Apr 01, 2019 02:50 UTC
  • Jumatatu, Aprili 1, 2019

Leo ni Jumatatu tarehe 25 Rajab 1440 Hijria sawa na tarehe Mosi Aprili 2019 Milaadia.

Siku kama ya leo miaka 1257 iliyopita, Imam Musa Kadhim (as) mmoja wa wajukuu watoharifu wa Mtume Mtukufu (saw) aliuawa shahidi. Imam Kadhim (as) alizaliwa mwaka 128 Hijiria huko katika eneo la Ab'waa lililoko baina ya miji mitakatifu ya Madina na Makka. Mtukufu huyo kwa miaka 20 alipata malezi na elimu muhimu kutoka kwa baba yake ambaye ni Imam Jaafar as-Swadiq (as). Baada ya kuuawa baba yake huyo, Imam Kadhim (as) alipata fursa ya kuuongoza umma wa Kiislamu kwa muda wa miaka 35, ambapo alipata mateso na mashaka mengi katika njia hiyo. Katika zama zake ambazo zilisadifiana na ustawi mkubwa wa utamaduni na elimu ya Kiislamu pamoja na kuimarishwa uhusiano na mataifa ya kigeni, Imam alifanya juhudi kubwa za kueneza mafunzo ya Kiislamu katika mataifa hayo kupitia wanafunzi wake. Mbali na hayo, Imam pia aliendesha mapambano makali dhidi ya watawala dhalimu wa Bani Abbas. Hatimaye Haroun ar-Rashid kutoka ukoo wa Bani Abbas aliyehofia sana kuporomoka kwa utawala wake, alimfunga jela Imam Kadhim (as). Licha ya kufungwa jela lakini Imam (as) hakusimamisha shughuli zake za kuhubiri dini na kupambana na madhalimu bali alifundisha na kuwaelimisha watu waliokuwa pembeni yake hali halisi ya mambo iliyotawala katika zama hizo. Hatimaye Haroun ar-Rashid alifanya njama ya kumuua Imam kwa kumpa sumu. Huku tukitoa mkono wa pole kwa Waislamu wote duniani kwa mnasaba huu mchungu wa kuuawa shahidi Imam Kadhim (as), tunakunukulieni hapa moja ya semi zake zenye mafunzo na busara kubwa. Imam anasema: 'Njia bora zaidi ya kumkurubia Mwenyezi Mungu baada ya kumjua ni kusimamisha swala, kuwatendea wema wazazi wawili na kuachana na husuda na majivuno.'

Miaka 441 iliyopita katika siku kama hii ya leo, alizaliwa nchini Uingereza William Harvey, tabibu na msomi wa elimu ya tiba. Harvey alianza kufundisha katika chuo kikuu baada ya kuhitimu mafunzo ya tiba na baadaye akaendelea kufanya utafiti katika uga huo. Mwaka 1616 tabibu Harvey aligundua namna damu inavyozunguka mwilini na kuandika makala kuhusu utafiti huo. William Harvey alifariki dunia mwaka 1657.

William Harvey

Siku kama ya leo miaka 204  iliyopita alizaliwa Otto Von Bismarck mmoja kati ya shakhsia waliokuwa na nguvu na ushawishi mkubwa katika karne ya 19 barani Ulaya na Kansela wa Ujerumani aliyepewa lakabu ya 'Kansela Madhubuti'. Alisoma sheria katika Chuo Kikuu cha Gottingen na baada ya hapo kuhudumu kama mwanadiplomasia wa Ujerumani huko New York na Paris hadi mwaka 1862 alipoteuliwa kuwa Waziri Mkuu na Wairi wa Mambo ya Nje. Alishiriki katika vita kadhaa na mwaka. Mfalme Kaiser Wilhelm II aliyekuwa mfalme wa wakati huo wa Ujerumani mwaka 1871 alimteua Bismmarck kuwa kansela wa nchi hiyo na alibakia katika nafasi hiyo kwa muda wa miaka 20. Lakini baada ya kushadidi hitilafu kati yake na Mfalme Wilhelm II, Bismarck alilazimika kujiuzulu. Bismarck alifariki dunia Agosti 24 mwaka 1898.

Otto Von Bismarck

Miaka 74 iliyopita muwafaka na leo, vikosi vya jeshi la Marekani vilianza mashambulizi makubwa katika kisiwa cha Okinawa huko Japan. Mashambulizi hayo yaliyofanywa na wanajeshi wa Marekani mwishoni mwa vita vya Pili vya Dunia yanahesabiwa kuwa vita vikubwa zaidi vya baharini na nchi kavu kuwahi kushuhudiwa kati ya Marekani na Japan. Meli 1300 na karibu ndege za kivita za Marekani elfu 10 zilishiriki kwenye vita hivyo vilivyodumu kwa muda wa siku 83.

Kisiwa cha Okinawa

Siku kama ya leo miaka 40 iliyopita, sawa na tarehe 12 Farvardin mwaka 1358 Hijiria Shamsia, baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu, wananchi Waislamu wa Iran walishiriki katika kura muhimu ya kihistoria ya maoni ya kuamua mfumo uliotakiwa kutawala hapa nchini. Kura hiyo ya maoni ilifanyika kwa muda wa siku mbili. Katika kura hiyo ya maoni asilimia 98.2 ya wananchi Waislamu wa Iran waliunga mkono kuanzishwa mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu nchini. Kuanzia hapo, kila mwaka ifikapo tarehe 12 mwezi Farvardin, Iran huadhimisha siku hii inayojulikana hapa nchini kwa jina la "Siku ya Jamhuri ya Kiislamu."