Dec 19, 2018 12:00 UTC

Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur'ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SW, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu.

Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur'ani. Hii ni darsa ya 794 na sura tunayoizungumzia hivi sasa ni ya 36 ya Ya-Sin. Tunaianza darsa yetu kwa aya ya 36 ambayo inasema:

سُبْحَانَ الَّذِي خَلَقَ الْأَزْوَاجَ كُلَّهَا مِمَّا تُنبِتُ الْأَرْضُ وَمِنْ أَنفُسِهِمْ وَمِمَّا لَا يَعْلَمُونَ

Subhana, Ametakasika, aliye umba jozi katika kila vinavyo mea katika ardhi na katika nafsi zao, na katika wasivyo vijua. 

Katika darsa iliyopita tulisoma aya zilizozungumzia baadhi ya ishara za Tauhidi na Upekee wa Allah SW katika maumbile. Aya hii inaendeleza maudhui hiyo kwa kuashiria moja ya misingi muhimu inayotawala katika mfumo wa uumbaji, yaani kanuni ya vitu kuwa jozi ya vitu viwili tofauti na kueleza kwamba: Mwenyezi Mungu amejaalia mimea, wanyama na watu kuwa na jozi ya viwili viwili tofauti, na nyinyi mnajua hivyo. Kanuni hiyo inatawala katika vitu vingine pia lakini nyinyi hamjui. Mungu mwenye uwezo kama huo katika uumbaji, na akahakikisha idadi ya viumbe inaongezeka kwa njia ya kuchanganyika mbegu tofauti za jozi ya kike na kiume, ametakasika na kila ila, kasoro na upungufu na wala hahitaji mshirika au msaidizi katika uumbaji. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba Mungu ambaye ni Muumba wa jozi za vitu ametakasika na sifa ya kuwa na mwenza au mshirika katika ulimwengu. Yeye ni wa pekee na asiye na mfanowe. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa mwanadamu yuko sawa na viumbe wengine katika masuala ya kimwili na ghariza za kimaumbile; na katika hilo hana ubora kwa viumbe wenzake. Aidha tunajielimisha kutokana na aya hii kwamba elimu na ujuzi wa mwanadamu una mpaka, na kuna mambo mengi katika hakika za ulimwengu wa maumbile ambazo hajaweza kuzigundua.

Tunaiendeleza darsa yetu kwa aya ya 37 hadi ya 40 ambazo zinasema:

وَآيَةٌ لَّهُمُ اللَّيْلُ نَسْلَخُ مِنْهُ النَّهَارَ فَإِذَا هُم مُّظْلِمُونَ

Na usiku ni Ishara kwao. Tunauvua humo mchana, mara wao wanakuwa gizani.

وَالشَّمْسُ تَجْرِي لِمُسْتَقَرٍّ لَّهَا ۚ ذَٰلِكَ تَقْدِيرُ الْعَزِيزِ الْعَلِيمِ

Na jua linakwenda kwa kiwango chake. Hayo ni makadirio ya Mwenye nguvu, Mwenye kujua. 

وَالْقَمَرَ قَدَّرْنَاهُ مَنَازِلَ حَتَّىٰ عَادَ كَالْعُرْجُونِ الْقَدِيمِ

Na mwezi tumeupimia vituo, mpaka unakuwa kama karara kongwe.

لَا الشَّمْسُ يَنبَغِي لَهَا أَن تُدْرِكَ الْقَمَرَ وَلَا اللَّيْلُ سَابِقُ النَّهَارِ ۚ وَكُلٌّ فِي فَلَكٍ يَسْبَحُونَ

Haliwi jua kuufikia mwezi, wala usiku kuupita mchana. Na vyote vinaogelea katika njia zao.

Aya hizi zinaashiria harakati yenye nidhamu maalumu ya sayari mbili za mbinguni yaani jua na mwezi ambazo Mwenyezi Mungu amezipangia njia au mzingo mahususi na kuziwekea kiwango na kasi ya mwendo wao kwa kipimo na kiwango maalumu. Mwanadamu hujionea kwa macho yake mbinguni mwezi wakati wa usiku na jua wakati wa mchana. Nukta ya kuvutia ni kwamba harakati ya jua, mwezi na sayari ya dunia katika mizingo yao ziliyopangiwa imenadhimiwa kwa namna ambayo haitokei katu sayari hizo tatu kugongana wala kutokea mparaganyiko wowote katika mfumo wa maumbile. Maumbile ya sayari ya dunia ni ya hali ya giza, kwa sababu haina nuru na mwangaza unaotokana na sayari yenyewe. Ile sehemu ya sayari ya dunia inayoelekeana na jua huwa na mwangaza kutokana na kuangaziwa na mwanga wa jua. Kinachotokea hasa ni kwamba, jua linapochomoza, siku katika upande wa sayari ya dunia unaopatwa na mwangaza huo huwa ndio inaanza. Lakini wakati sayari hiyo inapoendelea na harakati ya kujizunguka yenyewe jua huanza kuzama kidogo kidogo, na sayari ya dunia kugubikwa tena na giza. Ni kama kwamba mwanga wa jua ni mithili ya guo jeupe ambalo linatanda kila siku juu ya dunia, na wakati jua linapozama linatanduka juu ya sayari hiyo. Tab'an wakati wa usiku pia Mwenyezi Mungu hakutaka wakazi wa ardhini wabaki kwenye giza totoro mutlaki. Kwa hivyo amekiweka kioo kikubwa mbele ya jua kiitwacho mwezi ili kupitia kioo hicho, sehemu ya mwanga wa jua uendelee kuangazia sayari ya dunia. Mwezi ni mithili ya taa ya kulalia, ambayo kwa mbaamwezi yake huwapa raha na utulivu wakazi wa sehemu ya ardhini iliyogubikwa na guo la usiku. Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba mfumo unaotawala katika maumbile, harakati ya mwezi na jua pamoja na sayari ya dunia, kuingia na kutoka usiku na mchana pamoja na vitu vingine vya maumbile ni miongoni mwa ishara za Mwenyezi Mungu Mjuzi na Mweza. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa njia ya harakati na kasi ya mzunguko wa jua, mwezi na dunia vinafanyika kwa kipimo na mahesabu makini na yaliyokamilika. Hakuna shaka yoyote kwamba hayo si mambo yanayotokea kwa sadfa na bila ya ratiba na mpango maalumu. Wa aidha tunajielimisha kutokana na aya hizi kwamba hali za mwezi kuanzia unapokuwa na umbo la hilali au mwezi mchanga hadi kufikia mwezi kamili zinafanyika kwa tadbiri na uendeshaji wa Mwenyezi Mungu mwenye hekima. Kwa mujibu wa aya nyingine za Qur'ani, hali tofauti za umbo la mwezi ni kalenda ya maumbile ya kuhesabia masiku, miezi na miaka.

Darsa yetu ya leo inahitimishwa na aya ya 41 hadi 44 ambazo zinasema:

وَآيَةٌ لَّهُمْ أَنَّا حَمَلْنَا ذُرِّيَّتَهُمْ فِي الْفُلْكِ الْمَشْحُونِ

Na ni Ishara kwao kwamba Sisi tuliwapakia dhuriya zao katika jahazi ilio sheheni. 

وَخَلَقْنَا لَهُم مِّن مِّثْلِهِ مَا يَرْكَبُونَ

Na tukawaumbia kutoka mfano wake wanavyo vipanda.

وَإِن نَّشَأْ نُغْرِقْهُمْ فَلَا صَرِيخَ لَهُمْ وَلَا هُمْ يُنقَذُونَ

Na tukitaka tunawagharikisha, wala hapana wa kuwasaidia, wala hawaokolewi,

إِلَّا رَحْمَةً مِّنَّا وَمَتَاعًا إِلَىٰ حِينٍ

 Isipo kuwa kwa rehema zitokazo Kwetu na starehe kwa muda. 

Aya hizi zinaashiria vitu vikubwa kadhaa katika ulimwengu wa maumbile kama bahari na bahari kuu na kueleza kwamba merikebu ndogo na mameli makubwa yanayosafirisha mizigo na watu ni miongoni mwa ishara za uwezo wa Mola Muumba. Sababu ni kwamba Allah SW ameyaumba maji kwa namna ambayo ujazo wa mizigo na wasafiri ndani ya meli na majahazi unabebeka ndani yake bila ya tabu yoyote na kuvifanya vyombo hivyo vielee na kukata masafa ya karibu na ya mbali kabisa kwenye maji bila ya kuzama. Tab'an kuna nyenzo nyingine za uchukuzi ambazo baadhi yao ni viumbe wa Mwenyezi Mungu kama ngamia na baadhi ya nyama hoa wengine, lakini katika dunia ya sasa iliyoendelea, na licha ya kuwepo anuai za magari, ndege na treni uchukuzi na usafirishaji wa kiwango kikubwa zaidi cha mizigo unafanyika kupitia baharini kwa kutumia meli. Kama leo hii meli zinazobeba shehena za vyakula na bidhaa nyingine zinazohitajiwa na watu au zile zinazokata maji ya bahari zikiwa zimebeba shehena za mafuta, zitasita kufanya kazi, maisha ya wanadamu yatakabiliwa na matatizo makubwa. Kwa hivyo, kama Allah SW atayaondolea maji sifa hiyo yaliyonayo, meli na majahazi yote yaliyosheheni mizigo na watu walioabiri ndani yake yataghariki na kuzama baharini na hakuna yeyote yule ghairi ya Yeye Mola awezaye kuwaokoa. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba vyombo vya uchukuzi na usafirishaji vya nchi kavu na baharini ni miongoni mwa mahitaji ya kimaumbile na ya msingi ya wanadamu ambayo kwa hekima na ukarimu wake Mola, amewaandalia viumbe hao mazingira mwafaka kwa ajili ya utumiaji wa vitu hivyo. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kututaka tujue kwamba neema tulizonazo zinatokana na ukarimu na ihsani ya Allah, si haki tunayostahiki kuipata. Kwa hivyo tusiingiwe na ghururi kwa neema tulizo nazo kwa sababu yumkini zikawa sababu ya kughadhibikiwa na Mola. Wapenzi wasikilizaji, darsa ya 794 ya Qur'ani imefikia tamati. Tunamwomba Allah atuwezeshe kuitumia kila aina ya neema aliyotujaalia katika njia sahihi na kwa namna inayomridhisha Yeye. Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.