Dec 31, 2018 07:12 UTC
  • Ulimwengu wa Spoti, Disemba 31

Mkusanyiko wa matukio muhimu ya spoti ndani ya siku saba zilizopita, kitaifa na kimataifa....

Soka U23: Iran yakubali sare na Jordan

Timu ya taifa ya soka ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ya vijana wenye chini ya umri wa miaka 23 ililazimishwa sare ya bao 1-1 na Jordan katika mchuano wa kirafiki Jumanne iliyopita. Kwenye mechi hiyo iliyopigwa mjini Irbid, nchini Jordan, wenyeji walifunga bao la mapema kupitia mchezaji Hadi al Hourani na kuwa kifua mbele kwa dakika kadhaa.

Wachezaji wa Iran wakishangilia bao

 

Timu hiyo ya mabarobaro wa Iran inayofahamika kama "Omid" au matumaini, ilisawazisha mambo kupitia mshambuliaji Vahid Namdari, kunako dakika ya 30. Hapo kabla, timu hiyo ya Iran iliichachafya Syria mabao 3-1 katika mchuano mwingine wa kirafiki, uliopigwa siku ya Ijumaa ya wiki iliyopita. Mabao ya timu hiyo ya Iran yalifungwa na Vahid Namdari, Alireza Arta na Mohammad Reza Azadi. Vijana hao wa mkufunzi Zlatko Kranjcar wanatumia michuano hii ya kirafiki kama sehemu ya maandalizi ya michuano ya Mabingwa wa Asia itakayoandaliwa na Shirikisho la Soka Asia AFC mwaka 2020.

Wanyanyua uzani wa Iran wazoa medali kibao Bahrain

Wanamichezo wa kunyanyua vitu vizito (uzani) wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran wamezoa medali kochokocho, zikiwemo dhahabu 4 katika mashindano ya kikanda ya mchezo huo yanayoendelea katika mji mkuu wa Bahrain, Manama. Kwa mujibu wa tovuti rasmi ya Shirikisho la Unyayuaji Uzani la Iran, Payman Dehqani wa timu ya Jeshi la Nchi Kavu la Iran ameishindia Iran ya Kiislamu dhahabu tatu katika safu za wanyanyua uzani wenye kilo 55, 79 na 115. Dhahabu nyingine ya Iran ilitwaliwa na Mohammad Hussein Golparvar katika kategoria ya kilo 89.

Mnyanyua uzani wa Iran

 

Muirani ni wa 2 Sataraji ya Dunia

Bingwa wa mchezo wa sataraji au chesi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Sarah Khadimu Sharia ameibuka wa pili katika mashindano ya dunia ya mchezo huo, katika mji wa St. Petersburg nchini Russia. Binti huyo wa Kiirani ameibuka mshindi wa pili kwa nyingine tena mwaka huu, baada ya kunyakua alama 13 kwa 17. Raia wa Russia ameibuka kidedea kwa alama 13.5, huku Mchina akifunga orodha ya 3 bora kwa alama 12.5.

Sarah Khadimu Sharia

 

Waziri wa Michezo na Vijana wa Iran, Masoud Soltanifar amempongeza mwanasataranji huyo wa Kiiran kwa kufanya vyema katika mashindano hayo ya kimataifa ya 'World Rapid and Blitz Championships.'

Droo ya CAF

Droo ya upangaji ratiba na makundi ya Ligi ya Klabu Bingwa Barani Afrika ilifanyika Ijumaa usiku ya Disemba 28 mjini Cairo, nchini Misri, ambapo wawakilishi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla, klabu ya Simba wameorodheshwa katika Kundi D pamoja na Al-Ahly ya Misri, JS Saoura ya Algeria na AS Vita Club ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Kwa klabu hiyo kutinga hatua ya makundi, tayari imejihakikishia dola 550,000, kiasi ambacho kitakuwa kinaongezeka kadri timu hiyo itakavyofanya vyema katika hatua hiyo. Ikumbukwe kuwa, Simba imefuzu kwenye hatua hii mara baada ya kuwatoa klabu ya Nkana FC kutoka nchini Zambia kwa jumla ya mabao 4-3 katika michezo yote miwili waliocheza nyumbani na ugenini. Mwaka 1974, Simba ilinguruma hadi nusu fainali ya Klabu Bingwa (Ligi ya Mabingwa) na kutolewa na Mehalla al-Kubra ya Misri, rekodi ambayo haijawahi kufikiwa na klabu yoyote ile ya Tanzania. Mashabiki wa Simba wanaendelea kuipongeza timu hiyo kwa kuandika historia ya kutinga hatua ya makundi baada ya zaidi ya muongo mmoja.

CAF ikitangaza Droo ya Ligi ya Mabingwa Afrika

 

Ghairi ya Simba, timu nyingine za kanda ya Afrika Mashariki zimeshindwa kufuza katika michuano ya klabu bingwa na ile ya Kombe la Shirikisho Afrika, zikiwemo KCCA ya Uganda, Gor Mahia ya Kenya na Mukura ya Rwanda, ambazo kwa sasa zinatarajiwa kucheza hatua ya mwisho ya mtoani ya Taji la shirikisho. Katika droo hiyo ya Disemba 28, Kundi A inazijumuisha Lobi Stars ya Nigeria, Waydad Athletic ya Morocco, Mimosas ya Kodivaa na Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini. Katika Kundi B, Platinumz FC ya Zimbabwe imejumuishwa pamoja na Horoya AC ya Guinea, EST ya Tunisia na Orlando Pirates ya Afrika Kusini.

Kombe la Mapinduzi

Michuano ya Kombe la Mapinduzi inatarajia kuanza kutifua mavumbi Januari Mosi, 2019 na kumalizika Januari 13, visiwani Zanzibar. Michuani hii itahusisha timu tisa ambazo zitawekwa kwenye makundi mawili huku kundi A likiwa na timu nne na kundi B timu tano.  Kundi A litakuwa na timu za Chipukizi, Mlandege, KMKM na Simba, huku kundi B likihusisha bingwa mtetezi wa michuano hiyo katika mwaka uliopita klabu ya Azam FC, Malindi, Yanga, Jamhuri na KVS. Azam wanatarajia kushuka dimbani Januari 2 kuvaana na Jamhuri, huku Yanga wakitupa karata yao ya kwanza Januari 3 watakapowavaa KVS. Kwa upande wa Simba watacheza dhidi ya Chipukizi Januari 4. Taarifa kutoka kwa kamati ya maandalizi ya michuano hiyo imeeleza kuwa mshindi wa kwanza wa michuano hiyo atazawadia kiasi cha Shilingi milioni 15 milioni, medali za dhahabu pamoja na kombe.

Ligi ya EPL

Na tunafunga kipindi kwa kutupia jicho baadhi ya mechi za Ligi Kuu ya Soka nchini Uingereza. Tuanze na michuano ya Jumapili, ambapo klabu ya Machester City iliisasambua Southampton mabao 3-1 katika mchezo uliopigwa katika uwanja wa St. Mary. City ndio walikuwa wa kwanza kuona nyavu, kupitia goli la mapema la David Silva, alilotia kimyani dakika 10 tu baada ya kupulizwa kipenga cha kuanza ngoma. Southampom walisawazisha mambo na kuwa 1-1 kunako dakika ya 37, lakini City wakapangua mambo tena kwa bao la Ward-Prowse katika dakika za kuhesabika kabla ya kumalizika kipindi cha kwanza. City walipigilia msumari wa mwisho kwenye jeneza la mahasimu wao, kupitia goli la Sergio Aguero katika dakika za ziada kwenye kipindi cha kwanza.

Kombe na EPL na baadhi ya wachezaji

 

Aidha siku ya Jumapili Manchester United waliifanya vibaya Bournemouth kwa kuichabanga mabao 4-1 wakiupigia nyumbani Old Trafford. Kana kwamba alitaka kuonesha dunia kwamba kiwango chake cha soko kilididimizwa kwa kiasi Fulani na uhasama kati yake mkufunzi wake aliyetimuliwa Jose Mourinho, mchezaji Paul Pogba alipachika wavuni mabao 2 ya aina yake katika dakika za 5 na 33. Marcus Rashford aliwaongezea Mashetani Wekundu la tatu kabla ya kumalizika kipindi cha kwanza, huku Romelu Lukaku, akifunga la nne katika dakika ya 72. Bao la kufutia machozi la Bournmouth lilipacikwa kimyani na kiungo Ake. Aidha Jumapili Chelsea iliizaba Crystal Palace bao moja la uchungu bila jibu, wakati ambapo West Ham ilikuwa inapokea kichapo cha mabao 2-0 kutoka Burnley.

Hata hivyo mchuano ulioibua gumzo ni ule wa Ijumaa, ambapo Liverpool ilishuka dimbani kuvaana na Arsenal. Hata hivyo bunduki za Gunners zilifanikiwa kufyatua risasi moja tu, na mkabala wake waligaragazwa mabao 5. Mchezaji Roberto Firmino ndiye aliyekuwa nyota wa mchuano huo, kwani aliwafungia Majogoo wa Mjini mabao 3 ya hatrrick, katika dakika za 14, 16 na 65 kupitia mkwaju wa penati aliyoachiwa na Mohammed Salah. Kabla ya kumalizika kipindi cha kwanza Salah alikuwa ameshacheka na wavu kupitia mkwaju mwingine wa penati. Bao jingine la Liverpool lilifungwa na Sadio Mane kunako dakika ya 32. Huenda bao la mapema la Arsenal lililofungwa na Ainsley Maitland ndilo lililoamsha ghadhabu za Majogoo wa Mjini, waliowaonesha kuwa kutangulia sio kufika na kuwatia skulini.

Stamfor Bridge, Uwanja wa Chelsea

 

Chelsea na Arsenal, wapo katika nafasi ya nne na tano mtawalia katika msimamo wa ligi na wameachwa nyuma kwa alama 11 na Liverpool. Liverpool, ndiyo timu pekee mpaka sasa ambayo haijapoteza mchezo katika Ligi ya Premia, na katika mchuano wake ujao watavaana na Newcastle United katika dimba la Anfield. Liverpool wapo kileleni mwa msimamo wa ligi kwa sasa wakiwa na alama 54, wakifuatiwa na City wenye alama 47. Tottenham kwa sasa wanafunga orodha ya tatu bora wakiwa ana alama 45.

……………………TAMATI………………..

 

 

Tags