Jumanne, Juni 25, 2019
Leo ni Jumanne tarehe 21 Mfunguo Mossi Shawwal 1440 Hijria sawa na Juni 25 mwaka 2019 Milaadia.
Siku kama ya leo miaka 1348 iliyopita mwafaka na leo, ardhi ya Andalusia iliyoko Uhispania ya sasa ilikombolewa na jeshi la Kiislamu chini ya uongozi wa Twariq bin Ziyad. Twariq akiwa na wanajeshi elfu 12 alivuka kwa meli lango bahari lililoko kati ya Morocco na Uhispania ambapo hii leo limeitwa kwa jina lake la Jabal Tāriq.
Miaka 1086 iliyopita mwafaka na leo, alifariki dunia Ibn Habban, mtaalamu wa hadithi, elimu ya fiq'hi na mwanahistoria mashuhuri wa karne ya 14 Hijiria. Alipata elimu ya msingi kwa walimu mashuhuri wa zama zake na kisha akaelekea Neishabur kaskazini mwa mashariki mwa Iran, ambao katika kipindi hicho ulikuwa ni moja ya vituo muhimu vya kielimu. Ibn Habban anahesabika kuwa mtu mwenye nadharia muhimu katika elimu ya hadithi. Miongoni mwa athari muhimu za msomi huyu mkubwa ni pamoja na kitabu cha"At-Thuqat" na Rawdhatul-Uqalaai wa Nazahatul-fudhalaai."

Siku kama ya leo miaka 197 iliyopita kundi la watumwa wa Marekani wenye asili ya Afrika ambao waliachiwa huru na wamiliki wao wazungu wa nchi hiyo, walirejea Afrika na kuanzisha makazi katika ardhi ambayo leo hii inajulikana kama Liberia. Raia hao weusi wa Marekani walianzisha harakati ya ukombozi mwanzoni mwa karne ya 19 kwa lengo la kujiondoa utumwani na kuunda nchi yao. Kwa sababu hiyo kundi la Wamarekani weusi wenye asili ya Afrika lilihamia Magharibi mwa Afrika na kuasisi nchi ya Liberia kwa kusaidiwa na taasisi ya wahamiaji, baada ya kuwa utumwani kwa miaka mingi huko Marekani. Awali Liberia ilikuwa ikiendeshwa kama moja ya majimbo ya Marekani, lakini mwaka 1847 nchi hiyo iliasisi mfumo wa jamhuri na rais wake wa kwanza akawa Joseph Roberts, mtumwa kutoka jimbo la Virginia.
Siku kama ya leo miaka 69 iliyopita, kufuatia harakati za kichokozi za Marekani katika eneo la Peninsula ya Korea, Korea Kaskazini iliishambulia Korea Kusini na kusonga mbele haraka upande wa nchi hiyo hasimu. Hata hivyo kupasishwa azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, Marekani na nchi nyingine 15 zilituma askari wao kwa ajili ya kukabiliana na kuzuia kusonga mbele zaidi Korea Kaskazini sambamba na kuisaidia Korea Kusini. Hatimaye majeshi hayo ya kigeni kwa kushirikiana na Korea Kusini yaliweza kuizuia kusonga mbele Korea Kaskazini. Hata hivyo hatua ya China ya kuingilia kati vita hivyo kwa maslahi ya Pyongyang, kulifanya uvamizi wa Marekani na vikosi vya kigeni kufikia tamati katika eneo hilo. Ni baada ya hapo ndipo kukaanza mchakato wa mazungumzo ambapo mwaka 1953 kulitiwa saini makubaliano ya usitishaji vita hivyo. Hata hivyo hadi sasa mkataba rasmi wa amani baina ya Korea mbili bado haujatiwa saini na daima hali ya ushindani imeendelea kushuhudiwa baina yao, huku Marekani ikiendeleza siasa zake za uchochezi katika eneo hilo.

Siku kama ya leo miaka 56 iliyopita baada ya kutiwa mbaroni Imamu Khomein (MA) Mwasisi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran na Shirika la Intelijinsia na Usalama wa Taifa la Iran wakati huo, maarufu kwa jina la SAVAK, alihamishiwa katika kambi ya Eshratabad. Siku 40 baada ya kuzuiliwa katika kambi hiyo, Imamu kwanza alibaidishwa katika nchi ya Uturuki na mwaka mmoja baadaye akabaidishiwa tena nchini Iraq. Kwa kipindi cha miaka 13 Imamu Khomein aliendeleza harakati za mapinduzi kupitia wanafunzi wake. Katika kipindi hicho, wanafunzi hao walikuwa wakifanya mawasiliano na watu wa Iran na kuwafikishia ujumbe kutoka kwake. Imamu alirejea nchini Iran, mwezi Bahman mwaka 1357 sawa na Februari mwaka 1979 Miladia na kuanguka rasmi utawala wa kifalme wa Shah siku 10 tangu aliporejea nchini Imam (MA).
Siku kama ya leo miaka 44 iliyopita, yaani tarehe 25 Juni mwaka 1975, Msumbiji ilipata uhuru. Mwishoni mwa karne ya 15 kundi moja la mabaharia wa Kireno likiongozwa na mvumbuzi mashuhuri Vasco da Gama lilifika Msumbiji na kuanzia hapo mabaharia hao wakaanza kuikoloni nchi hiyo, ukoloni ambao uliendelea kwa karne tano. Wareno walianza kupora maliasili na utajiri wa Msumbiji na makumi ya maelfu ya wananchi wapigania ukombozi wa Msumbiji waliuawa wakitetea nchi yao.
Na siku kama ya leo miaka 31 iliyopita yaani tarehe 4 Tir 1367 Hijria Shamsiya, ndege za utawala wa Saddam Hussein, dikteta wa zamani wa Iraq, kwa mara nyingine tena ziliwashambulia kwa mabomu ya kemikali wapiganaji wa Kiirani waliokuwa katika visiwa vya Majnun. Mamia ya wanajeshi wa Iran waliuawa shahidi na wengine kujeruhiwa katika mashambulizi hayo ya kinyama ya utawala wa Saddam. Utawala wa zamani wa Iraq ulitumia silaha za maangamizi ya umati za kemikali tangu mwanzoni mwa vita vyake dhidi ya Iran mwaka 1359 Hijria Shamsiya, na kuzidisha matumizi ya silaha hizo sambamba na ushindi wa wapiganaji wa Iran.
