadamu na kidini.

Wapenzi wasikilizaji sehemu ya 30 ya kipindi hiki cha Katika Maktaba ya Imam Khomeini (MA) ambacho kimekujieni kupitia Idhaa ya Kiswahili, Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, inaishia hapa kwa leo. Mimi ni Sudi Jafar, kwaherini.

 

 

Tags