Jul 04, 2019 11:38 UTC

Ni matumaini yangu kuwa hamjambo popote pale mlipo wakati huu. Ninakukaribisheni tena kusikiliza kipindi hiki cha Katika Maktaba ya Imam Khomeini (MA) kinachokujieni, siku na saa kama hii, kupitia Idhaa ya Kiswahili Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran hii ikiwa ni sehemu ya 29. 

Katika kipindi kilichopita tuliendelea kufafanua miongozo na nasaha za Imam Khomeini kwa vijana ambapo pia alisisitiza kwamba, uenezwaji la mihadarati na madawa ya kulevya vilivyokuwa vikishuhudiwa katika miaka ya mwanzo nchini Iran zilikuwa ni njama za wakoloni za kutaka kulisahaulisha tabaka la vijana na masuala muhimu ya nchi yao. Leo pia tutaendelea kufafanua suala hilo hivyo endeleeni kuwa pamoja nami hadi mwisho wa kipindi hiki.

Ndugu wasikilizaji Imam Khomeini (MA) alielezea njama hizo za wakoloni katika kueneza madawa ya kulevya kwa vijana kwa kusema: “Msichukulie suala hili kwamba limetokea ghafla tu kwa kumuona mtu anauza mkononi madawa ya kulevya aina ya Heroin na huku kundi jingine likiwa limeathirika na madawa hayo. Bali jambo hili pia ni moja ya njama zilizoratibiwa na madola makubwa ambayo yanatumia suala hilo kama njia ya kutoa pigo kwa tabaka la vijana. Hii ni kwa kuwa kwa njia hiyo wataweza kudhibiti uchumi wetu na hatimaye wataweza kwa kuwatumia vijana hao kuharibu misingi bora ya kiutamaduni, kimfumo na kisiasa. Hii ni moja ya njama za kuwadhoofisha vijana. Mtu sahihi hawezi kufikiria kutumia madawa ya kulevya katika siasa, wala hawezi kupiga hatua za kiuchumi iwapo tabaka la watu fulani limeathirika na wala hawezi pia kushiriki vita akiwa na jamii ya namna hiyo.” Hotuba yake ya tarehe 5/10/1358.

Wamagharibi wanafanya njama chafu kujaribu kuwarubuni vijana wa Iran, lakini njama zao zimekuwa zikigonga mwamba

Kadhalika mwanachuoni huyo daima alikuwa akiwaonya sana vijana wasikubali kuathiriwa na propaganda chafu zinazoenezwa dhidi ya dini au dhidi ya mfumo wa Kiislamu nchini Iran na katika uwanja huo alisema: “Ni lazima vijana wetu wafahamu kwamba propaganda zozote zinazolenga moja ya nembo za Uislamu, kwa hakika propaganda hizo zinaratibiwa na madola makubwa na wasaliti vibaraka kwa lengo la kuisambaratisha dini ya Kiislamu. Alhamdulillah vijana wetu ni Waislamu na ni wanaharakati wazuri, hivyo ni lazima wafahamu kwamba ni jukumu lako kuzipinga vikali nara zozote zinazolenga kuuchafua Uislamu.” Hotuba ya Imam Khomeini ya tarehe 14/8/1359 Hijiria Shamsia.

******

Kama ndio kwanza unafungua redio yako, kipindi kilicho hewani ni sehemu 29 ya mfululizo wa vipindi vinavyozungumzia nadharia na mitazamo ya Mwasisi wa Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran yaani Imam Khomeini (MA), kinachokujieni kupitia Idhaa ya Kiswahili Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Kadhalika Imam Khomeini (MA) aliutambua uhuru wa fikra na kujieleza kuwa ni haki ya vijana na katika uwanja huo alitoa mwito kwa maualama na wasomi wa kidini kuwafungulia milango vijana ambao wanahoji masuala tofauti kuuhusu Uislamu. Imam Khomeini alisema: “Ninapenda kusisitiza na kuwakumbusha maulama na shakhsia wa kidini wa leo kwamba akthari ya vijana na wasomi wanahisi uwepo wa anga ya uhuru ndani ya Iran ya Kiislamu na kwamba sasa wanaweza kuhoji maudhui na masuala tofauti ya Kiislamu, hivyo wanatakiwa kuwafungulia milango na kusikiliza maswali yao, sambamba na kujibu vyema na kuwaonyesha upendo na urafiki wa Kiislamu. Na ni lazima wazingatie nukta hii kwamba, haifai kufumbia macho mapenzi na hisia zao za kimaanawi na kiirfani na badala yake wafanye haraka kuondoa aina ya upotovu uliokita mizizi kwenye mioyo ya watu hao na kuwaondolea shaka waliyo nayo.” Hotuba yake ya tarehe 29/4/1367 Hijiria Shamsia.

Vijana wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran

Mbali na hayo Imam Khomeini (MA) aliutambua wadhifa wa maulama, wasomi wa dini na wahadhiri wa vyuo vikuu kuwa ni kufanya juhudi kubwa kwa ajili ya kuwalea vyema vijana na katika uwanja huo alisema tena kwamba: “Sisi wa upande wa dini na ninyi upande wa vyuo vikuu, ni wabeba dhima mbele ya Mwenyezi Mungu Mtukufu kwa ajili ya vijana hawa kwani tunatakiwa kuwafanya kuwa watu wema, watu wenye uchungu kwa nchi yao, wenye kuitumikia dini ya Kiislamu, waaminifu kwa nchi yao na wasiwe wahaini.” Hotuba ya Imam tarehe 21/3/1358 Hijiria Shamsia.

********

Katika sehemu nyingine Imam Khomeini aliitaja hali ya kukata tamaa kuwa ni moja ya majeshi ya shetani yanayolenga kuwavunja moyo vijana na hivyo aliwataka vijana hao kujinasua na vishawishi hivyo vya shetani kwa kusema: “Moja ya askari wa ibilisi ni kukatisha tamaa katika masuala ambayo mwanadamu anatakiwa kuwa na matumaini, matarajio na kufanya kazi kwa bidii. Lakini shetani huwa anazusha hali ya kukatisha tamaa, hivyo kwa kuzusha hali ya kukatisha matumaini kwa vijana hususan katika masuala ambayo vijana hao wanatakiwa wawe na uamuzi sahihi, (shetani huyo) huwa amepiga hatua ya kufanikisha anayoyataka kupitia kuwalemaza vijana.” Hotuba yake ya tarehe 30/4/1358. Kadhalika mwanachuoni huyo mwanaharakati sambamba na kuwapongeza vijana wanamichezo akiwatajana kuwa ni nembo muhimu ya kupambana na hali ya kukata tamaa, aliwataka vijana hao kujiweka sawa kimwili na kiroho kwa kusema: “Mwili na roho vinapokuwa na nguvu, jambo hilo huleta nguvu nyingine ya kimwili katika kumsukuma mtu kwenye kufanya kazi. Wakati nguvu hizo mbili zinapokutana huunda mwanadamu mkamilifu.” Hotuba ya Imam Khomeini ya tarehe 8/3/1358 Hijiria Shamsia.

Wapenzi wasikilizaji sehemu ya 29 ya kipindi hiki cha Katika Maktaba ya Imam Khomeini (MA) ambacho kinakujieni kwa mnasaba wa kutimia miaka 40 ya Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran na kupitia Idhaa ya Kiswahili, Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, inaishia hapa kwa leo. Mimi ni Sudi Jafar, kwaherini.  

 

 

Tags