Jumatatu 31 Disemba 2018
Leo ni Jumatatu tarehe 23 Rabiuthani 1440 Hijria sawa na Disemba 31 mwaka 2018.
Tarehe 10 Dei miaka 24 iliyopita yaani tarehe 31 Disemba mwaka 1994 Idhaa ya Kiswahili ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ilianza kazi kwa shabaha ya kufikisha sauti na ujumbe wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran kwa wazungumzaji wa lugha hiyo. Matangazo ya Idhaa hii yalianza sambamba na sherehe ya kubaathiwa na kupewa utume Nabii Muhammad (saw). Matangazo ya Idhaa ya Kiswahili Redio Tehran yanahusu masuala ya kisiasa, kijamii, kiuchumi na kadhalika.
Kwa sasa unaweza kuyasikiliza matangazo yetu kwa njia ya moja kwa moja na kupitia hifadhi ya matangazo wakati wowote. Unaweza pia kuyapata matangazo ya Idhaa ya Kiswahili Radio Tehran kupitia simu ya mkononi bila ya kutoa malipo yoyote isipokuwa gharama zako za kawaida za Intaneti kupitia njia ya kupakua aplikesheni ya matangazo yetu katika Google Play au App Store wakati tunapokuwa hewani.

Katika siku kama ya leo miaka 19 iliyopita, Rais Boris Yeltsin wa Russia aliondoka madarakani na nafasi yake ikachukuliwa na Vladimir Putin. Kipindi fulani Yeltsin alikuwa Katibu Mkuu wa Chama cha Kikomunisti. Boris Yeltsin alichaguliwa kuwa Rais wa Russia Januari mwaka 1991 na alikuwa akiungwa mkono na madola ya Magharibi. Hata baada ya kusambaratika Umoja wa Sovieti mwishoni mwa mwaka 1991, aliendelea kuwa Rais wa Russia akitumai kwamba, kwa kutumia misaada ya kifedha ya Magharibi angeweza kuiokoa nchi hiyo kutokana na matatizo ya kiuchumi yake ya kiuchumi. Kinyume na matarajio yake, viongozi wa madola ya Magharibi hawakutekeleza ahadi zao, hali iliyopelekea siasa za Rais Boris Yeltsin kushindwa. Kushambuliwa kijeshi eneo lililotangaza kujitawala la Chechnia na kukaliwa kwa mabavu ardhi hiyo na majeshi ya Russia, ni miongoni mwa matukio yaliyojiri katika kipindi cha utawala wa Boris Yeltsin nchini Russia.

Miaka 143 iliyopita katika siku kama ya leo Arthur Christensen mtaalamu wa masuala ya Mashariki alizaliwa huko Copenhagen mji mkuu wa Denmark. Christensen alionyesha hamu kubwa ya kujifunza masuala ya Mashariki hususan historia ya Iran na mwishoni mwa masomo yake, alifanya utafiti kuhusu historia ya fasihi ya Irani. Arthur Christensen aliweza kujifunza vyema lugha ya Kifarsi. Mojawapo ya vitabu vyake muhimu ni kile alichokipa jina la "Iran katika Zama za Wasasani." Christensen aliaga dunia mwaka 1945 Miladia.

Katika siku kama ya leo miaka 191 iliyopita, yaani tarehe 31 Disemba mwaka 1827 kibiriti kilivumbuliwa na John Walker mtaalamu wa madawa wa Uingereza. Hata hivyo awali, mbali na kibiriti cha Walker kuwaka kwa taabu na mashaka kilikuwa pia na hatari kwa watumiaji wake. Ni kutokana na sababu hiyo ndio maana wataalamu wengine wakafanya jitihada za kukikamilisha kibiriti hicho. Hatimaye mwaka 1855 mtaalamu mmoja wa Kiswedeni alifanikiwa kutengeneza kibiriti kama hiki kinachotumiwa leo hii baada ya kufanya majaribio na utafiti wa muda mrefu.
Siku kama ya leo miaka 195 iliyopita, alifariki dunia, Allamah Ahmad Naraqi, mtaalamu wa sheria za Kiislamu (fiqhi), hadithi na malenga mkubwa wa Iran. Alizaliwa mwaka 1185 Hijiria na akiwa kijana mdogo alisoma elimu ya dini kwa wasomi wakubwa wa mji wa Kashan, moja ya miji ya katikati mwa Iran na kufikia daraja ya ijtihadi. Aidha alisafiri mjini Najaf, Iraq kwa ajili ya kuujiendeleza kielimu. Baada ya kufariki dunia baba yake mzazi, Allamah Ahmad Naraqi alirejea mjini Kashan na kujishughulisha na kazi ya ukufunzi na malezi ya vijana wa mji huo. Moja ya athari muhimu za msomi huyo ni pamoja na kitabu cha 'Mi'rajus-S'adah' na Asraarul-Hajj'.

Siku kama ya leo miaka 841 iliyopita, alizaliwa Shihabud-Din Abdul-Rahman Dimashqi Muqaddasi, maarufu kwa jina la Abu Shamah, mmoja wa walimu wenye itibari katika vyuo vya mjini Damascus, Syria ya leo. Baada ya kuhitimu masomo yake ya msingi Shihabud-Din Abdul-Rahman Dimashqi, alielekea mjini Alexandria nchini Misri na akiwa hapo akajifunza elimu za hadithi, fiqhi na elimu nyingine za zama hizo. Baada ya hapo msomi huyo alisimamia chuo cha hadithi cha Darul-Hadith Ashrafiyyah. Kadhalika Abu Shamah aliandika vitambu mbalimbali vya historia na baadhi vikiwa vinahusiana na lugha ya Kiarabu.
