May 27, 2019 02:19 UTC
  • Jumatatu, Mei 27, 2019

Leo ni Jumatatu tarehe 21 ya mwezi Mtukufu wa Ramadhani mwaka 1440 Hijria sawa na tarehe 27 Mei mwaka 2019 Miladia.

Siku kama ya leo miaka 1400 iliyopita katika mwaka wa 40 Hijria Qamaria Ali bin Abi Talib AS Khalifa wa baada ya Mtume Muhammad SAW na mmoja wa watu wa Nyumba Tukufu ya Bwana Mtume alikufa shahidi. Siku mbili kabla ya hapo Imam Ali AS alielekea msikitini kwa ajili ya Sala ya asubuhi na akiwa katika sijda alipigwa upanga kichwani na Ibn Muljim aliyekuwa mfuasi wa tapo la Khawarij na kumpasua utosini. Imam Ali AS alikufa shahidi katika siku kama ya leo na hivyo kufikia saada aliyokuwa akiitaraji daima, yaani kufa shahidi katika njia ya Mwenyezi Mungu. Kuuliwa shahidi Imam Ali AS kulisababisha pigo na msiba usioweza kusahaulika wala kufutika kwa Uislamu na Waislamu.

 

Siku kama ya leo miaka 536 iliyopita katika mwaka 1482 Miladia alifariki dunia akiwa na umri wa miaka 82, Luca della Robbia, msanii mkubwa wa uhunzi wa Italia. Akiwa kijana alijifundisha kazi ya ufuaji dhahabu, hata hivyo aliachana na kazi hiyo baadaye na kujihusisha na uhunzi wa masanamu. Katika kipindi hicho alipata kuunda masanamu na athari mbalimbali za kale. Athari kadhaa za Luca della Robbia zipo katika majengo tofauti ya maonyesho duniani.

 

Na siku kama ya leo miaka 182 iliyopita sawa na tarehe 27 Mei 1837, ulitiwa saini mkataba wa amani kati ya Ufaransa na Amir Abdulqadir wa Algeria kiongozi wa wapigania uhuru wa nchi hiyo. Tangu mwaka 1832 baada ya mashambulizi ya jeshi la Ufaransa nchini Algeria Amir Abdulqadir aliendesha mapambano dhidi ya wavamizi huko Algeria na kusimama kidete dhidi yao kwa miaka kadhaa na kujulikana kama kiongozi wa wanamapambano wa Algeria dhidi ya Ufaransa. Baada ya kufikiwa makubaliano hayo maeneo mengi ya Algeria yaliyokuwa chini ya Ufaransa yalipewa uhuru.

Amir Abdulqadir

 

 

Tags