May 08, 2019 01:22 UTC
  • Jumatano, Mei 8, 2019

Leo ni Jumatano tarehe Pili Ramadhani 1440 Hijria inayosadifiana na tarehe 8 Mei 2019 Milaadia

Tarehe nane ya kila mwezi Mei inatambuliwa kuwa siku ya Msalaba Mwekundu na Hilali Nyekundu. Msalaba Mwekundu ni shirika la kimataifa ambalo liliundwa kwa ajili ya kutuliza machungu ya wanadamu na kulinda maendeleo ya sekta ya afya ya kijamii kwa mujibu wa mkataba wa Geneva, Uswisi hapo mwaka 1864 Miladia. Jean Henri Dunant raia wa Uswisi, alikuwa na nafasi kubwa katika kuundwa shirika hilo la kimataifa. Hii ni kwa kuwa mwaka 1862 alitoa pendekezo la kusaidiwa wagonjwa na majeruhi wa kijeshi, pendekezo ambalo lilipokelewa na asasi za masuala ya misaada ya kibinaadamu na kukubaliwa hapo baadaye na kongamano la kimataifa mjini Geneva mwaka 1864. Ni baada ya hapo ndipo shirika hilo la Msalaba Mwekundu likaundwa na kuanza kuenea duniani. Katika nchi za Kiislamu shirika hilo linaitwa kwa jina la Hilali Nyekundu.

Siku ya Msalaba Mwekundu na Hilali Nyekundu

 

Siku kama ya leo miaka 1100 iliyopita, alifariki dunia mjini Damascus, Syria Abdur-Rahman Zajaji Nahawandi, fasihi, mtaalamu wa lugha na mtaalamu wa sheria za Kiislamu wa karne ya nne ya Hijiria.  Nahawandi alizaliwa kusini magharibi mwa Iran na akiwa kijana alielekea mjini Baghdad, Iraq na kupata kusoma elimu ya sheria za Kiislamu na lugha kwa wasomi wakubwa wa zama zake kama vile Ibn Durayd. Baada ya muda Abdur-Rahman Zajaji Nahawandi alitokea kuwa mwalimu katika uga huo. Mwaka 311 Hijiria alielekea Sham ambapo aliishi huko hadi mwisho wa uhai wake. Miongoni mwa athari za msomi huyo ni pamoja na kitabu cha ‘Aamal Zajaji’ ‘Iidhaahul-Kaafi’ na ‘Iidhahu fi ilalin-Nahw.’ 

Abdur-Rahman Zajaji Nahawandi

 

Katika siku kama ya leo miaka 202 iliyopita James Parkinson aligundua ugonjwa wa Parkinson na namna unavyotokea. Kwa sababu hiyo ugonjwa huo ulipewa jina la tabibu huyo. Dalili za ugonjwa huo ni kama vile kutetemeka sana na kwa muda mrefu kwa ulimi, kichwa na mikono na kushindwa kuvuta miguu wakati wa kutembea hususan katika kipindi cha uzeeni na pia kukakamaa misuli katika sehemu yoyote ya mwili. Ugonjwa wa Parkinson unasababishwa na baadhi ya matatizo katika ubongo na hadi kufikia sasa hakuna dawa mujarabu iliyopatikana kwa ajili ya kutibu maradhi hayo.

James Parkinson

 

Siku kama ya leo miaka 225 iliyopita, Antoine Lavoisier msomi wa Ufaransa alinyongwa kufuatia kujiri harakati ya mapinduzi makubwa ya nchi hiyo. Lavoisier alikuwa mvumbuzi na msomi mashuhuri wa Ufaransa huku akiwa pia mwanzilishi wa kanuni ya kielimu ya elimu ya kemia. Licha ya kuhitimu awali masomo yake ya sheria, lakini kutokana na kwamba alipendelea sana elimu ya sayansi akaamua kuingia uwanja huo. Akiwa na miaka 25 alichaguliwa kujiunga na Chuo cha Kifalme cha Sayansi. Katika uwanja huo alifanikiwa kuvumbua gesi ya Oxygen na umuhimu wa matumizi na pia kuvumbua muundo wa hewa. Antoine Lavoisier ndiye msomi wa kwanza aliyethibitisha kuwa joto la mwili linatokana na mmeng'enyo wa sukari mwilini na kwa ajili hiyo akatambuliwa kuwa mwasisi wa elimu ya tiba na biokemia. Itafahamika kuwa, baada ya kujiri mapinduzi makubwa ya Ufaransa kila mtu aliyekuwa na mahusiano na utawala wa kifalme wa nchi hiyo alikamatwa na kuhukumiwa. Ni kwa msingi huo ndipo Antoine Lavoisier akatiwa mbaroni na kisha kuhukumiwa na kunyongwa katika siku kama ya leo mwaka 1794 Miladia akiwa na umri wa miaka 51.

Antoine Lavoisier