Jul 04, 2019 12:09 UTC

Ni matumaini yangu kuwa hamjambo wapenzi wasikilizaji na karibuni kutegea sikio sehemu ya 32 ya kipindi hiki cha Katika Maktaba ya Imam Khomein (MA) ambacho kinakujieni kupitia Idhaa ya Kiswahili Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Katika kipindi kilichopita tuliishia katika nukta ya umuhimu wa kutoingilia masuala ya ndani ya nchi nyingine na kwamba jambo hilo ni kati ya masuala yaliyosisitizwa sana na Imam Khomeini (MA). Pia tukasema kuwa, mtazamo huo wa Imam unatokana na mafundisho ya dini ya Uislamu. Katika kipindi cha leo tutaendelea kufafanua suala hilo hivyo endeleeni kuwa pamoja nami hadi mwisho wa kipindi hiki. Ndugu wasikilizaji baadhi ya wafasiri wa Qur'an wamezitaja aya za 90 na 91 za Surat Nisaai, kuwa chimbuko la kujitenga ambapo kwa mujibu wake nchi zinatakiwa kutoingilia masuala ya ndani ya nchi nyingine. Katika uwanja huo Imam Khomeini anasema: "Serikali ijayo itatakiwa kutoegemea upande wowote katika uga wa  mahusiano na mataifa mengine, bali itatakiwa iwe na uhusiano mwema na mataifa yote kwa namna ya uadilifu, madamu tu uhusiano wa pande mbili uwe mzuri."

Iran inapinga kuingilia masuala ya ndani ya nchi nyingine

Ndugu wasikilizaji Mwasisi wa Mapinduzi ya Kiislamu, alikutaja kupenda amani na kuchunga heshima ya pande mbili na kutoingilia masuala ya ndani ya nchi nyingine kuwa msingi wa siasa za mfumo wa Kiislamu, na ni kutokana na hali hiyo ndipo katiba ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na katika vifungu tofauti, ikaitaka serikali kujiepusha kikamilifu na kila aina ya uingiliaji katika masuala ya ndani ya mataifa mengine. Hata hivyo swali ambalo linaweza kujitokeza ni hili kwamba, ni vipi mambo mawili yanayoonekana kugongana kidhahiri yanaweza kufungamanishwa sehemu moja katika siasa za kigeni? Yaani kuwaunga mkono watu waliodhulumiwa na pia kuwatetea Waislamu duniani na wakati huo huo kutoingilia masuala ya ndani ya nchi nyingine. Kwa ibara nyingine ni kwamba ni vipi watu wanyonge na Waislamu wataungwa mkono katika nchi nyingine bila ya kuingilia masuala ya ndani ya nchi husika?

*******

Ili kuondoa mgongano huo wa kidhihiri, kuna udharura wa kuzingatia nukta muhimu katika mtazamo wa Imam Khomeini (MA) nayo ni kwamba uungaji mkono na msaada kwa watu hao ni wa kimaanawi na sio uingiliaji wa moja kwa moja. Ukweli ni kwamba Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imekuwa ikifanya jitihada za kuwaunga mkono wanyonge na Waislamu duniani kupitia asasi na taasisi za kimataifa na vilevile kutumia njia za amani na udiplomasia.

Taifa la Iran kama linavyokataa kuingilia masuala ya ndani ya nchi nyingine, pia inapambana na ubeberu wa Marekani

Kifungu cha 154 cha katiba ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran pia kimeelezea kutogongana masuala hayo kwa kusema: "Jamhuri ya Kiislamu ya Iran huku ikijiepusha na uingiliaji wowote wa masuala ya ndani ya mataifa mengine, itaunga mkono mapambano ya watu wanyonge dhidi ya mabeberu katika pembe zote za dunia."

**********

Kama kwanza ndio unafungulia redio yako, kipindi kilicho hewani ni sehemu ya 32 ya mfululizo wa vipindi vinavyofafanua nadharia ya Imam Khomeini (MA), kuhusu Mapinduzi ya Kiislamu, kinachokujieni kupitia Idhaa ya Kiswahili Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Ndugu wasikilizaji moja ya misingi ambayo ilizingatiwa sana na Mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika uga wa siasa za kigeni ni kuheshimu mikataba na sheria za kimataifa. Msingi huo ulipewa umuhimu na Imam Khomeini ikiwa ni katika kulinda usalama na uthabiti wa kimataifa. Katika uwanja huo, Imam Khomeini alisema: "Kwa kuzingatia kuwa sisi tunafuata dini ya Kiislamu, tutaheshimu mikataba iliyofikiwa." Hotuba ya Imam Khoneini ya tarehe 22/11/1359 Hijiria Shamsia.

Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Nyuklia (IAEA), miongoni mwa taasisi ambazo zinakiri kuwa Iran ni mtekelezaji wa ahadi na mikataba ya kimataifa

Kwa kuzingatia msingi huo, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran pia ikiwa mwanachama anayewajibika wa jamii ya kimataifa daima imekuwa ikiheshimu mikataba, sheria, makubalino na mapatano ya kimataifa. Kuheshimiwa vipengee vya makubaliano ya mwaka 1975 kati ya Iran na Iraq, taarifa ya 1359 kati ya Iran na Marekani baada ya kuibuka mgogoro wa utekaji nyara, na kadhalika uanachama wa Mkataba wa Kuzuia Uzalishaji na Uenezaji wa Silaha za Atomiki (NPT) na mkataba wa hivi karibuni kabisa wa Mpango Kamili wa Pamoja wa Utekelezaji (JCPOA) ambao licha ya ukwamishaji mambo wa Marekani, lakini Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imeendelea kuuheshimu na kuutekeleza, ni mifano michache tu ambayo inathibitisha namna Iran inavyoheshimu na kutekeleza sheria na mikatana ya kimataifa. Msimamo huo wa Imam na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, kama ilivyokuwa misimamo tuliyoijadili katika vipindi vilivyopita, unatokana na mafundisho ya kidini ambayo inasisitiza kuheshimiwa sheria na mikataba. Na hii ni kwa kuwa katika dini ya Uislamu, kutekeleza ahadi kwa mtu binafsi, kijamii na kisiasa, ni jambo ambalo limepewa umuhimu mkubwa na dini, ambapo kumetajwa kuwa ni moja ya alama za imani. Mwishoni mwa aya ya 177 ya Suratul-Baqarah Mwenyezi Mungu anasema: “….Na wanaotimiza ahadi yao wanapoahidi na wanaovumilia katika shida na madhara na wakati wa vita, hao ndio waliosadikisha na hao ndio wacha-Mungu.”

Mapatano ya kimataifa ya JCPOA ambayo licha ya kufikiwa kwa tabu kubwa, lakini Marekani iliyakiuka mwaka 2018

Aidha aya na riwaya nyingi zimesisitiza ulazima na wajibu wa kuheshimiwa ahadi na mikataba ima ya kisiasa au ya kijamii katika ngazi za kimataifa. Aidha aya na riwaya hizo zinabainisha umuhimu wa kuheshimiwa mikataba na ahadi kati ya Waislamu na wasiokuwa Waislamu, kama ambavyo Mtume Muhammad (saw) anavyosema wazi kuwa: “Haifai kutotekeleza ahadi iwe kwa Mwislamu au kwa kafiri.” Kitabu cha Nahjul-Fasaha Ukurasa wa 847.

Wapenzi wasikilizaji sehemu ya 32 ya kipindi hiki cha Katika Maktaba ya Imam Khomeini (MA) ambacho kimekujieni kupitia Idhaa ya Kiswahili, Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, inaishia hapa kwa leo. Mimi ni Sudi Jafar, kwaherini.