Jan 14, 2019 07:24 UTC
  • Ulimwengu wa Michezo, Jan 14

Mkusanyiko wa matukio muhimu ya spoti ndani ya siku saba zilizopita, kitaifa na kimataifa....

Kombe la Asia, Iran

Timu ya taifa ya soka ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imeendelea kufanya vyema katika michuano ya Kombe la Asia inayoendelea kutifua mavumbi katika viwanja vya kandanda vya Umoja wa Falme za Kiarabu. Iran imetinga hatua ya muondoano baada ya kuisasambua Vietnam mabao 2-0 katika mchuano wa Jumamosi katika Uwanja wa Al Nahyan mjini Abu Dhabi. Strika machachari wa kikosi hicho cha Team Melli kama kinavyojulikana hapa nchini, Sardar Azmoon ndiye aliyekuwa nyota wa mechi, baada ya kuifungia timu hiyo ya Iran mabao hayo mawili katika dakika ya 38 na 70.

Wachezaji wa Iran wakishangilia goli

 

Kabla ya hapo Iran iliidhalilisha Yemen kwa kuizaba mabao 5-0 katika mchuano wake wa pili wa Kundi D. Timu hiyo ya Iran siku ya Jumatano inatazamiwa kucheza mchuano wa mwisho wa hatua ya makundi dhidi ya Iraq, katika Uwanja wa Al Maktoum mjini Dubai ili kujiweka katika mazingira mazuri ya kutinga nusu fainali. Hii ni fursa nzuri wa vijana wa mkufunzi Carlos Queiroz kulipiza kisasi cha duru iliyopita ya mashindano haya, ambapo walilazimika kuyaaga mashindano haya ya kieneo baada ya kufungwa mabao 7-6 katika upigaji penati, baada ya dakika 90 za ada na 30 za nyongeza kushuhudia majirani hawa wakitoka sare ya mabao 3-3.

Hayo ni ya kale sasa, lakini kwengineko Iraq iliichabanga Yemen mabao 3-0 katika mechi yake ya pili ya Kundi D mjini Abu Dhabi. Mabao ya Wairaqi yalifungwa na Muhammad Ali, Bashar Rasan huku Alaa Abbas akipiga msumari wa mwisho kwenye jeneza la Wayemen, kwa bao la dakika za majeruhi.

Kombe la Asia

 

Japan na Uzbekistan pia zimetinga hatua ya mtoano baada ya kushinda mechi zao. Japan iliitandika Oman bao 1 bila jibu mjini Abu Dhabi katika mchuano wa Kundi F, bao lililotiwa kimyani na Genki Haraguchi kupitia mkwaju wa penati tata.

Uzbekistan kwa upande ilipata ushindi mnono wa mabao 4-0 iliposhuka dimbani kutoana udhia na Turkmenistan, katika mchuano ulioonekana kuwa debi la jamhuri za zamani za Sovieti. Wauzbeki wanahitaji japo sare ili kujiweka pazuri watakapotoa kijasho na Wajapani siku ya Alkhamisi katika mchuano wa Kundi F. Duru ya 17 ya mashindano hayo ya kibara yanayofahamika kama AFC Asian Cup ilianza Jumamosi ya Januari 5 na inatazamiwa kufunga pazia lake Februari Mosi.

Kombe la Mapinduzi

Kwa mara nyingine tena klabu ya Azam ya Tanzania imetwaa ubingwa wa Kombe la Mapinduzi baada ya kuichabanga Simba mabao 2-1 katika mechi ya fainali iliyopigwa katika Uwanja wa Gombani kisiwani Pemba. Azam FC wameendeleza ubabe na kunyakua ubingwa wa Mapinduzi Cup, hii ikiwa ni mara ya tatu mfululizo na hivyo kuchukua kombe hilo moja kwa moja. Mchezo huo wa wikendi ulikuwa wa kusisimua licha ya Simba kuchezesha timu B.

Wachezaji na mashabiki wa Azam wakinyayua Kombe la Mapinduzi

 

Azam ndiyo walikuwa wa kwanza kucheka na nyavu, kupitia goli la kiungo Yahya Mudathir katika dakika ya 44. Hata hivyo Simba walinguruma kidogo na kufanya mambo kuwa 1-1, kupitia bao lililofungwa na Yusuf Mlipili katika dakika ya 63 ya mchezo. Hata hivyo Azam walijizoa, kujipapatua na kujikusanya tena na kulizamisha jahazi la Simba, kwa kufunga bao la pili na ushindi, lililotiwa kimyani na Obrey Chirwa dakika tisa baadaye.

Kabla ya hapo, Azam FC ilikuwa imeisasambua Yanga mabao 3-0 katika mechi ya hatua ya makundi. 

Simba yawadhalilisha Waarabu

Lakini kama wanavyosema wenye kusema, usimuone Simba kanyeshewa ukadhani ni paka. Klabu ya Simba ya Tanzania iliwashushia kichapo cha mbwa klabu ya JS Saoura ya Algeria katika mchuano wa Ligi ya Mabingwa wa Afrika uliopigwa Jumamosi katika Uwanja wa Taifa wa Dar es Salaam. Katika dakika za nyongeza kipindi cha kwanza kimalizike, mchezaji nyota wa Simba Emmanuel Okwi alifanikiwa kutumia uwezo wake wa mguu wa kushoto na kumalizia pasi ya Clyetous Chama ambaye alipiga pasi mpenyezo iliyomkuta Okwi, ambaye naye aliwaminya mabeki Waarabu na kumalizia kwa shuti kali.  Kuumia kwa John Bocco na kuingia kwa Meddie Kagere kulifanya Simba iongeze magoli mawili kunako dakika ya 52 na 67. Katika dakika ya 52 Okwi alimtengenezea pasi Meddie Kagere ambaye aliandikia Simba bao la pili.  Dakika ya 67 Kagere alimalizia pasi nyingine ya Okwi na kuandika bao la tatu kwa Simba lililowanyanyua mashabiki toka vitini katika Uwanja wa Taifa Dar es Salaam. 

Wachezaji wa Simba

 

Simba SC sasa itasafiri kwenda Congo January 19 kucheza mchezo wake wa pili dhidi ya AS Vita, siku moja baada ya al-Ahly ya Misri kutua Algeria kuvaana na JS Saouro. Katika mechi nyingine ya Ligi ya Mabingwa wa Afrika, al Ahly ya Misri iliikaribisha AS Vita ya Kongo DR katika uwanja wa Burj al Arab mjini Alexandria, ambapo mwenyeji aliibuka na ushindi wa magoli 2-0. Kwa matokeo hayo, Simba ya Tanzania inaongoza Kundi D, ikiwa na alama 3 na magoli 3, ikifuatiwa na al- Ahly yenye alama 3 na magoli 2. AS Vita ipo katika nafasi ya tatu kwa kutokuwa na alama wala goli la kufunga huku JS Soura ikivuta mkia.

Dondoo za Hapa na Pale

Shirikisho la Soka Afrika CAF lilitangaza Jumanne iliyopita kuwa Misri ndiyo itakuwa mwenyeji wa michuano ya soka ya Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon) 2019, baada ya kuipokonya Cameroon uenyeji huo. Kamati kuu ya CAF ilikutana Jumanne iliyopita katika mji mkuu wa Senegal, Dakar na kupiga kura ya kuamua ni nani kati ya Misri na Afrika Kusini itapewa uenyeji huo wa Afcon. Awali shughuli hii ilikuwa imepangwa kufanyika Jumatano. Mashindano hayo ya kibara yatakayozileta pamoja timu za taifa za mataifa 24 ya Afrika yanatazamiwa kufanyika kati ya Juni 15 na Julai 13 mwaka huu 2019. CAF iliipokonya Cameroon haki za kuandaa kindumbwendumbwe hicho kutokana na hali duni ya usalama na pia miundombinu isiyoridhisha. Cameroon ilipokonywa uenyeji huo mnamo Novemba 30 mwaka uliomalizika, wakati kamati kuu ya CAF ilipofanya kikao chake jijini Accra, Ghana.

Wakati huohuo, mshambuliaji wa timu ya taifa ya soka ya Misri na klabu ya Liverpool nchini Uingereza, Mohammed Salah, kwa mara ya pili mfululizo amepata tuzo ya mchezaji bora barani Afrika. Mo Salah mwenye umri wa miaka 26, amepata tuzo hiyo katika hafla iliyofanyika jijini Dakar nchini Senegal na kuwashinda Sadio Mane, anayecheza naye klabu moja, na pia Pierre-Emerick Aubameyang raia wa Gabon anayecheza soka katika klabu ya Arsenal. 

Na Malaysia imesema haitawaruhusu wanariadha wa utawala wa Kizayuni wa Israel kukanyaga ardhi ya nchi hiyo, ikiwa ni katika mwendelezo wa serikali ya Kuala Lumpur wa kupambana na utawala huo batili. Waziri Mkuu wa Malysia, Dakta Mahathir Mohammad amewaambia waandishi wa habari kuwa, "Serikali yangu haitatoa kibali cha kuwaruhusu wanariadha wa michezo ya walemavu wa Israel kuingia nchini hapa na iwapo watajileta, tutaihesabu hatua hiyo kama ukiukaji wa sheria." Dakta Mahathir amefafanua kuwa, Malaysia ni muungaji mkono wa Palestina na wala haina uhusiano wa kidiplomasia na utawala haramu wa Israel, na kwa msingo huo, serikali yake itakuwa inakiuka sheria iwapo itatoa viza kwa ajili ya wanamichezo hao wa Israel.

Dkt Mahathir

 

Licha ya mashinikizo kutoka kwa Kamati ya Kimataifa ya Paralimpiki na Shirikisho la Olimpiki la Israel ya kuitaka Malaysia iangalie upya uamuzi wake huo, lakini serikali ya Dakta Mahathir imeshikilia kuwa haitawaruhusu wanamichezo hao wa Kizayuni kuingia nchini humo, kushiriki mashindano ya kimataifa ya uogoleaji ya walemavu. Mashindano ya Mabingwa wa Kuogolea ya Walemavu (World Para Swimming Championships) yanatazamiwa kufanyika kati ya Julai 29 na Agosti 4 mwaka huu, katika mji Kuching, kisiwani Borneo, kusini mashariki mwa Malaysia. Huko nyuma pia Malaysia ilikataa kuziruhusu timu za tenisi na mchezo wa upigaji makasia za utawala huo wa Kizayuni kuingia katika nchi hiyo kushiriki mashindano ya kimataifa ya michezo hiyo.

…………………….TAMATI……………….

 

 

Tags