Jumapili, Januari 13, 2019
Leo ni Jumapili tarehe sita Jamadul-Awwal 1440 Hijiria, sawa na tarehe 13 Januari 2019 Miladia.
Siku kama ya leo miaka 1026 iliyopita alifariki dunia Abu Said Muhammad Abdul-Jalil Sistani, mtaalamu wa hisabati mashuhuri wa Waislamu. Alikuwa mahiri katika uwanja wa hisabati, uhandisi na nujumu. Abu Said Sistani aliiandikia kitabu kila elimu aliyoipata, sambamba na kuwafundisha wengine. Kitabu cha 'Jamiu Shahi' kinachozungumzia masuala ya hisabati ni moja ya athari za msomi huyo katika uwanja huo. Aidha kitabu kingine ni 'Al-Madkhal' katika uwanja wa nujumu, 'Al-maani fii Ahkaamin-Nujuum' na 'Al-Dail fii Ahkaamin-Nujuum.'
Siku kama ya leo miaka 503 iliyopita alifariki dunia Zahīr ud-Dīn Babur, mfalme wa silsila ya Mongolia wa India. Zahīr Muhammad Bin Mirza Omar, aliyekuwa mmoja wa wajukuu wa Amir Timur Mongolia, alishika hatamu za madaraka ya mji wa Fergana wa Transoxiana, (Mā warāʼ an-Nahr) akiwa na umri wa miaka 11 hapo mwaka 899 Hijiria baada ya baba yake kufariki dunia. Awali na akiwa na miaka 11 alipigana vita na wafalme wa Uzbek na Tatar, na baada ya kuhisi udhaifu wao alidhibiti miji ya Kabul na Kandahar. Baada ya kuidhibiti Afghanistan aliitawala nchi hiyo kwa miaka 22. Mwaka 932 alielekea India kwa ajili ya kuidhibiti nchi hiyo na baada ya kupata ushindi akaingia New Delhi. Katika kipindi hicho Zahīr ud-Dīn Babur alipata umashuhuri wa silsila ya Mongolia wa India kutokana na kuasisi utawala wa Mongolia nchini humo. Utawala huo ulitawala India hadi mwaka 1264 Hijiria yaani kwa muda wa miaka 332. Msikiti maarufu wa Babri nchini India ni moja ya majengo ya utawala wa Zahīr ud-Dīn Babur. Aidha alitawala New Delhi hadi mwaka 937 kwa kipindi cha miaka mitano na kufariki dunia akiwa na umri wa miaka 49.
Siku kama ya leo miaka 492 iliyopita alifariki dunia Ghiyathud-Din Mansur, tatibu na mtaalamu wa hisabati wa Irani na kuzikwa mjini Shiraz. Ghiyathud-Din Mansur alisomea kwa baba yake na maulama wengine elimu za mantiki na hadithi. Kwa amri ya mtawala wa Shah Ismail Safavid, alitakiwa kukarabati kituo cha kufuatilia nyota cha Maraghe. Alibakia katika kazi hiyo hadi katika kipindi cha utawala wa Tahmasp Safavid ambapo baadaye aliachana na kazi hiyo na kusalia mjini Shiraz akijishughulisha na ufundishaji na kuandika vitabu. Miongoni mwa athari za Ghiyathud-Din Mansur ni pamoja na kitabu cha 'Hujjatul-Kalaam', 'Mashaariqu wa Mir'aat' na 'Al-Haqaaiqu.'
Siku kama ya leo miaka 569 iliyopita, alizaliwa baharia na mvumbuzi wa Kireno kwa jina la Bartholomew Diaz. Baada ya kusafiri katika Bahari ya Atlantic kuelekea kusini mwaka 1488, Diaz aligundua Rasi ya Tumaini Jema au (Cape of Good Hope) katika sehemu ya kusini zaidi ya bara la Afrika. Miaka kumi baadaye baharia mwenzake kwa jina la Vasco Da Gama naye pia alifanikiwa kugundua njia ya baharini kuelekea India kupitia eneo hilo.
Siku kama ya leo miaka 328 iliyopita alifariki dunia George Fox mrekebishaji wa Kikristo wa nchini Uingereza. Fox alizaliwa 1624 katika familia ya kidini. George Fox hakuwa akiweza kustahamili mgongano uliokuwako katika maneno na vitendo vya makasisi na wafuasi wa Ukristo na vilevile vita vya watawala wa zama hizo. Akiwa na miaka 19, Fox alikata shauri kufanya utafiti kwa ajili ya kutafuta ukweli. George Fox alikuwa akiamini kwamba, kuna ulazima wa kurejea katika mafundisho asili ya Ukristo na kujiepusha na umwagaji damu na wakati huo huo kusimama kidete kukabiliana na dhulma. Hata hivyo, Fox nae pia alitumbukia katika makosa kwenye itikadi zake. Pamoja na hayo, fikra zake zilipingana na mafundisho ya Ukristo katika zama hizo. Mara kadhaa George Fox alitiwa mbaroni na kutupwa jela na mamia ya wafuasi wake walikuwa wakiteswa gerezani. Harakati yake ya kupigania mabadiliko ya kidini iliendelea baada ya kuaga kwake dunia na harakati hiyo ingalipo.
Siku kama ya leo miaka 78 iliyopita, mkutano wa kihistoria wa nchi waitifaki za Ulaya katika Vita vya Pili vya Dunia ulifanyika mjini London, Uingereza. Mkutano huo ulifanyika kufuatia pendekezo la waziri mkuu wa wakati huo wa Uingereza Winston Churchill, lengo kuu lilikuwa kuratibu siasa za wakuu wa nchi za Ulaya katika medani za vita dhidi ya nchi mbili za Ujerumani na Italia. Vilevile nchi za Uingereza, Uholanzi, Ubelgiji, Ufaransa, Ugiriki, Norway, Luxembourg na Denmark zilishiriki katika mkutano huo.
Siku kama ya leo miaka 40 iliyopita yaani tarehe 23 Dei 1357 Hijria Shamsia, kulitokea mapigano makali baina ya askari wa utawala wa Shah na wananchi wa Iran na watu kadhaa kuuawa shahidi na kujeruhiwa wakati wa kujiri maandamano ya miji kadhaa ya Iran. Aidha katika siku hii wananchuo na wananchi wa Tehran ambao walikuwa katika mkusanyiko wao mkubwa katika Chuo Kikuu cha Tehran walitangaza upinzani wao dhidi ya utawala wa Shah na waking'ang'ania msimamo wao wa kurejea hapa nchini Imam Khomeini MA aliyekuwa uhamishoni Ufaransa.

Na siku kama ya leo miaka 38 iliyopita, shambulio la kwanza la kemikali la jeshi la utawala wa wakati huo wa Iraq chini ya uongozi wa dikteta Saddam lilitekelezwa dhidi ya Iran ikiwa ni chini ya miezi minne tu tangu Iraq ianzishe vita vya kichokozi dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Shambulio hilo lisilo la kibinadamu ambalo lilitekelezwa kilomita 50 magharibi mwa mji wa Ilam magharibi mwa Iran, lilipelekea kuuawa shahidi na kujeruhiwa raia kadhaa. Jeshi la utawala wa Baath likipata himaya na misaada ya madola ya Magharibi na Umoja wa Kisovieti lilitumia mara chungu nzima silaha zilizopigwa marafuku dhidi yya wananchi na wapiganaji wa Iran katika kipindi chote cha vita vyake vya kichokozi dhidi ya taifa hili. Takribani watu elfu kumi waliuawa shahidi na laki moja na elfu 30 kujeruhiwa kufuatia mashambuluio hayo ya silaha zilizopigwa marufuku.