Mar 30, 2019 06:09 UTC

Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur’ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SW, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu. Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur’ani.

Hii ni darsa ya 822. Baada ya kukamilisha tarjumi na maelezo ya sura ya 37 ya Ass 'Affat, katika darsa hii tutaanza kutoa tarjumi na maelezo kwa ufupi ya Suratu S’aad. Hii ni sura ya 38 kwa mpangilio wa sura za Qur’ani tukufu na ina jumla ya aya 88. Tunaianza darsa yetu ya leo kwa aya yake ya mwanzo na ya pili ambazo zinasema:

ص ۚ وَالْقُرْآنِ ذِي الذِّكْرِ

S'ad, Naapa kwa Qur'ani yenye ukumbusho.

بَلِ الَّذِينَ كَفَرُوا فِي عِزَّةٍ وَشِقَاقٍ

Lakini walio kufuru wamo katika majivuno na upinzani

Suratu S’aad, kama zilivyo sura nyingine 28 za Qur’ani tukufu imeanza kwa herufi ya mkato. Tulipotoa maelezo ya aya ya mwanzo ya Suratul Baqarah tulieleza kwamba kwa kawaida, kila baada ya herufi hizo, huwa inazungumziwa adhama na utukufu wa Qur’ani. Kwa sababu Qur’ani tukufu imeandikwa kwa herufi hizi hizi za alfabeti za Kiarabu zinazotumiwa na watu wote; lakini pamoja na hayo ni muujiza ambao hakuna mwanadamu yeyote aliyeweza na atakayeweza kuleta mfano wake. Sura hii pia baada ya kutajwa herufi ya S’aad, inaielezea Qur’ani kwa kusema: Kitabu hiki kimejaa utajo na ukumbusho. Inapasa kueleza kwamba, mwanadamu anazijua hakika nyingi za mambo kwa fitra na maumbile ya batini aliyopewa na Allah, lakini mghafala, matamanio ya nafsi, ghariza za batini na sababu za nje humfanya mtu azisahau hakika hizo. Lakini kuisoma Qur’ani na kuzingatia muhtawa na yaliyomo kwenye aya zake, humtoa mtu kwenye mghafala na kumfanya ayakumbuke mambo hayo. Vilevile inawezekana mwanadamu akazisahau na kughafilika nazo baadhi ya hakika ambazo amezikubali kutokana na mafundisho ya dini, kama mathalani kujiri kwa Kiyama. Kwa sababu hiyo, sehemu kubwa ya aya za Qur’ani tukufu zinamkumbusha mwanadamu katika masuala na minasaba mbalimbali yale yatakayomtokezea baada ya kufa.

Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba, kuiapia Allah SW Qur’ani ni ishara ya adhama ya kitabu hicho na ukweli wa aliyekileta. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa, Qur’ani tukufu inazindua na kuamsha dhamiri ya mwanadamu na kumkumbusha anayoyajua, ambayo alikuwa ameyasahau na kughafilika nayo. Aya hizi aidha zinatuelimisha kwamba, Qur’ani imeletwa kuwakumbusha na kuwaongoza watu, lakini baadhi yao hawako tayari kuikubali haki kutokana na ghururi, kibri na inadi.

Darsa yetu hii inahitimishwa na aya ya 3 na ya 4 ambazo zinasema:

كَمْ أَهْلَكْنَا مِن قَبْلِهِم مِّن قَرْنٍ فَنَادَوا وَّلَاتَ حِينَ مَنَاصٍ

Vizazi vingapi tumeviangamiza kabla yao, na wakapiga kelele, lakini wakati wa kuokoka ulikwisha pita.

وَعَجِبُوا أَن جَاءَهُم مُّنذِرٌ مِّنْهُمْ ۖ وَقَالَ الْكَافِرُونَ هَـٰذَا سَاحِرٌ كَذَّابٌ

Na walistaajabu kuwajia mwonyaji anaye tokana na wao wenyewe, na makafiri wakasema: Huyu ni mchawi, mwongo.

Walinganiwaji wa mwanzo wa Qur’ani tukufu walikuwa ni washirikina wa Makka. Aya hizi tulizosoma zinawapa indhari watu hao kwamba, kama mtazingatia hatima ya kaumu zilizopita, mtabaini kuwa yoyote miongoni mwao, iliyokuwa imeghariki kwenye dimbwi la shirki na ukafiri, ilighadhibikiwa na kuteremshiwa adhabu na Allah na wala watu hao hawakuwa na pa kukimbilia ili kujiokoa. Kisha aya zinaendelea kueleza kuwa: Lakini wakati Mtume anapowasomea washirikina aya hizi na kuwaonya, badala ya wao kupata somo la ibra na mazingatio kutokana na hatima za kaumu zilizotangulia, wakatafakari yaliyomo kwenye aya walizosomewa na kuitambua njia ya uongofu, wanamtuhumu na kumwita mtukufu huyo mchawi na muongo. Katika vitabu vya historia imeelezwa kuwa, wakubwa wa Makureishi walimwendea Abu Talib, ami yake Bwana Mtume Muhammad SAW na kumwambia: Mwana wa nduguyo ametupotoshea vijana wetu na kuidhihaki miungu yetu. Kama anachotafuta ni umaarufu au utajiri, sisi tuko tayari kumtajirisha awe na mali zaidi kuliko Mkureishi yeyote yule, lakini kwa sharti kwamba aache anayoyasema. Wakati Abu Talib alipomfikishia Bwana Mtume SAW salamu alizopewa na washirikina, mtukufu huyo alisema: Lau kama wataliweka jua kwenye mkono wangu wa kulia, na mwezi kwenye mkono wangu wa kushoto ili niache kufikisha maneno haya, sitofanya hivyo abadani, mpaka maneno yangu haya yaenee katika jamii au niuawe katika njia hii. Abu Talib alipoona Bwana Mtume Muhammad SAW yuko thabiti na imara katika msimamo wake wa njia anayolingania, alimwambia: Endelea na ulinganiaji wako, nami sitoacha katu kukuhami na kukusaidia. Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba, ukafiri na shirki, ikiwa utatokana na inadi na ukaidi, utasababisha kuangamizwa mtu hata duniani pia. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa, hakuna hifadhi wala kimbilio lolote la kumkinga mtu na kudura na irada ya Allah SW. Toba na maghufira vina taathira kabla ya kuteremshwa adhabu ya Mwenyezi Mungu, lakini inapofikia hatua ya kuteremshwa adhabu, huwa haviwezi kuwa na faida wala taathira yoyote. Aya hizi aidha zinatuelimisha kwamba, Mitume inapasa wawe miongoni mwa wanadamu wenyewe, ili kutokana na mahitaji na hali maalumu za pamoja walizonazo wanadamu wote, waweze kuwa ruwaza na kigezo mwafaka kwa watu cha kuiga na kufuata. Vilevile aya hizi zinatutaka tuelewe kuwa, tuhuma na matusi ni miongoni mwa mbinu zilizozoeleka zaidi kutumiwa na makafiri kukabiliana na waumini. Ikiwa wao wanawatusi Mitume wa Allah kwa kuwatuhumu kuwa ni waongo na wachawi, Mitume nao wanapaswa wawe na utayari wa kukabiliana na kila aina ya tuhuma na matusi ya maadui hao wa dini ya Allah. Wapenzi wasikilizaji, darsa ya 822 ya Qur’ani imefikia tamati. Tunamwomba Allah atuonyeshe haki na atupe taufiki ya kuifuata, na atuonyeshe batili na atuwezeshe kuiepuka. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh…/