Jun 19, 2019 05:00 UTC
  • Jumatano tarehe 19 Juni 2019

Leo ni Jumatano tarehe 15 Shawwal 1440 Hijria sawa na Juni 19 mwaka 2019

Siku kama ya leo miaka 1188 iliyopita inayosadifiana na tarehe 15 Mfunguo Mosi Shawwal mwaka 252 Hijria, alifariki dunia Abdul-Adhim Hassani. Mtukufu huyu ni miongoni mwa wajukuu wa Mtume Muhammad SAW kupitia shajara ya Imam Hassan Al-Mujtaba (AS). Abdul-Adhim al Hassani alikuwa mashuhuri sana kwa karama zake nyingi. Maimamu watukufu walithibitisha ukweli na uchamungu wake na walikuwa wakinukuu hadithi kutoka kwake. Baada ya kushadidi dhulma na ukandamizaji wa utawala wa Bani Abbas, Abdul-Adhim al Hassani alilazimika kuhajiri na kuhamia mjini Rey kusini mwa Tehran ya leo. Mtukufu huyo anajulikana pia kama shahidi ambaye aliuawa kwa kupewa sumu. Haram Tukufu ya Abdul-Adhim Hassani ipo katika mji wa Rey na wapezi wa Ahlul Bayt AS kutoka kona mbalimbali za dunia humiminika katika eneo hilo kwa ajili ya kwenda kufanya ziara.

Haram ya Sayyid Abdul Adhim al Hassani, Rey

Siku kama ya leo miaka 192 iliyopita aliaga dunia mwanazuoni mkubwa wa Kiislamu Seikh Muhammad Taqi Razi katika mji wa Isfahan nchini Iran. Sheikh Taqi Razi maarufu kwa jila la Agha Najafi, alielekea katika mji mtakatifu wa Najaf kwa ajili ya elimu ya juu ya kidini baada ya kukamilisha elimu ya msingi. Alipata elimu kwa wanazuoni mashuhuri kama Mirza Muhammad Hassan Shirazi na Sheikh Mahdi Kashiful Ghitaa. Baada ya kurejea Isfahan, Sheikh Agha Najafi alikuwa marejeo ya Waislamu katika masuala ya kidini na kisheria. Alikuwa mstari wa mbele kupambana na wakoloni kupitia harakati iliyopewa jina la Harakati ya Tumbaku. Vitabu mashuhuri vya mwanazuoni huyo ni pamoja na "Anwarul Arifin", "Asrarul Ayat" na "Al-Ijtihad Wattaqlid".

Siku kama ya leo miaka 152 iliyopita inayosadifiana na tarehe 19 Juni 1867, Maximilian mwana wa mfalme wa Austria ambaye aliikalia kwa mabavu Mexico, alinyongwa na wapigania uhuru wa nchi hiyo. Baada ya Benito Juarez kujinyakulia urais wa Mexico mwaka 1855, aliwakata mikono wazungu na kupunguza nguvu za Kanisa nchini Mexico. Hatua hiyo iliwakasirisha mno wazungu na wakoloni wa Ulaya waliokuwa wakiongozwa na Ufaransa, na kulazimika kutuma jeshi nchini Mexico kwa shabaha ya kulihami Kanisa pamoja na wawekezaji nchini humo.

Siku kama ya leo miaka 142 iliyopita inayosadifiana na tarehe 19 Juni 1877, Enrico Forlanini mhandisi wa Kiitalia alifanikiwa kufanya majaribio ya kwanza ya kurusha angani helikopta katika mji wa bandari wa Alexandria nchini Misri. Helikopta hiyo iliboreshwa zaidi na mtaalamu wa Kipolandi, na ubunifu huo ukaandikwa kwa jina lake.

Siku kama ya leo miaka 58 iliyopita nchi ya Kuwait iliyoko katika eneo la Ghuba ya Uajemi ilijipatia uhuru baada ya kufutwa makubaliano ya ukoloni ya mwaka 1899 kati ya Uingereza na Kuwait. Katikati ya karne 18, iliasisiwa silsila ya al Swabah nchini humo na ilipofikia mwishoni mwa karne ya 19, Kuwait iliomba uungaji mkono wa Uingereza kwa shabaha ya kukabiliana na dola la Othmaniya. Mwaka 1899, Uingereza na Kuwait zilifanya makubaliano ambayo yaliiweka Kuwait chini ya ukoloni wa Uingereza.

Bendera ya Kuwait

 

Na siku kama ya leo miaka 42 iliyopita, sawa na tarehe 29 Khordad 1356 Hijria Shamsia, alifariki dunia Dakta Ali Shariati mwandishi na msomi wa zama hizi wa Kiirani mjini London, Uingereza. Dakta Shariati alipata elimu yake ya juu katika taaluma ya fasihi sambamba na kuwa mstari wa mbele katika mapambano dhidi ya utawala wa mfalme hapa nchini. Dakta Shariati alikuwa bega kwa bega na Shahidi Mutahhari na Shahidi Bahonar, katika kuanzisha Husseiniya ya Ershad mjini Tehran kwa shabaha ya kuzikomaza fikra za tabaka la vijana. Ameandika zaidi ya vitabu 200 na miongoni mwao ni 'Uislamu na Mwanadamu', 'Historia ya Ustaarabu' na 'Fatima ni Fatima'.

Ali Shariati

 

Tags