Jun 10, 2019 02:30 UTC
  • Jumatatu tarehe 10 Juni mwaka 2019

Leo ni Jumatatu tarehe 6 Shawwal 1440 Hijria sawa na Juni 10 mwaka 2019.

Katika siku kama ya leo miaka 655 iliyopita, alifariki dunia Ibn Bardes, malenga na mpokeaji wa hadithi wa Kiislamu. Ibn Bardes alizaliwa huko Ba'labak moja kati ya miji ya Lebanon na kuelekea katika mji wa Damascus baada ya kukamilisha masomo yake ya awali, ambapo alinufaika na elimu ya maulamaa maarufu wa zama hizo. Msomi huyo wa Kiislamu alisafiri katika nchi mbalimbali za Kiislamu na akaanza kufundisha baada ya kukamilisha masomo yake. Alikuwa mashuhuri baina ya watu kwa kushikamana na dini, kutakasa nafsi na maadili mema. Miongoni mwa vitabu vya msomi huyo ni al Iilamu fii Wafayatil Aalam.

Miaka 229 iliyopitaka katika siku kama ya leo inayosadifiana na tarehe 10 Juni 1790 vikosi vya Jeshi la Uingereza viliivamia ardhi ya Melaya inayojulikana hii leo kama Malaysia. Wakati huo Uholanzi ilikuwa ikiikoloni Maleya na kupora utajiri mkubwa wa nchi hiyo wa madini ya bati. Kwa kuingia vikosi vya Uingereza Maleya iliibidi Uholanzi ianze kuondoka nchini humo na ilipofikia mwaka 1824 Uholanzi ilikubali kuiachia Uingereza ardhi hiyo kwa sharti kwamba nayo iachiwe Indonesia ambayo ilikuwa ina umuhimu mkubwa kwa Uholanzi. Malaysia ilijipatia uhuru wake mwaka 1957 na Indonesia mwaka 1956.

Katika siku kama ya leo miaka 207 iliyopita, vita vya Marekani na Uingereza vilianza. Miongoni mwa matukio muhimu ya historia ya Marekani katika nusu ya kwanza ya karne ya 19 ni vita hivyo vilivyodumu kwa miaka miwili. Sababu ya kuanza vita hivyo inasemekana kuwa ni kuzingirwa Ufaransa na Uingereza kutokea baharini na kuzuiwa safari za meli za Marekani katika maji yanayozunguka nchi za Ulaya. Lakini pamoja na hayo Marekani ilikuwa na sababu zingine za kuanzisha vita hivyo, muhimu kati yazo ikiwa ni madai ya uungaji mkono wa siri wa Uingereza kwa Wahindi Wekundu wa Marekani dhidi ya serikali kuu ya nchi hiyo. Kufuatia vita hivyo, tarehe 18 Juni 1812 askari jeshi wa Marekani walivamia vituo na mali za Uingereza huko Canada na kuuteketeza mji wa Toronto. Vita hivyo vilipamba moto kiasi kwamba, mwezi Agosti 1814 Uingereza ilituma askari wake katika pwani ya mashariki ya Marekani na kuendesha vita hadi katika mji mkuu wa nchi hiyo, Washington DC. Hatimaye mazungumzo ya amani baina ya nchi mbili hizo yalitiwa saini huko Ubelgiji na kupelekea kusimamishwa vita hivyo mwezi Disemba mwaka huhuo wa 1814. 

Katika siku kama ya leo miaka 38 iliyopita, Bani Sadr Rais wa kwanza wa Iran baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu aliuzuliwa wadhifa wa Amiri Jeshi Mkuu wa majeshi yote kutokana kufanya hiyana na usaliti. Tangu awali baada ya kuchaguliwa kuwa Rais, Bani Sadr alikumbwa na kiburi na ghururi sana na akawa anafuatilia suala la kuviweka kando vikosi vya mapinduzi vilivyokuwa vitiifu kwa Imam Khomeini, Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu. Aidha Bani Sadr alikuwa akishirikiana na makundi yaliyokuwa yakipinga Mapinduzi ya Kiislamu. Bani Sadr alikwamisha utendaji wa serikali kutokana na kukwepa kwake kumkubali Waziri Mkuu Muhammad Rajai mmoja wa wanamapambano mashuhuri aliyekuwa amechaguliwa na Bunge kwa wingi wa kura. Ukwamishaji huo wa Bani Sard ulifikia kilele katika vita vya kichokozi vya Iraq dhidi ya Iran na kupelekea miji mingi ya Iran katika kipindi hicho cha vita kukaliwa kwa mabavu na utawala wa dikteta Saddam Hussein. Hatimaye katika siku kama ya leo, Imam Khomeini alimuuzulu Bani Sadr cheo cha Amiri Jeshi Mkuu. Siku chache baadaye Bunge lilipasisha kwa wingi wa kura mpango kutokuwa na imani na uwezo wa kisiasa Rais huyo.

Bani Sadr

Siku kama ya leo miaka 19 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 10 Juni mwaka 2000, alifariki dunia Rais Hafidh Assad wa Syria baada ya kuugua kwa muda mrefu. Hafidh Assad alizaliwa mwaka 1930 na aliteuliwa kuwa kamanda wa vikosi vya Jeshji la Anga la Syria mwaka 1964, miaka mitatu baadaye alichaguliwa kuwa Waziri wa Ulinzi wa nchi hiyo. Ilipofika mwaka 1970 kupitia mapinduzi ya kijeshi, Hafidh Assad alitwaa madaraka ya nchi hiyo na baadaye kuchaguliwa kuwa kiongozi wa chama cha Baath. Miongoni mwa sifa za siasa za nje za Syria wakati wa urais wa Hafidh Assad, zilikuwa ni kutofanya mapatano na utawala wa Kizayuni wa Israel na kuimarisha uhusiano na nchi zinazopinga Uzayuni kama Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Hafidh Assad

 

Tags