Sura ya S’aad, aya ya 12-19 (Darsa ya 824)
Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur’ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SW, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu.
Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur’ani. Hii ni darsa ya 824 na sura tunayoizungumzia hivi sasa ni ya 38 ya S’aad. Tunaianza darsa yetu kwa aya ya 12 hadi ya 14 ambazo zinasema:
كَذَّبَتْ قَبْلَهُمْ قَوْمُ نُوحٍ وَعَادٌ وَفِرْعَوْنُ ذُو الْأَوْتَادِ
Walikadhibisha kabla yao kaumu ya Nuhu, na kina A’adi na Firauni mwenye vigingi.
وَثَمُودُ وَقَوْمُ لُوطٍ وَأَصْحَابُ الْأَيْكَةِ ۚ أُولَـٰئِكَ الْأَحْزَابُ
Na Thamud na kaumu ya L’uti na watu wa Machakani. Hayo ndiyo makundi.
إِن كُلٌّ إِلَّا كَذَّبَ الرُّسُلَ فَحَقَّ عِقَابِ
Hao wote waliwakadhibisha Mitume; basi wakastahili adhabu yangu.
Katika darsa iliyopita tulieleza kwamba, wakubwa wa Makureishi wa Makka hawakuwa tayari kuukubali wahyi alioteremshiwa Bwana Mtume Muhammad SAW kwa hoja kwamba, wao ndio wastahiki na wanaofaa zaidi kwa jambo hilo kuliko Bwana Mtume. Aya tulizosoma zinamhutubu mtukufu huyo kwamba: Hawa si watu wa mwanzo kusimama kuipingia haki, bali Mitume wote waliotangulia kabla yako, nao pia walikabiliwa na upinzani wa aina hiyo, kwa sababu matajiri na wenye madaraka katika kaumu zao walikuwa wakijiona wao ndio wanaostahiki kuteremshiwa wahyi. Kwa hivyo hawakuwa tayari kuikubali haki kwa sababu wahyi huo wameteremshiwa watu ambao, kama walivyo watu wengine wote wa kawaida, hawana mali na utajiri, wala nguvu za mamlaka na madaraka. Lakini wao wanasahau kwamba wale wanaokutana na Mitume wa Mwenyezi Mungu, wakayasikia maneno yao na wakathibitikiwa na ukweli wa ujumbe wao kisha wakaamua kutoikubali haki kwa sababu ya inadi na ukaidi au ubinafsi na uhasidi, Mwenyezi Mungu anawaadhibu papa hapa duniani. Ni kama ilivyogharikishwa kaumu ya Nabii Nuh au walivyoangamizwa kwa upepo mkali watu wa kaumu ya Nabii Hud. Firauni na watu wake pia walighariki kwenye mawimbi makali ya maji ya Mto Nile. Baadhi ya kaumu nyingine pia zilifikwa na hatima zinazofanana na hizo. Kaumu ya Thamud ilimkadhibisha Nabii Saleh, kaumu ya Lut iliyakumbatia maasi, ufuska na vitendo vichafu na kaumu ya Shuaib, ambayo watu wake walikuwa wakiishi kwenye maeneo yenye hali ya hewa mwanana iliyojaa miti na mimea nayo pia iliyakaidi mawaidha na maonyo ya Mtume wao huyo. Lakini mwishowe, kaumu zote hizo zilishukiwa na adhabu ya Allah na kuangamizwa. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba, kuisoma historia ya kaumu zilizopita na hatima zilizowafika, ni jambo linalokubaliwa na kupewa umuhimu na Qur’ani tukufu ili watu wapate ibra na ukumbusho. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa, wanadamu wote, iwe ni watawala na majabari wenye nguvu kama Firauni, au watu wanyonge na wa kawaida, hawana uwezo wa kukabiliana na adhabu ya Mwenyezi Mungu. Wa aidha aya hizi zinatuelimisha kwamba, kuifanyia haki inadi na uadui hakuna mwisho mwengine ghairi ya udhalili na maangamizi.
Tunaiendeleza darsa yetu kwa aya ya 15 na 16 ambazo zinasema:
وَمَا يَنظُرُ هَـٰؤُلَاءِ إِلَّا صَيْحَةً وَاحِدَةً مَّا لَهَا مِن فَوَاقٍ
Na wala hawa hawangojei ila ukelele mmoja tu usio na muda.
وَقَالُوا رَبَّنَا عَجِّل لَّنَا قِطَّنَا قَبْلَ يَوْمِ الْحِسَابِ
Na wao husema: Mola wetu Mlezi! Tuletee upesi sehemu yetu ya adhabu kabla ya Siku ya Hisabu.
Aya hizi zinaendeleza yale yaliyozungumziwa katika aya zilizopita kwa kusema: Jinsi washirikina na makafiri wanavyoikaidi na kuipa mgongo haki, utadhani wanachongojea hivi sasa ni ukelele mkali wa mbinguni ambao utawashukia ghafla na kuwaangamiza. Kwa sababu, wao wanajua hatima iliyozipata kaumu zilizopita, lakini pamoja na hayo hawaachi ukaidi na uadui wao wa kuipinga haki. Wanavyomfanyia Bwana Mtume Muhammad SAW, ni sawa na namna makafiri wa zama zilizopita walivyokuwa wakiwafanyia Mitume wao; basi na wangojee kufikwa na adhabu kama iliyowapata wao. Adhabu ambayo, itakapokuja, haitatoa fursa ya kurejea na itaangamiza kila kitu. Kisha aya zinaendelea kueleza kwamba: Washirikina wanakadhibisha kuteremshwa adhabu hapa duniani na kusimamishwa mahakama ya uadilifu ya Allah Siku ya Kiyama; kwa hivyo wanasema kwa kejeli na stihzai: Mwambie huyo Mungu wako aiharakishe adhabu yetu kabla ya hiyo siku ya malipo. Kwa nini tukae tusubiri mpaka tufe kisha tufufuke ndipo tuadhibiwe!?; sisi tunataka tuadhibiwe kwa amali zetu papa hapa duniani. Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba, mtu ambaye anaijua hatima na mwisho wa waliotangulia, kisha akasimama kumpinga Mwenyezi Mungu na Mtume wake, ni kama anangoja kushukiwa na adhabu na ameshaamua kuyaendea maangamizi kwa miguu yake mwenyewe. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa, ghururi na ukaidi huwafanya makafiri na wakadhibishaji wazikejeli na kuzifanyia stihzai imani za waumini; na badala ya kutumia hoja na mantiki wanawafanyia dhihaka na shere waumini hao. Vile vile aya hizi zinatuelimisha kwamba, kutubia kunakubaliwa kabla ya kuteremshwa adhabu, lakini wakati adhabu inapokuja, hakuna toba tena itakayopokelewa.
Tunaihitimisha darsa yetu ya leo kwa aya ya 17 hadi 19 ambazo zinasema:
اصْبِرْ عَلَىٰ مَا يَقُولُونَ وَاذْكُرْ عَبْدَنَا دَاوُودَ ذَا الْأَيْدِ ۖ إِنَّهُ أَوَّابٌ
Subiri kwa hayo wayasemayo, na umkumbuke mja wetu Daudi, mwenye nguvu. Hakika yeye alikuwa mwingi wa kutubia.
إِنَّا سَخَّرْنَا الْجِبَالَ مَعَهُ يُسَبِّحْنَ بِالْعَشِيِّ وَالْإِشْرَاقِ
Hakika tuliidhalilisha milima pamoja naye ikisabihi asubuhi na jioni pamoja naye.
وَالطَّيْرَ مَحْشُورَةً ۖ كُلٌّ لَّهُ أَوَّابٌ
Na pia ndege waliokusanywa makundi kwa makundi; wote walikuwa wanyenyekevu kwake.
Baada ya aya zilizotangulia, ambazo zimeashiria lugha chafu na ya kejeli ya wapinzani wa haki, aya hizi zinasema: Hata Nabii Daud, ambaye alikuwa na utawala wenye adhama na mamlaka makubwa hakusalimika na maneno ya kejeli na ufidhuli ya watu wake. Kwa kuanzia aya zinasema: Ewe Mtume! na enyi waumini! Kuweni na subira na vumilieni kejeli na stihzai mnazofanyiwa; na jueni kwamba hatimaye nyinyi ndio mtakaoshinda. Jengine ni kwamba Nabii Daud (as) alikuwa daima akifanya munajat na kumwomba Mola. Na kwa irada ya Allah, akawa na mamlaka na utawala mkubwa, mpaka Mwenyezi Mungu akamtiishia na kumdhalilishia milima isiyo na roho na ndege wapaao angani, ambapo wakati alipokuwa anamsabihi Mola wake, viwili hivyo, navyo pia vikawa vinashirikiana naye kufanya hivyo. Kwa mujibu wa aya za Qur’ani, viumbe vyote ulimwenguni vimo kwenye hali ya kumsabihi Allah SW; tab’an sisi wanadamu hatuna uwezo wa kukufahamu kusabihi huko. Kutokana na aya za sura hii inabainika kwamba, wakati Nabii Daud alipokuwa anamsabihi Mwenyezi Mungu, viumbe wengine pia walikuwa wakiungana naye katika kufanya hivyo, naye Mtume huyo wa Allah akafahamu namna wao pia wanavyomsabihi Mola. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba, kejeli na propaganda za maadui dhidi ya haki na watetezi wake ni nyingi na kali, na zinadumu na kuendelea. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa, haifai waumini kuyumba na kudhoofishwa na stihzai na maneno ya kifidhuli ya maadui. Wanatakiwa wawe na subira na uvumilivu wa kuzikabili kejeli na maneno yao ya jeuri na ufidhuli, na kuwa thabiti na imara katika kushikamana na itikadi na misingi ya dini yao. Vile vile aya hizi zinatuelimisha kwamba, madaraka ya utawala ni kitu hatari na chenye kuitia wasiwasi nafsi, isipokuwa kama mtu atakuwa daima anajielekeza kwa Mola na kutubia, kunyenyekea na kujitambua kuwa yeye ni mja wa Allah. Wa aidha aya hizi zinatufunza kuwa, hata kama makafiri watafanya inadi na ukaidi na kukataa kumnyenyekea Allah, lakini wajue kwamba viumbe wote ulimwenguni wakiwemo wanyama na vitu visivyo na roho, vimo kwenye hali ya kumsabihi Mwenyezi Mungu Mtukufu. Na pia aya hizi zinatutaka tujue kwamba, kama mwanadamu atakuwa mja halisi wa Allah, harakati za ulimwengu wa maumbile zitakwenda sambamba na harakati zake. Wapenzi wasikilizaji, darsa ya 824 ya Qur’ani imefikia tamati. Tunamwomba Allah atujaalie kuwa waja wake wa kweli, ambao daima humfikiri na kumkumbuka Yeye nyoyoni mwao, na kumsabihi na kumdhukuru kwa ndimi zao. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh…/