Jul 04, 2019 11:31 UTC

Katika kipindi kilichopita tuliendelea kuzungumzia umuhimu wa kipindi cha ujana na nafasi yake athirifu katika kuilea nafsi na kujirekebisha vijana. Kadhalika tulibainisha kwamba Imam Khomeini (MA) aliwapa usia vijana akiwataka kutumia vizuri neena ya kipindi cha ujana katika kunufaika vizuri na matukufu ya duniani na Akhera.

Ndugu wasikilizaji, Imam Khomeini aliutaja mwamko wa wananchi wa Iran kuwa ni moja ya matukio muhimu yaliyoyoathiriwa na ushiriki wa vijana katika jamii na kuhusiana na hilo aliwataka vijana hao kutambua vyema nafasi na majukumu yao. Imam alisema: "Nyinyi vijana wenye nguvu, nyinyi vijana wenye imani, nyinyi vijana hatua zenu ndizo zilizofanikisha ushindi huu. Ninakushukuruni nyote ambao kwa kutumia nguvu zote, irada yote na kwa uwezo wa Mwenyezi Mungu nyote mliamka na kuweka kando kazi zenu zote na mkaamua kufuatilia jambo hili ambalo ni wadhifa wetu sote. Alama ya ushindi ni umoja wenu." Hotuba ya Imam tarehe 14/12/1357. Kadhalika Imam Khomeini hakutambua nafasi chanya ya vijana kuwa inaishia tu kwenye Ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu, bali aliamini kwamba msingi wa kukatwa ufisadi na kuiokoa nchi viko mikononi mwa watu ambao hawatawatenga vijana katika ulingo wa Mapinduzi Alisema:

Vijana ambao Imam Khomeini (MA) aliwataka kuwa makini na wasifuate kibubusa umagharibi

 "Kwa hima yenu ya juu nyinyi vijana na matabaka yote ya watu wa Iran mmeufikisha hapa mwamko huu. Ni hima yenu ya juu ndiyo iliyotufanya tukafanikiwa kupata ushindi na kuweza kukata mizizi ya ufisadi. Na Inshallah (Mwenyezi Mungu akipenda) kuanzia sasa na kuendelea, kwa hima yenu ya juu nyinyi vijana, tutafanikiwa kukata kikamilifu mizizi ya ufisadi. Ni nyinyi ambao damu yenu ilimwagwa nchi nzima. Ni nyinyi ambao kwa kujitolea kwenu mmeweza kuuokoa Uislamu kutoka mikononi mwa maajnabi na maadui wake. Na ni nyinyi ndio ambao kwa umoja na uwezo wenu, Uislamu mmeuondoa kutoka kwa watu mahaini ambao walikuwa wakieneza chembe chembe za unafiki kati ya matabaka ya wananchi." Hotuba ya Imam tarehe 17 1/1358.

**********

Kama ndio kwanza unafungulia redio yako, kipindi kilichoko hewani ni sehemu 28 ya mfululizo wa vipindi vinavyozungumzia nadharia na mitazamo ya Mwasisi wa Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran yaani Imam Khomeini (MA), kinachokujieni kupitia Idhaa ya Kiswahili Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Kadhalika mwanachuoni huyo aliitaja nafasi ya vijana katika Mapinduzi ya Kiislamu kwamba ni sawa na muujiza wa Mwenyezi Mungu uliodhihiri kwa wanadamu na kwamba wamethibitisha uwezo wao wa kusimama imara mbele ya madola ya kiistikbari na kibeberu duniani kwa kusema: "Nyinyi vijana watukufu mmethibitisha kwamba mnaweza kusimama imara mbele ya madola ya kibeberu na mnaweza kuilinda nchi yenu….. Nyinyi mmethibitisha kwamba mnaweza kufikia kile mnachokihitaji. Mmeifikishia dunia muujiza ambao ni muujiza wa Mwenyezi Mungu kwa mwanadamu. Mmesimama mbele ya madola yote ya kibeberu ambayo yalikuwa yanataka kuitwaa Iran na kumeza thamani zake. Mlipambana na hatimaye mkashinda." 

Jamii ya vijana wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ambayo ilikuwa na mchango mkubwa katika Ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu

Hotuba ya Imam Khomeini ya tarehe 10/12/1360. Kadhalika Imam Khomeini aliashiria nafasi chanya na ya kimapambano ya vijana dhidi ya udikteta wa watawala wa ndani na pia muqawama wao mbele ya wakoloni wa kigeni na madola ya kiistikbari duniani na kusisitiza kuwa ni nafasi hiyo ni ya kupigiwa mfano na ni kigezo bora kwa wanyonge wote duniani. Amesema: "Mapambano yenu nyinyi vijana Waislamu imara wa Iran ambayo kwa kutumia umoja na mshikamano wenu yameweza kukata mikono ya madola ya kigeni, ni ya kupigiwa mfano kwa ajili ya watu wote wanyonge duniani." Hotuba ya Imam ya tarehe 2/2/1358. Aidha alisisitiza kuwa Mapinduzi ya Kiislamu yameleta mabadiliko makubwa kwa vijana wa Iran ambapo kwa baraka za mwamko huo yameweza kuleta fursa nyingi kwa wananchi na kuwaondoa katika haramu haramu kwa kusema: "Tunamshukuru Mwenyezi kwamba mabadiliko makubwa yamepatikana katika jamii na katika nchi yetu. Na vijana wetu ambao walikuwa wakifanya kazi zisizo za kisheria wameondolewa huko na kuingizwa katika huduma za kumtumikia Mwenyezi Mungu Mtukufu. Tunatakiwa kuziunga mkono juhudi hizi za vijana. Tangu mwanzo tulikuwa tukitegemea nguvu za wananchi na vijana." Hotuba ya Imam ya tarehe 8/8/1358.

*********

Imam Khomeini (MA) aliyaelezea mabadiliko katika roho za vijana kuwa ni yenye umuhimu mkubwa kuliko mabadiliko ya mapinduzi ndani ya jamii kwa kusema: "Mabadiliko haya ambayo yapo kwa vijana wetu yamepatikana kwa watu wale ambao wametoa ahadi madhubuti kwa Mwenyezi Mungu. Umuhimu wake ni zaidi ya mabadiliko ambayo yamepatikana nchini kwetu." Hotuba yake ya tarehe 12/10/1358. Kadhalika alikutaja kumtegemea Mwenyezi Mungu kuwa ni chanzo na sababu kuu ya kupatikana mabadiliko hayo kwa vijana kuelekea kwenye utakaso wa nafsi na kujilea kwa akhlaqi njema ndani ya kipindi kifupi ambapo matunda yake yalikuwa ni kuwavutia vijana kwenye kumtumikia Mwenyezi Mungu na kufikia daraja ya juu ya kupenda kufa shahidi katika njia ya Allah. Imam Khomeini alisema: "Watu ambao wanakusudia kuzilea na kuzitakasa nafsi zao, hufanya juhudi kwa miaka 50  na ni baada ya hapo ndio huweza kufikia daraja angalau moja. Lakini vijana hawa Mwenyezi Mungu ameweza kuwabadilisha ndani ya kipindi kifupi na kuweza kufikia daraja ya juu ambayo wale waliofanya juhudi kwa miaka 50 hawakuweza kuifikia. Hii ni kwa kuwa, bila ya tawfiki ya Mwenyezi Mungu hakuna chochote kinachoweza kufikiwa. Mabadiliko haya hayawezi kutambuliwa na kambi ya Mashariki wala ya Magharibi." Hotuba ya Imam Khomeini tarehe 23/3/1361.

Malezi ya vijana yanatakiwa kuanzia tangu utotoni

Aidha mwanachuni huyo mkubwa wa zama hizi aliyatambua mabadiliko ya kiroho na kimaanawi ya vijana kuwa ni ya kipekee katika Mapinduzi ya Kiislamu ikilinganishwa na mapinduzi mengine yaliyojiri duniani na alisema: “Mapenzi na msaada maalumu wa Mwenyezi Mungu Mtukufu ndio ulioleta mabadiliko kwa wananchi hawa katika uwanja wa kimaanawi, kwa vijana kutoka katika hali yao ya zamani na kuelekea kwenye hali mpya ya Kiislamu. Na kutambua kuwa kwa kupitia Uislamu, wanatakiwa kufanikisha ushindi wa Mapinduzi. Iwapo suala hili lisingefikiwa, basi mapinduzi ya hapa (Iran) yangekuwa sawa na mapinduzi mengine ya dunia ambayo wenyewe mnaweza kuona hatima yake.” Hotuba ya Imam Khomeini ya tarehe 21/11/1364.

************

Kwa kuzingatia nadharia ya wataalamu wanaofuatilia matatizo yanayoikabili jamii ya vijana, Imam Khomeini aliwataka vijana hao kujiepusha sana na kuzama katika dimbwi la utumiaji wa madawa ya kulevya hususan Heroin, kama ambavyo pia alisisitiza kwamba ugawaji wa mihadarati hiyo na mingineyo ni katika njama zilizoratibiwa na wakoloni kwa lengo la kulifanya tabaka la vijana kuwa  la watu wasilojitambua wala lisiloweza kufuatilia maendeleo ya nchi yao.

Wapenzi wasikilizaji sehemu ya 28 ya kipindi hiki cha Katika Maktaba ya Imam Khomeini (MA) ambacho kinakujieni kwa mnasaba wa kutimia miaka 40 ya Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran na kupitia Idhaa ya Kiswahili, Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, inaishia hapa kwa leo. Mimi ni Sudi Jafar, kwaherini.  

 

 

Tags