Spoti, Machi 4
Hujambo mpenzi msikilizaji wa na karibu tutupie jicho baadhi ya matukio muhimu ya spoti yaliyojiri ndani ya siku saba zilizopita, kitaifa na kimataifa….
Taekwondo: Iran yatwaa Kombe la Rais
Timu ya wanaume ya taekwondo ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imetwaa Kombe la Rais katika mchezo huo kanda ya Asia mwaka huu 2019. Wanataekwondo wa Iran wameibuka kidedea katika duru ya tatu ya mashindano hayo yaliyofanyika kisiwani Kish, katika pwani ya kusini mwa nchi tangu Februari 28, baada ya kuzoa jumla ya alama 763. Wanataekwondo wa Iran ya Kiislamu wametoa kibindoni medali 5 za dhahabu, fedha 2 na shaba 1. Jordan ambayo ilikuwa na alama 279 imeibuka ya pili na kuzoa medali 2 za dhahabu na shaba 1. Korea Kusini imemaliza ya tatu katika mashindano hayo yanayofahamika kwa Kiingereza kama 3rd World Taekwondo President's Cup Asian Region, kwa kupata alama 128.
Safu ya watoto ya mashindano hayo yamefanyika Jumamosi huku mashindano hayo kwa ujumla yakifunga pazia lake Jumapili ya Machi 3. Mashindano hayo yamehudhuriwa na Rais wa Shirikisho la Taekwondo Dunia, Chungwon Choue. Aidha safu ya wanadada, Iran imeng'ara baada ya kuzoa medali 9 za dhahabu na fedha moja, huku wakizoa jumla ya alama 1169. Jordan imeibuka ya pili huku India ikifunga orodha ya tatu bora. Kadhalika katika kategoria ya vijana barubaru, vijana wa Iran wameibuka washindi baada ya kutwaa medali 9 za dhahabu na fedha 1, huku wakikusanya alama 1169. Jordan na Syria zimeibuka za pili na tatu kwa usanjari huo. Wanataekwondo 172 kutoka nchi mbalibali duniani kama vile, Azerbaijan, Marekani, Jordan, Armenia, Uzbekistan, Afghanistan, Ukraine, Iran, Pakistan, Tunisia, China, Russia, Syria, Sweden, Iraq, Oman, Kazakhstan, Korea Kusini, Georgia, Lebanon, Poland na India, wameshiriki mashindano hayo.
Mpira wa Kikapu, Iran yatinga Kombe la Dunia
Timu ya taifa ya mpira wa kikapu ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imetinga Kombe la Dunia la Basketboli baada ya kuigaragaza Australia katika kipute cha fainali cha Kundi F. Katika mchezo huo wa mwisho wa mkondo wa sita wa kufuza Kombe la Dunia la Mpira wa Kikapu mwaka huu 2019 uliopigwa mjini Melbourne, Iran iliichachafya Australia vikapu 85 kwa 74 na hivyo kujikatia tiketi ya kushiriki mashindano hayo ya dunia yatakayofanyika nchini China.
China itakuwa mwenyeji wa mashindano hayo ya dunia yanayofahamika kwa Kimombo kama Basketball World Cup 2019 yanayoandaliwa na Shirikisho la Mpira wa Kikapu Duniani FIBA, kuanzia Agosti 31 hadi Septemba 15 mwaka huu.
Kombe la Shirikisho Afrika CAF
Klabu ya Gor Mahia ya Kenya ilishuka dimbani wikendi kupepetana na mwenyeji wake wa Algeria, klabu ya Hussein Dey katika mji mkuu Algiers katika michuano ya Kombe la Shirikisho barani Afrika. Katika mechi hiyo ya Kundi D, Kogalo imekubali kuzabwa goli 1-0 na Waarabu hao wa Algeria, ingawaje ilidhaniwa kuwa wangenyolewa zaidi kwa chupa kwa kuchezea ugenini. Hussein Dey iliingia uwanjani wakifahamu fika kuwa, lazima wapate ushindi katika mchezo huo wa nyumbani, kwa kutilia maanani kuwa, tayari walikuwa wamekubali kichapo cha mabao 2-0 walipocheza na Gor Mahia katika mechi yao ya tatu ya Kombe la Shirikisho iliyopigwa katika Uwanja Taifa wa Kasarani jijini Nairobi.
Mashabiki wa Kogalo wanahisi Gor walichezewa rafu, baada ya goli la kichwa la Shafik Batambuze baada ya kupokea mpira wa kona kutoka kwa Francis Kahata kukataliwa. Kwa ushindi huo, Hussein Dey wamerejea kileleni mwa Kundi D wakiwa na alama 7, huku KOgalo wakishushwa tena hadi katika nafasi ya pili wakiwa na pointi 6. Katika michuano mingine ya Kombe la Shirikisho barbi Afrika, klabu ya Zamalek ya Misri imefanikiwa kuifunga Petro Atletico goli 1 bila jibu. huku Al Hilal Omdurman ikiisasambua Zesco United goli 3-1. Asante Kotoko ya Ghana imeizaba Nkana FC ya Zambia magoli 3-0 kwenye mechi ya Kundi C. Matokeo ya Kundi B, Etoile De Sahel imeifunga Enungu Rangers magoli 2-0, huku CS Sfaxien ikiambulia sare tasa na Salitas.
Vita dhidi ya Hijabu Michezoni nchini Ufaransa
Duka moja la nguo na vifaa vya michezo nchini Ufaransa limekusanya na kuondoa nguo za michezo za mtindo wa hijabu kwa ajili ya wanawake Waislamu baada ya kuandamwa na shutuma kali za wanasiasa na mitandao ya kijamii ya nchi hiyo. Hatua ya duka la Decathlon ya kuuza nguo hizo za michezo zijulikanalo kama "hijab de running" zinazowawezesha wanawake Waislamu kusitiri vichwa vyao wakati wanapofanya mazoezi ya viungo na ya utembeaji imeamsha moto wa hasira ndani ya Ufaransa huku wanasiasa mbalimbali wa nchi hiyo akiwemo wa chama tawala cha rais Emmanuel Macron wakidai kuwa kitendo hicho kinakiuka misingi ya Usekulari inayotawala nchini humo.
Baada ya siku kadhaa za mijadala na ukosoaji mkali katika mitandao ya kijamii, wauzaji wa nguo hizo za michezo wametoa taarifa na kutangaza kuwa wanasimamisha uuzaji wa bidhaa hiyo ndani ya Ufaransa kwa kuhofia usalama wa wafanyakazi wao, ambao wamesema wanaandamwa na matusi na vitisho katika mitandao ya kijamii. Kwa mujibu wa kampuni ya Decathlon, wamepokea zaidi ya simu na jumbe 500 za baruapepe, mbali na kauli za matusi na vitisho zinazowaandama wafanyakazi wao. Hata hivyo Waziri wa Sheria wa Ufaransa Nicole Belloubet alitangaza jana kuwa maduka ya vifaa vya michezo yako huru kuuza nguo za michezo za mtindo wa hijabu na kwamba hakuna kizuizi kisheria juu ya suala hilo.
Haya yanajiri siku chache baada ya ulimwengu wa michezo kushangilia na kupoka kwa mikono miwili habari njema kulihusu vazi hilo la staha kwa wanamasumbwi wa Kiislamu. Shirikisho la Ndondi Duniani AIBA limepasisha uamuzi wa kuwapa idhini wanamasumbwi wa kike wa dini ya Kiislamu kuvaa hijabu wakiwa katika mapambano ya kimataifa. Baada ya kufanya mkutano mjini Istanbul nchini Uturuki, Kamati Kuu ya shirikisho hilo imesema, "Wanawake sasa wataruhusiwa kuvaa hijabu iwapo watafanya hivyo kwa msingi wa mafundisho wa dini yao." Aghalabu ya mashirikisho ya michezo duniani yameruhusu vazi hilo la staha kuvaliwa uwanjani katika michezo mbalimbali kama vile taekwondo, karate, mpira wa kikapu na voliboli miongoni mwa michezo mingine.
Dondoo za Hapa na Pale
Kamati ya maadili ya Shirikisho la Soka duniani (FIFA) chini ya mwenyekiti wake, Vassilios Skouris imemfungia maisha mwamuzi wa zamani wa kimataifa na Katibu wa Chama Cha Waamuzi Tanzania (FRAT), Oden Charles Mbaga kutojihusisha na masuala ya soka ngazi ya kitaifa na kimataifa baada ya kutiwa hatiani kwa rushwa na upangaji matokeo. Afisa habari na mawasiliano wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Cliford Mario Ndimbo amesema mjini Dar es Salaam kwamba baada ya uchunguzi uliofanyika kuanzia Julai 11 mwaja jana, Mbaga amekutwa na hatia ya kuhusika kwenye upangaji wa matokeo ikiwa ni kinyume na kanuni za maadili za FIFA.
Mbali na hayo, Waziri wa Michezo nchini Kenya, Rashid Echesa amepigwa kalamu nyekundu katika mabadiliko madogo ya baraza la mawaziri yaliyofanywa na Rais Uhuru Kenyatta. Nafasi yake sasa imechukuliwa na Amina Mohammed aliyekuwa akihudumu kama Waziri wa Elimu. Mbali na kuandamwa na tuhuma za ufisadi, Echesa amekuwa akikosolewa na wadau wa michezo kwa kile wanachokitaja kuwa, ukosefu wa ushirikiano na utepetevu. Hata hivyo waziri huyo ambaye alikuja kurithi mikoba ya Hassan Wario, ambaye alitimuliwa kutokana na sakata la ufisadi katika Mashindano ya Olimpiki, ameonekana kutoguswa sana na hatua hiyo ya yeye kufutwa kazi.
Kwengineko, wanamieleka wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran wametwaa medali mbili za dhahabu na shaba moja katika mashindano ya dunia ya United World Wrestling (UWW) Dan Kolov-Nikola Petrov mjini Sofia nchini Bulgari. Hassan Yazdani na Parviz Hadi kila mmoja alijishindia medali ya dhahabu katika safu ya mieleka ya kujiachia katika mashindano hayo ya Jumapili. Katika mashindano hayo yaliyoandaliwa na Shirikisho la Mieleka Bulgaria, Yazdani pia alinyakua medali ya shaba baada ya kumlemea raia wa Russia, Igor Alekseevitch Ovsiannikov katika kitengo cha wanamieleka wenye kilo 97.
Na mchezaji tenisi nyota wa dunia, Roger Federer ameingia katika madaftari ya kumbukumbu baada ya kushinda taji lake la 100 katika mchezo huo. Katika fainali ya mashindano ya Dubai Championships, Federer alimtandika Mgiriki, Stefanos Tsitsipas seti 2 za 6-4 na 6-4 na kutwaa taji lake la 100. Federer alishinda taji lake la 99 Oktoba mwaka jana, katika mchezo wa nyumbaji mjini Basel. Mfalme huyo wa tenisi duniani ni wa pili kutwaa taji 100, akitanguliwa na Jimmy Connors ambaye ana mataji 109.
………………….TAMATI.……………