Sura ya S’aad, aya ya 5-11 (Darsa ya 823)
Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur’ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SW, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu. Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur’ani.
Hii ni darsa ya 823 na sura tunayoizungumzia hivi sasa ni ya 38 ya S’aad. Tunaianza darsa yetu kwa aya ya 5 hadi ya 7 ambazo zinasema:
أَجَعَلَ الْآلِهَةَ إِلَـٰهًا وَاحِدًا ۖ إِنَّ هَـٰذَا لَشَيْءٌ عُجَابٌ
Amewafanya miungu wote kuwa ni Mungu Mmoja tu? Hakika hili ni jambo la ajabu.
وَانطَلَقَ الْمَلَأُ مِنْهُمْ أَنِ امْشُوا وَاصْبِرُوا عَلَىٰ آلِهَتِكُمْ ۖ إِنَّ هَـٰذَا لَشَيْءٌ يُرَادُ
Na wakaondoka wakubwa wao wakiwaambia: Nendeni zenu na dumuni na miungu yenu, kwani hili ni jambo lililo pangwa.
مَا سَمِعْنَا بِهَـٰذَا فِي الْمِلَّةِ الْآخِرَةِ إِنْ هَـٰذَا إِلَّا اخْتِلَاقٌ
Sisi hatukusikia haya katika mila hii ya mwisho. Haya si chochote ila ni uzushi tu.
Katika darsa iliyopita tulisema kuwa wakubwa wa washirikina wa Kikureishi hawakuwa tayari kuyasikiliza na kuyakubali maneno ya Bwana Mtume Muhammad SAW; na ili kuwafanya watu wengine pia wasivutiwe na maneno ya mtukufu huyo, wakawa wanamtangaza Nabii huyo wa rehma kuwa eti ni mchawi na muongo. Aya hizi tulizosoma zinasema: Wao walikuwa wakiwaambia pia watu kwamba: Nyinyi mna miungu yote hii, na kila mmoja mnamuomba kwa kila haja maalumu mliyonayo. Lakini huyu Mtume, anataka kukuondoleeni miungu yenu hii yote na badala yake muwe na Mungu mmoja tu ambaye haonekani, wala nyinyi hamwezi kumwona na kumgusa. Kama nyinyi mnataka mupate muyatakayo, ishikeni barabara dini yenu hii ya kuabudu masanamu, msiyaache masanamu yenu na wala msisikilize maneno ya ajabu anayosema mtu huyu (Mtume). Sababu ni kuwa, anayoyasema yeye hayakuwapo kabla huko tutokako. Haya ndiyo tuliyofunzwa sisi na wazee wetu waliotutangulia kuhusu namna ya kuabudu; na wala hatuoni dini na mafunzo kama haya anayosema yeye, katika utaratibu wao wa kufanya ibada. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba, jukumu muhimu zaidi la Mitume lilikuwa ni kudhihirisha ubatili wa miungu bandia na ya uongo na kuthibitisha ukweli wa Mungu mmoja pekee wa haki; jambo ambalo linaonekana kitu kigeni na cha ajabu kwa washirikina na wakanushaji haki. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa, akthari ya watu hupenda waishi kwa kufuata utaratibu waliourithi kutoka kwa wazee wao. Kwao wao ni jambo gumu na lisiloweza kufikirika, kuachana na itikadi za zamani na kukubali kufuata njia na mfumo mpya wa maisha. Aya hizi aidha zinatuelimisha kwamba, vinara wa ukafiri huzusha shubha na utata na kueneza fitna juu ya ukweli wa haki. Hutumia propaganda hasi na za upotoshaji ili kuwakanya na kuwataka watu wajiweke mbali na mijumuiko inayolinganiwa ndani yake maneno ya haki. Hueneza mambo na kuhamasisha watu wadumu kwenye dhalala na upotofu.
Tunaiendeleza darsa yetu kwa aya ya 8 ambayo inasema:
أَأُنزِلَ عَلَيْهِ الذِّكْرُ مِن بَيْنِنَا ۚ بَلْ هُمْ فِي شَكٍّ مِّن ذِكْرِي ۖ بَل لَّمَّا يَذُوقُوا عَذَابِ
Ati yeye tu ndiye aliye teremshiwa mawaidha peke yake katika sisi? Lakini hao wana shaka na mawaidha yangu, bali hawajaionja adhabu yangu.
Moja ya visingizio vilivyokuwa vikitumiwa na washirikina wa Makka kueneza shaka kuhusu ukweli wa wito wa Bwana Mtume Muhammad SAW ilikuwa ni kuwaambia watu: Kwa kuwepo mabwana wote hawa wa Kikureishi, iweje mtu yatima, asiye na utajiri, wala cheo na hadhi awe ndiye wa kuteremshiwa wahyi! Kama Mwenyezi Mungu ilikuwa ateremshe malaika wake na kuwatuma kwa mtu, ingepasa amchague mtu huyo miongoni mwa mabwana wa Kikureishi, aliye maarufu na mwenye sauti, mali na utajiri mkubwa. Ni wazi kwamba maneno hayo yanatokana na mantiki ya wapenda jaha na dunia, ambao hukipima kila kitu kwa kutumia kipimo na mizani ya umaada na kudhani kwamba, kila mwenye mali na mamlaka makubwa zaidi ndiye anayestahiki kutawala na kuongoza jamii. Ilhali ni jambo lisilo na shaka kuwa uongofu wa Allah ni suala la umaanawi, na sharti la ustahiki wa ufikishaji wito wa uongofu ni mtu kuwa na roho safi na fitra iliyotakasika. Na yeye Allah SW ni mjuzi zaidi wa mja aliyepambika kwa sifa hizo na mwenye uwezo wa kubeba na kutekeleza jukumu la kufikisha ujumbe wake. Kisha aya zinamalizia kwa kusema: Wale ambao hawako tayari kuikubali haki kutokana na inadi, ukaidi na husuda wataionja adhabu ya Mwenyezi Mungu na kuona matokeo ya kukanusha kwao haki. Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba, husuda na mtu kujiona bora ni chanzo mojawapo cha kuikadhibisha haki na kutokuwa tayari kuifuata. Wakati mwengine kujiona bora, humfanya mtu ahisi walivyo navyo wenzake ni haki yake yeye; na yeye ni mstahiki zaidi wa kuvipata hivyo kuliko watu wengine. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa, ni jambo la kimaumbile mtu kuwa na shaka na hatihati juu ya jambo. Lakini anachopaswa kufanya pale anapokuwa na hali hiyo ni kufanya utafiti na uhakiki, mpaka shaka imuondoke na ukweli umbainikie. Haiwezekani kulipinga na kulikanusha jambo kwa sababu tu ya kuwa na shaka nalo.
Darsa yetu ya leo inahitimishwa na aya ya 9 hadi 11 ambazo zinasema:
أَمْ عِندَهُمْ خَزَائِنُ رَحْمَةِ رَبِّكَ الْعَزِيزِ الْوَهَّابِ
Au wanazo wao khazina za rehema za Mola wako Mlezi, Mwenye nguvu, Mpaji?
أَمْ لَهُم مُّلْكُ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ وَمَا بَيْنَهُمَا ۖ فَلْيَرْتَقُوا فِي الْأَسْبَابِ
Au wao wana ufalme wa mbingu na ardhi na vilivyomo kati yao? Basi na wazipande njia za kwendea huko!
جُندٌ مَّا هُنَالِكَ مَهْزُومٌ مِّنَ الْأَحْزَابِ
Ni jeshi litakaloshindwa miongoni mwa makundi yatayo shindwa.
Aya hizi zinaendeleza maudhui iliyozungumziwa katika aya zilizotangulia kwa kuwahutubu wanaokanusha kuteremshiwa wahyi Bwana Mtume Muhammad SAW ya kwamba: Kwani Mwenyezi Mungu amewapa wao kazi ya kuainisha Mitume, hata iwe yule wanayempenda wao ndiye amteue na kumpa jukumu la Utume, na yeyote wasiyemtaka wao asistahiki kupewa jukumu hilo? Kwa nini baadhi ya watu ni wabinafsi na wenye kujiona bora, mpaka wanajiwa na dhana ya kuhisi wanajua kila kitu na wana uwezo wa kutambua kila jambo, na kufikia hadi ya kumpangia na kumuainishia hata Mwenyezi Mungu la kufanya na kujipa haki hata ya kutoa maoni kuhusiana na hukumu na maamrisho ya Mola, kwamba yepi ni sahihi na yepi si sahihi! Sehemu inayofuatia ya aya tulizosoma inamhutubu Bwana Mtume SAW na Waislamu ya kwamba: Maneno yasiyo na maana ya washirikina yasikuvunjeni nguvu wala kukufanyeni muwe dhaifu, kwa sababu wao ni kundi dogo tu kulinganisha na makundi na matapo mbalimbali yaliyosimama kuipinga haki, lakini yote hayo hayakuweza kuizima nuru ya wito wa haki uliolinganiwa na Mitume. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba, kuongozwa watu kufuata uongofu na Mitume ni dhihirisho la rehma kubwa za Allah SW. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa, mfumo wa upangaji hukumu na sharia kwa ajili ya wanadamu uko kwenye mamlaka ya Allah SW peke yake, ambaye ndiye Muumba wa mfumo wote wa ulimwengu na mwendeshaji wa masuala yote ya ulimwengu huo. Vilevile aya hizi zinatuelimisha kwamba, mirengo na makundi yanayosimama kuipinga haki, mwishowe yatashindwa na kuangamia, hata kama kidhahiri yanaonekana kuwa na nguvu na uwezo mkubwa. Wapenzi wasikilizaji, darsa ya 823 ya Qur'ani imefikia tamati. Tunamwomba Allah aupe nusra Uislamu na Waislamu na ushindi dhidi ya maadui wa dini hiyo ya haki. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh…/