Alkhamisi, 10 Januari, 2019
Leo ni Alkhamisi tarehe 3 Jamadithani 1440 Hijria sawa na Januri 10, mwaka 2019.
Tarehe 10 Januari miaka 56 iliyopita, ilibuniwa saa ya elekroniki na wataalamu wa Uswisi, Solvil na Titus baada ya kupitisha miaka 12 ya juhudi zao, hatimaye walifanikiwa kutengeneza chombo hicho kwa kuweka vifaa kadhaa muhimu na makini. Aina hii ya saa haina mipaka kwa watoto wadogo na imetengenezwa kwa umakini mno na inafanya makosa machache sana ikilinganishwa na saa nyingine.
Siku kama ya leo miaka 99 iliyopita, inayosadifiana na 10 Januari 1920, Jumuiya ya Mataifa ilianza shughuli zake rasmi huko Geneva, Uswisi. Jumuiya hiyo, iliundwa baada ya Vita vya Kwanza vya Dunia, kwa shabaha ya kuimarisha amani na usalama duniani. Mwanzoni mwa shughuli za jumuiya hiyo, nchi za Kiafrika na Urusi hazikujiunga na jumuiya hiyo, na badala yake nchi za Uingereza na Ufaransa ndizo zilizobeba jukumu la kuzisaidia nchi hizo. Baada ya Vita vya Pili vya Dunia, mnamo mwezi Aprili 1946, uliundwa Umoja wa Mataifa, na kuchukua nafasi ya Jumuiya ya Mataifa, ingawa matatizo yaliyokuwa yakiikumba Jumuiya ya Mataifa bado yanaendelea kuukumba Umoja wa Mataifa hadi hii leo.
Siku kama ya leo miaka 103 iliyopita alifariki dunia Ayatullah Sayyid Ismail Sadr, alimu na mujtahidi wa ngazi ya juu mjini Kadhimiya, Iraq. Alisoma masomo ya awali ya dini ya Kiislamu kwa kaka yake na kisha akaelekea mjini Najaf, Iraq kwa ajili ya kujiendeleza zaidi katika uwanja huo. Akiwa mjini Najaf alijifunza elimu ya sheria za Kiislamu (fiqhi), elimu ya akhlaq na elimu nyingine tofauti za kidini. Baada ya kufariki dunia mwalimu wake mkubwa Ayatullah Mirza Shirazi, Ayatullah Sayyid Ismail Sadr alichukua jukumu la ufundishaji mjini Karbala nchini humo.
Siku kama ya leo miaka 148 iliyopita, alifariki dunia Ayatullah Mirza Abu Abdillah Sheikhul-Islami Zanjani, aalim na malenga aliyekuwa na uwezo mkubwa wa Waislamu. Alizaliwa mwaka 1224 Hijiria mjini Zanjan, moja ya miji ya Iran na akiwa kijana alielekea mjini Isfahan kwa ajili ya masomo. Akiwa mjini Isfahan alijiunga na chuo cha hauza ambacho kilikuwa moja ya vituo vyenye itibari katika elimu ya kidini wakati huo ambapo alifikia elimu ya juu na kisha kurejea nyumbani baada ya kuhitimu masomo yake. Sambamba na kujishughulisha na kazi ya ufundishaji Ayatullah Mirza Abu Abdillah Sheikhul-Islami Zanjani, aliandika vitabu vingi vikiwemo vya 'Hujjatul-Abraar' na 'Hidaayatul-Muttaqin'.
Siku kama ya leo miaka 195 iliyopita inayosadifiana na 10 Januari 1824, Joseph Aspdin mwanakemia wa Uingereza, alifanikiwa kutengeneza saruji na kwa utaratibu huo kupatikana mabadiliko makubwa katika shughuli za ujenzi. Hatua hiyo ilitambuliwa kama tukio kubwa katika shughuli za kimaendeleo na ujenzi mpya wa nyumba. Joseph Aspdin ambaye alikuwa akifanya utafiti kwa miaka kadhaa ili kutengeneza mada ambayo ingesaidia kuimarisha msingi wa nyumba, hatimaye alifanikiwa kutengeneza saruji baada ya majaribio chungu nzima.