Feb 25, 2019 07:26 UTC
  • Ulimwengu wa Spoti, Feb 25

Huu ni mkusanyiko wa matukio muhimu ya michezo yaliyojiri ndani ya siku saba zilizopita, kitaifa na kimataifa...

Badminton: Binti wa Kiirani atunukiwa Uganda

Mchezaji wa mpira wa vinyoya wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ametunukiwa medali ya shaba baada ya kuibuka wa tatu katika mashindano ya dunia ya mchezo huo nchini Uganda. Samin Abed Khojaste aliibuka wa tatu baada ya kushindwa katika mchezo dhidi ya raia wa Myanmar.

Samin Abed Khojaste

 

Katika katagoria ya wachezaji wawili kila upande kwenye mashindano hayo yanayofahamika kama badminton kwa Kiingereza, binti huyo wa Kiirani akishirikiana na mwenzake wa Jordan waling'ara dhidi ya Wazambia na kutinga mpambano wa fainali. Washindi watatuzwa dola elfu 10 za US.

Soka: Zob Ahan yatoka nyuma na kuibanjua al-Gharafa ya Qatar

Klabu ya Zob Ahan ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ilitoka nyuma na kuibanjua al-Gharafa ya Qatar mabao 3-2 katika hatua ya muondoano ya michuano ya Ligi ya Klabu Bingwa Barani Asia ya AFC, mwaka huu 2019. Zob Ahan walienda mapumzikoni wakiwa wanyonge, baada ya wenyeji kucheka na nyavu zao mara mbili, kupitia magoli yaliyofungwa na Ahmed Al Aaeldin na Mehdi Taremi.

Timu ya kandanda ya Zob Ahan ya Iran

 

Hata hivyo baada ya kujizoa na kurekebisha mapungufu, klabu hiyo ya soka ya Iran iliingia uwanjani ikiwa makini zaidi katika kipindi cha pili. Kiungo Christian Osaguona alipachika wavuni bao la kwanza la Zob Ahan dakika mbili baada ya kuanza nusu ya pili ya mchezo, kabla ya Amir Arsalan Motahari kufanya mambo kuwa suluh bin suluh kwa goli alilolifunga kunako dakika ya 63. Zon Ahan ya Iran ilipata bao la ushindi katika dakika ya 79 licha ya kuchezea ugenini, kupitia mchezaji Mohammad Nejad Mehdi.

Zob Ahan ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ilitinga hatua ya muondoano katika michuano ya kusaka tiketi ya Ligi ya Klabu Bingwa Barani Asia ya AFC, mwaka huu 2019, baada ya kuichachafya klabu ya al-Kuwait bao moja bila jibu katika mchuano wa mkondo wa pili uliopigwa katika uwanja wa Foolad Shahr mjini Isfahan. Sasa klabu hiyo imejiunga na Al Wasl ya Imarati, Al Zawraa ya Iraq pamoja klabu ya Saudi Arabia ya Al Nassr katika Ligi ya Klabu Bingwa Barani Asia ya AFC, mwaka huu 2019. 

Klabu nyingine ya Iran ya Saipa ambayo ilitinga hatua ya muondoano baada ya kuipa kichapo cha mbwa klabu ya India ya Minerva Punjab, kwa kuichabanga mabao 4-0, ilizabwa mabao 3-1 iliposhuka dimbani kupepetana na klabu ya al-Rayyan ya Qatar katika mechi nyingine ya muondoano.

Michuano ya Kombe la Shirikisho

Klabu ya Gor Mahia ya Kenya iliidhulumu klabu ya Hussein Dei ya Algeria mabao 2-0 katika mechi yao ya tatu ya Kombe la Shirikisho. Katika kitimutimu hicho cha Jumapili, Kogalo wakichezea nyumbani katika Uwanja Taifa wa Kasarani jijini Nairobi walifanikiwa kuvuna ushindi huo mnono, na kujiweka katika nafasi nzuri ya kusonga mbele. Mabao ya Gor Mahia ambao pia wanafahamika kama Sirkal yalifungwa na Francis Kahata na Jacques Tuyisenge.

Mchezaji wa Gor Mahia akipambana na Muarabu wa Zamaleck

 

Kwa ushindi huo Gor Mahia imerejea kileleni mwa Kundi D ikiwa na alama 6 huku Waarabu hao wa Algeria wakidondoka hadi nafasi ya pili wakiwa na pointi 4. Hata hivyo mchezo wa Jumapili katika uwanja wa Kasarani uligubikwa na kisirani na vimbwaga vya hapa na pale, huku mchezaji wa Hussein Dei akilishwa kadi nyekundu na kuipa nakisi timu yake.

Nayo klabu ya Nkana Red Devils ya Zambia iliigaragaza Asante Kotoko ya Ghana kwa mabao 3-1 katika mchezo wa Kundi C wa Kombe la Shirikisho Afrika uliofanyika katika uwanja wa Kitwe nchini Zambia. Kipigo hicho ambacho ni cha pili kwa Kotoko kimewashusha hadi mkiani mwa msimamo wa kundi hilo ikiwa na alama tatu. Mchezo wa marudiano baina ya timu hizo mbili utapigwa Jumapili ya Machi 3 nchini Ghana.

Kwengineko, klabu ya Yanga ya Tanzania wamefanikiwa kutinga robo fainali ya michuano ya Kombe la Shirikisho la Soka la Tanzania maarufu kama Azam Sports Federation Cup (ASFC) baada ya kuifanya mambo Namungo FC katika Uwanja wa Kassim Majaliwa wilayani Ruangwa mkoani Lindi. Shujaa wa Yanga kwa mara nyingine alikuwa mshambuliaji wake, Heritier Makambo raia wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo aliyefunga bao hilo la pekee kunako dakika ya 82 kwa kichwa cha kuparaza, akimalizia krosi iliyochongwa na Deus Kaseke kutoka upande wa kulia.

Timu nyingine zilizofanikiwa kutinga robo fainali ni Singida United, African Lyon, KMC, Kagera Sugar, Lipuli FC na Alliance FC.

Dondoo za Hapa na Pale

Timu ya Kenya ya mchezo wa magongo ya wachezaji watano kila upande imetwaa ubingwa wa mashindano ya kikanda ya mchezo huo yaliyofanyika nchini humo. Timu hiyo inayofahamika kama Tausi iliilemea Uganda na kuizaba mikwaju 2-1. Waganda hata hivyo wamerejea nchini kwao na medali ya fedha kutoka Kenya walikoshiriki mashindano ya mchezo huo kwa vijana wenye umri wa chini ya miaka 19. Kocha wa timu hiyo Moses Nsereko amewapongeza wachezaji wake licha ya kupoteza katika mchezo wa fainali dhidi ya timu ya Tausi ya Kenya.

Vincenzo Montella

 

Mbali na hayo, kuna tetesi kwamba, Muitaliano Vincenzo Montella, ambaye alikuwa mkufunzi wa klabu ya AC Millan ndiye atakayerithi mikoba ya aliyekuwa kocha mkuu wa timu ya taifa ya soka ya Iran, Carlos Queiroz. Kwa mujibu wa tovuti ya habari za michezo ya Goal.com, Montella mwenye umri wa miaka 44 amepewa ofa na Shirikisho la Soka la Iran ya kuionoa Team Melli ya Iran kwa mkataba wa miaka 3 na nusu kwa kima cha Pauni milioni 1.5. Mkufunzi huyo wa Italia ambaye kwa sasa hana timu anayoinoa, alitimuliwa na Seville Aprili mwaka jana 2018, kutokana na matokeo mabaya ya klabu hiyo aliyokuwa akiifundisha soka, katika michuano ya Ligi Kuu ya Soka ya Uhispani (La Liga). Montella ambaye enzi zake uwanjani alikuwa amepewa jina la utani la Aeroplanino kutokana na kasi ya ndege aliyokuwa nayo uwanjani, amewahi kuzichezea Empoli, Roma na Fulham. Queiroz aliondoka Tehran kuelekea Lisbon, Ureno baada ya kuwanoa vijana wa Team Melli kwa muda wa miaka minane. Kocha huyo mwenye umri wa miaka 65 aliachia ngazi muda mfupi baada ya Iran kukubali kichapo kutoka Japan katika mchuano wa nusu fainali ya Kombe la Asia. 

Aliyekuwa kocha wa timu ya mpira wa miguu ya Iran, Carlos Queiroz

 

 

Na klabu ya soka ya Uingereza ya Manchester City kwa mara nyingine tena imetwaa Kombe la Carabao baada ya kuizima Chelsea kupitia mikwaju ya penati katika fainali ya Jumapili. Chelsea iliyo chini ya kocha Maurizio Sarri na Man City inayonolewa na Pep Guardiola zilishindwa kutambiana katika dakika 90 za ada na 30 za nyongeza na ndiposa zikaishia kupiga mikwaju ya penati. Chelsea licha ya kuwa imara na kudhibiti mashambulizi ya Man City lakini walijikuta wakipoteza kwa penati iliyoishia kwa mabao 4-3.

Mwaka jana pia City walitwaa Kombe la Carabao

 

Hii ndio mara ya kwanza kwa mchezo wa fainali ya EFL Cup kuchezwa dakika 120 pasipo kupatikana bingwa toka mwaka 2016, ambapo Man City iliibuka tena bingwa wa michuano hiyo.

………………TAMATI…..………..

 

 

 

 

 

Tags