Jumatatu, 29 Aprili, 2019
Leo ni Jumatatu tarehe 23 Sha'aban 1440 Hijria mwafaka na tarehe 29 Aprili 2019.
Siku kama ya leo miaka 1136 iliyopita kulingana na kalenda ya Hijria, alifariki dunia Abu Muhammad Hassan Ibn Ali Atroosh, maarufu kwa lakabu ya Nasser Kabir, alimu na mwanamapambano mkubwa miongoni mwa wajukuu wa Mtume Muhammad (saw). Alizaliwa mwaka 230 Hijiria mjini Madina, na baada ya watawala wa Bani Abbas kuwaua na kuwabaidisha watu wa familia ya Mtume SAW akiwemo Imamu Hassan Askari (as), Ali Atroosh alipelekwa mjini Samarra, kaskazini mwa mji wa Baghdad, Iraq kwa amri ya watawala hao ikiwa ni baada ya baba yake kubaidishwa mjini hapo. Abu Muhammad Hassan Ibn Ali Atroosh alijifunza elimu ya dini mjini Baghdad na Kufa na kutokea kuwa msomi mkubwa huku akitabahari pia katika uwanja wa mashairi. Mbali na hayo alijihusisha na harakati za kisiasa ambapo katika kipindi cha mwamko wa Maalawi mjini Tabarestan, kaskazini mwa Iran, Atroosh alikimbilia katika eneo hilo. Baada ya kuanguka utawala huo, aliufufua huku akitawala sehemu kubwa ya maeneo ya kaskazini mwa Iran kwa uadilifu na usawa, sambamba na kueneza mafundisho ya dini ya Mtume Muhammad (saw). Katika harakati zake alifanikiwa kuwaingiza maelfu ya watu katika dini ya Uislamu. Vitabu vya 'Al-Bisat' 'Tafsir al-Utrush' na 'Imamatul-Kabir ni miongoni mwa makumi ya vitabu vilivyoandikwa na msomi huyo. ***
Katika siku kama ya leo miaka 707 iliyopita kulingana na kalenda ya Hijria, alifariki dunia Hussein bin Abdallah Tayyebi aliyekuwa na lakabu ya Sharafud-Deen, mpokezi wa hadithi na mwanafasihi mkubwa wa karne ya nane Hijiria. Abdallah Tayyebi alibobea katika elimu za fasihi ya lugha ya Kiarabu na alihesabiwa kuwa miongoni mwa shakhsia wakubwa na wasomi katika zama zake. Aidha alimu huyo alikuwa akitilia mkazo juu ya kufundisha tafsiri ya Qur'ani pamoja na hadithi. Vitabu vya 'Tafsirul-Qur'an' na 'Meshkat' ni miongoni mwa vitabu alivyoandika. ***
Miaka 623 iliyopita kwa mujibu wa kalenda ya Hijria, alizaliwa Nuruddin Abdul-Rahman Jami, mshairi na mwanafasihi mkubwa wa Kiirani wa karne ya 9 Hijria. Alizaliwa katika mji wa Jam ulioko katika mkoa wa Khorasan kaskazini mashariki mwa Iran. Alianza kujifunza elimu mbalimbali akiwa katika rika la ujana. Alikuwa na mapenzi na itikadi thabiti na watu wa Nyumba ya Bwana Mtume SAW. na katu hakuwahi kuwasifu wafalme na watawala.Silsilat al-Dhahab na Baharstan ni baadhi ya athari za Nuruddin Abdul Rahaman Jami. ***
Miaka 337 iliyopita, Peter the Great alichukua madaraka ya nchi huko Russia akiwa na umri wa miaka 10. Peter alikuwa ndugu wa Feodor katika kizazi cha tatu cha Tzar katika ukoo wa Romanov. Baada ya kuchukua madaraka Peter alivuliwa uongozi na dada yake na kubaidishwa katika kijiji kimoja karibu na mji wa Moscow. Baada ya muda Peter aliandaa jeshi kubwa na kwenda kupambana na dada yake. Katika vita hivyo Peter alishinda na kutawala nchi hiyo kwa mara nyingine. Kadhalika Peter alifanya marekebisho makubwa ndani ya Russia. Peter the Great alifariki dunia mwaka 1725. ***
Siku kama ya leo miaka 65 iliyopita, alizaliwa Henri Poincaré, mtaalamu wa sayansi na hisabati wa Ufaransa katika mji wa Nancy nchini humo. Poincare alikuwa mahiri katika somo la hisabati na alianza kufanya utafiti katika uwanja huo. Chunguzi mbalimbali zilizofanywa na mwanahisabati huyo wa Kifaransa kuhusiana na masuala ya uchanganuzi wa kimahesabu, mwangaza, umeme n.k zimetajwa kuwa muhimu na sahihi. ***
Katika siku kama ya leo miaka 91 iliyopita, sawa na tarehe 29 mwezi Aprili mwaka 1928 Miladia, nchini Uturuki herufi za Kilatini zilitambuliwa rasmi na kuchukua nafasi ya zile za Kiarabu. Hatua hiyo ilichukuliwa katika njama za kuipiga vita dini ya Kiislamu na badala yake kuingizwa tamaduni za Kimagharibi katika jamii ya wananchi Waislamu wa Uturuki. Mchakato huo ulianzishwa na Mustafa Kamal maarufu kama Ataturk kuanzia mwaka 1923. Mfumo wa Jamhuri ulishika hatamu za uongozi huko Uturuki chini ya Ataturk kuanzia mwezi Oktoba mwaka 1923 baada ya kuanguka kwa utawala wa Othmania uliodumu kwa miaka 623 nchini humo. ***
Miaka 74 iliyopita katika siku kama ya leo, majeshi ya waitifaki yalipata pigo kubwa mwishoni mwa Vita vya Pili vya Dunia. Vikosi vya nchi waitifaki wa Ulaya vilifanya shambulizi la pamoja dhidi ya Italia baada ya kusambaratishwa safu ya ulinzi ya Ujerumani. Italia ilikuwa muitifaki wa Ujerumani chini ya uongozi wa Benito Musolini. ***
Siku kama ya leo miaka 68 iliyopita, alifariki dunia Ludwig Wittgenstein, mwanafalsafa mashuhuri wa Austria. Alizaliwa mwaka 1889 Miladia mjini Vienna, mji mkuu wa nchi hiyo na baada ya kuhitimu masomo ya msingi aliendelea na masomo nchini Uingereza katika fani ya uhandisi. Kukutana kwake na Bertrand Russell, mwanafalsafa mkubwa wa Uingereza kulimvutia sana Ludwig Wittgenstein na kumfanya ajiunge na fani hiyo. Baada ya kusoma kitabu cha Russell alidai kwamba masuala yote ya falsafa yametatuliwa, hata hivyo baada ya miaka kadhaa alitambua kosa lake na mwaka 1929 alifikia daraja ya PHD katika falsafa na kufanikiwa kuwa mhadhiri katika chuo kikuu cha Cambridge. Ameacha athari kadhaa katika fani hiyo na moja ya athari hizo ni kitabu cha 'Tafiti za Kifalsafa'. ***
Na miaka 20 iliyopita katika siku kama ya leo ya tarehe 9 Ordibehesht mwaka 1378, wawakilishi wa duru ya kwanza ya Mabaraza ya Kiislamu ya Miji na Vijiji nchini Iran walianza kazi zao na siku hii inajulikana hapa nchini kwa jina la Siku ya Mabaraza. Kwa kuzingatia kwamba, katika Uislamu suala la mashauriano na kuwa na fikra moja lina umuhimu mno, katika Katiba ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran pia, Mabaraza yana nafasi muhimu na ni dhihirisho la urada ya wananchi katika mfumo wa kidini nchini Iran wenye ridhaa ya wananchi. Katika sheria hiii Mabaraza mbalimbali huchaguliwa na wananchi kwa ajili ya kuongoza masuala tofauti ya nchi ambapo Majlisi ya Ushauri wa Kiislamu (Bunge la Iran) na Baraza la Wanazuoni Wanazuoni Wanaomchagua Kiongozi Muadhamu ni miongoni mwa mabaraza hayo. ***