Apr 15, 2019 02:18 UTC
  • Jumatatu, Aprili 15, 2019

Leo ni Jumatatu tarehe 9 Sha'aban 1440 Hijiria, sawa na tarehe 15 April 2019 Miladia.

Siku kama ya leo miaka 959 iliyopita aliaga dunia Ibn Barraj mmoja wa mafaqihi na maulamaa mashuhuri wa Misri. Ibn Barraj alifahamika sana kwa jina la Trablosi kutokana na kuwa kwa muda fulani alikuwa na cheo cha kadhi katika mji wa Trablos yaani Tripoli huko kaskazini mwa Lebanon ya sasa. Msomi huyo wa Kiislamu alifunzwa na maulamaa kama vile Sayyid Murtadha na Sheikh Tusi. Ibn Barraj ni msomi mtajika wa Kiislamu ambaye fikra na mitazamo yake ilikuwa ikiheshimiwa na mafaqihi wakubwa wa zama hizo.

Siku kama ya leo miaka 863 iliyopita inayosadifiana na tarehe 9 Shaaban mwaka 577 aliaga dunia Abul Barakat Abdul Rahman bin Muhammad mashuhuri kwa lakabu ya Ibn Anbari fakihi na mtaalamu wa lugha wa mjini Baghdad. Alihitimu masomo yake katika skuli mashuhuri ya Nidhamiya mjini Baghdad na kutokana na kufaulu vizuri masomo yake na maarifa mengi aliyokuwa nao, alianza kufundisha katika skuli hiyo. Ibn Anbari ameandika vitabu na makala nyingi za kielimu. Kitabu cha al-Asrar al-Arabiyah ni moja ya athari mashuhuri ya alimu huyo.

Siku kama ya leo miaka 567 iliyopita, alizaliwa mchoraji na msanii mashuhuri wa kutengeneza vinyago wa Italia Leonardo da Vinci. Alionesha kipaji kikubwa cha kuchora akiwa bado mtoto mdogo na alikweya daraja za juu katika fani hiyo haraka mno. Mwaka 1506 Miladia da Vinci alichaguliwa kuwa mchoraji wa Mfalme Luis wa 12 kisha akawa mchoraji wa Mfalme Francis wa Kwanza. Mbali na uhodari wake katika kuchora na kutengeneza vinyago, Leonardo da Vinci pia alisomea fizikia na hisabati. Miongoni mwa kazi zake mashuhuri ni michoro ya kanisa kuu la mji wa Milan, mchoro wa picha ya "Tabasamu la Jugund," picha ya Mona Lisa na ya Karamu ya Mwisho ya Issa Masih (as). Leonardo da Vinci alifariki dunia mwaka 1519 akiwa na umri wa miaka 67.

Leonardo da Vinc

Siku kama ya leo miaka 107 iliyopita meli kubwa ya abiria ya Titanic ambayo ilitambuliwa kuwa nembo ya mafanikio makubwa ya viwanda vya meli vya wakati huo iligonga mwamba wa theluji na kugharibi katika Bahari ya Atlantic, katika safari yake ya kwanza kutoka bandari ya Southampon nchini Uingereza kuelekea New York, Marekani. Zama hizo Titanic ilitambuliwa kuwa meli kubwa zaidi na ya kifahari kuliko meli nyingine zote duniani. Watengenezaji wa meli hiyo walikuwa wakisema kuwa haingeweza kughariki na kuzama. Ni wasafiri 705 tu kati ya abiria wake wote 2207 waliokuwemo kwenye meli hiyo ndio waliookoka katika ajali hiyo. Ajali hiyo inatambuliwa kuwa ajali mbaya zaidi ya baharini na iliyosababisha idadi kubwa ya vifo vya watu duniani.

Meli ya Titanic

 

Siku kama ya leo miaka 73 iliyopita, alifariki dunia Ayatullah Sheikh Muhammad Taqee Bafaqi, alimu mkubwa na faqihi wa ulimwengu wa Kiislamu. Alizaliwa mwaka 1292 Hijiria katika eneo la Bafq, mjini Yazd nchini Iran. Baada ya kuhitimu masomo ya awali ya dini ya Kiislamu alielekea mjini Najaf, Iraq na kupata kusoma kwa maulama wakubwa wa zama hizo kama vile Allamah Akhund Khorasani, Sayyid Mohammed Kazem Yazdi na Sayyid Ahmad Karbalai. Baada ya Ayatullah Taqee Bafaqi kuishi mjini Najaf kwa kipindi cha miaka 19 alielekea mjini Qum, Iran na kujikita katika kazi ya ufundishaji. Aidha msomi huyo alikuwa miongoni mwa watu waliofanya maandalizi ya kumuhamishia mjini hapo Ayatullah Sheikh Abdul-Karim Haeri Yazdi na hatimaye kuasisi hauza ya kielimu ya Qum. Ayatullah Sheikh Muhammad Taqee Bafaqi hakuogopa chochote katika kuzuia machafu ya utawala wa Shah wa wakati huo nchini hapa hususan katika kupinga vikali tukio la kuingia wanawake wa ufalme huo katika haram ya Bibi Fatwimat Ma'asumah wakiwa katika mazingira machafu na bila ya hijabu. Kufuatia suala hilo tarehe Pili mwezi wa kwanza 1306 msomi huyo alikamtwa na maafisa wa utawala huo na kuteswa na kisha akabaidishwa mjini Ray. Alirejea mjini Qum baada ya mfalme Shah kukimbia nchi huku akifariki dunia akiwa na umri wa miaka 72 na kuzikwa katika haram ya Bibi Fatwimat Ma'asumah (as)  mjini hapo.

Ayatullah Sheikh Muhammad Taqee Bafaqi

Siku kama ya leo miaka 31 iliyopita, yaani sawa na tarehe 15 Aprili 1988, shirika la ujasusi la utawala bandia wa Israel MOSSAD lilimuua shahidi Khalil al Wazir maarufu kwa jina la Abu Jihad mwasisi na shakhsia nambari mbili wa Harakati ya Ukombozi ya Palestina PLO huko Tunis, Tunisia. Abu Jihad aliongozana na wenzake nchini Misri, na huko wakaamua kuanzisha harakati ya mapambano dhidi ya Wazayuni, na kuipatia jina la Harakati ya Ukombozi ya Palestina PLO.

Khalil al Wazir

Na siku kama ya leo miaka 25 iliyopita, ulitiwa saini mkataba wa kuanzisha Shirika la Biashara Duniani (WTO) nchini Morocco. Utangulizi wa kuasisiwa shirika hilo ulifanywa na Marekani na Uingereza wakati wa Vita vya Pili vya Dunia na kwa msingi huo, mwaka 1947 nchi 23 zilizoendelea zilitia saini makubaliano ya kuanzisha GATT. Makubaliano hayo yalisisitiza juu ya kufanyika mazungumzo ya kupunguza ushuru wa forodha na vizuizi vya biashara huru. Baadaye jumuiya ya GATT ilibadilishwa jina na kuwa WTO na hati yake kuanza kutekelezwa Januari mwaka 1995. Hata hivyo Marekani na nchi nyingine za Magharibi zimeliteka shirika hilo la kibiashara duniani na kulitumia kwa faida na maslahi yao wenyewe.