Mar 30, 2019 07:07 UTC

Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur’ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SW, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu.

Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur’ani. Hii ni darsa ya 827 na sura tunayoizungumzia hivi sasa ni ya 38 ya S’aad. Tunaianza darsa yetu kwa aya ya 29 ambayo inasema:

كِتَابٌ أَنزَلْنَاهُ إِلَيْكَ مُبَارَكٌ لِّيَدَّبَّرُوا آيَاتِهِ وَلِيَتَذَكَّرَ أُولُو الْأَلْبَابِ

Hiki ni Kitabu, tumekuteremshia wewe, kimebarikiwa, ili wazizingatie Aya zake, na wawaidhike wenye akili.

Katika darsa iliyopita tulisema, mfumo wa uumbaji na vilevile mfumo wa utoaji hukumu za adhabu na thawabu imewekwa kwa msingi wa haki na uadilifu. Kwa sababu hiyo, Mwenyezi Mungu hawatazami kwa jicho moja na kwa hali sawa wema na wabaya. Baada ya maelezo hayo, aya tuliyosoma inaendeleza maudhui hiyo kwa kusema: Qur'ani ni kitabu kilichoteremshwa kwa madhumuni ya kubainisha lengo la uumbaji na kwa ajili ya kujengeka, kupevuka na kutukuka wanadamu wote. Tab'an wanadamu hao ni wale wanaozitafakari aya za kitabu hicho, na wakatumia akili na fikra ili kuzifahamu, mpaka wakaweza kudiriki kwa undani utukufu wa maamrisho ya Allah ambayo ni ya hekima tupu na kuweza kuifikia njia ya saada na fanaka. Na sababu ni kuwa, watu walioghafilika na Allah na wakajisahau nafsi zao, huwa ni viumbe wafu japokuwa kidhahiri wako hai, na viwiliwili vyao vinakua na kunawiri. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba, lengo la kuteremshwa Qur'ani ni kuzingatia na kuzitafakari aya na ishara hizo za Mwenyezi Mungu, japokuwa kuzisoma aya za Kitabu hicho, nako pia kunamletea mtu baraka katika maisha yake. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa, kinyume na wanaodhani kwamba wahyi hauafikiani na akili na hekima, ukweli ni kwamba wahyi wa Allah unaafikiana na akili na hekima; na ndani ya Qur'ani halipatikani jambo lolote linalopingana na kukinzana na akili. Kwa hakika wahyi umeteremshwa ili akili za wanadamu ziweze kupevuka na kutukuka; na si kuidumaza na kuipiga vita akili. Aya hii aidha inatuelimisha kwamba, watu wenye hekima na wenye kuzitafakari aya za Qur'ani, huweza kubaini hukumu za kitabu hicho na siri zilizomo ndani yake.

Darsa yetu ya leo inahitimishwa na aya ya 30 hadi 33 ambazo zinasema:

وَوَهَبْنَا لِدَاوُودَ سُلَيْمَانَ ۚ نِعْمَ الْعَبْدُ ۖ إِنَّهُ أَوَّابٌ

Na Daudi tukamtunukia Suleiman. Mbora wa waja. Kwa hakika alikuwa mwingi wa kutubia.

إِذْ عُرِضَ عَلَيْهِ بِالْعَشِيِّ الصَّافِنَاتُ الْجِيَادُ

Alipopelekewa jioni farasi wasimamao kidete, wepesi wakimbiapo;

فَقَالَ إِنِّي أَحْبَبْتُ حُبَّ الْخَيْرِ عَن ذِكْرِ رَبِّي حَتَّىٰ تَوَارَتْ بِالْحِجَابِ

Basi akasema: Navipenda vitu vizuri kwa kumkumbuka Mola wangu Mlezi. Kisha wakafichikana nyuma ya boma.

رُدُّوهَا عَلَيَّ ۖ فَطَفِقَ مَسْحًا بِالسُّوقِ وَالْأَعْنَاقِ

Nirudishieni! Akaanza kuwapapasa miguu na shingo.

Aya hizi kwanza zinatoa habari za mwana aitwaye Suleiman aliyetunukiwa Nabii Daud (as). Mwana ambaye, kama alivyokuwa Nabii Daud mwenyewe, alikuwa mja mwema wa Mwenyezi Mungu, ambaye daima alikuwa akimrejea na kumuelekea Mola wake. Kisha aya zinaashiria adhama ya mamlaka na utawala wa Nabii Suleiman na ukaguaji wa jeshi lake lenye farasi hodari na wepesi wanaokwenda mbio kwa kasi na kueleza kwamba: Wakati gwaride la askari wapanda farasi hao lilipokuwa likipita mbele ya Nabii Suleiman, badala ya mtukufu huyo kuingiwa na ghururi na kiburi na kujihisi ana nguvu na mamlaka makubwa, alikuwa akiwaambia watu wake wa karibu waliomzunguka: Mimi ninawapenda farasi hawa kwa ajili ya Mwenyezi Mungu, ili wawe sababu ya kupatikana amani katika jamii na pia silaha ya kupigania jihadi na maadui. Nabii Suleiman alishughulika kuangalia harakati za farasi hao mpaka walipotoweka kwenye upeo wa uoni wa macho yake. Kisha akaamuru farasi hao warejeshwe tena. Mara hii akatoka yeye mwenyewe kwenda kuwalaki wale farasi, akawapapasa na kuwapuna kichwani na mgongoni, mambo ambayo kwa kawaida wenye farasi huwa wanawafanyia farasi wao baada ya kushuka, ambayo ni namna fulani ya kumuenzi farasi na kuonyesha mapenzi kwake. Lakini, tuseme pia kwamba, kwa masikitiko, kutokana na kutegemea baadhi ya kauli ambazo si sahihi, aya hizi zimefasiriwa kwa namna nyingine, ambapo kuhusiana na kadhia hii, Nabii Suleiman (as) amenasibishiwa mambo yasio laiki wala yasiyostahiki. Kwa mfano katika baadhi ya marejeo imeelezwa kwamba: Suleiman (as) alikuwa ametekwa na kuzama kwenye mawazo ya kuwaangalia farasi mpaka jua likazama akakosa kusali Sala ya Alasiri. Hapo ikabidi amwombe Mwenyezi Mungu alirudishe jua ili awahi kusali Sala yale. Inawezekanaje kukubali kitu kama hicho, kwamba kuangalia gwaride la askari na farasi kumshughulishe na kumsahaulisha kusali Nabii Suleiman mpaka lifike jua kuzama? Ni wazi kwamba, kauli kama hizi si sahihi, na jambo kama hilo haliwezi kufanywa hata na mtu wa kawaida seuze mja mwema na mteule kama Nabii Suleiman (as); Mtume ambaye katika aya hizi hizi tulizosoma, Allah SW amemtaja kwa uwazi kabisa kuwa ni mja mwema;  na akamsifu na kumwelezea kuwa ni mkithirishaji mno wa toba. Kauli hizo haziendani kabisa na muhtawa na yaliyomo ndani ya aya zenyewe. Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba, daraja ya juu kabisa ya mwanadamu ni kudhihirisha uja wake halisi kwa Allah na kumrejea na kumuelekea Yeye Mola. Na ndiyo maana Qur’ani imekuwa ikilitumia mara kwa mara neno “abd” kwa maana ya mja katika kuwazungumzia Mitume wa Allah. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa, kuwapa umuhimu maalumu walinzi wa usalama ni moja ya majukumu ya watawala katika jamii. Kwa hivyo ni jambo zuri kufanya shughuli kama za magwaride na ukaguaji wa vikosi na zana za kijeshi. Kwa sababu viongozi wa jamii inapasa wawe na taarifa na uelewa kuhusu kiwango na ubora wa vikosi vya ulinzi na wapiganaji pamoja na zana zao na kuonyesha nguvu na uwezo wao mbele ya maadui. Vile vile aya hizi zinatuelimisha kwamba, ikiwa madaraka na hatamu za utawala zitakuwa mikononi mwa waja wema, safi na wateule wa Allah havitatumika kufanyia uchokozi na uvamizi wala kutaka kuwakoloni na kuwatawala wengine. Kwa sababu waja hao huwa wanayatumia madaraka katika njia ya Allah tu na kwa ajili yake Yeye Mola. Wapenzi wasikilizaji, darsa ya 827 ya Qur’ani imefikia tamati. Tunamwomba Allah ayajaalie mataifa na jamii za Waislamu ziongozwe na watu wema, waadilifu na wenye kutawala kwa lengo la kupata radhi zake Yeye Mola. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh…/