Jun 25, 2019 14:31 UTC

Ni matumaini yangu kuwa hamjambo wapenzi wasikilizaji na karibuni kutegea sikio sehemu ya 25 ya kipindi hiki cha Katika Maktaba ya Imam Khomein (MA) ambacho kinakujieni kwa mnasaba wa kutimia miaka 40 ya Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran.

Ndugu wasikilizaji kama tulivyosema katika vipindi vilivyopita, baada ya Ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu na baada ya kuondolewa mfumo wa kitwaghuti uliokuwa ukimtumia mwanamke kama chombo cha starehe na anasa tu, kwa mara nyingine heshima ya mwanamke ilihuishwa nchini Iran ambapo hii leo anaweza kutumia vyema nafasi yake ndani ya mfumo wa Kiislamu. Aidha mwanamke ameweza kushika nafasi muhimu katika jamii na kuwa na taathira serikalini. Hii leo baada ya kupita miaka 40 ya Ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu, wanawake wanasimamia vyeo na nafasi muhimu katika Jamhuri ya Kiislamu, ambapo pia wameteuliwa kwa wingi katika nafasi za uwakilishi katika Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu (yaani bunge) kama ambavyo pia idadi yao kimasomo ni kubwa kuliko hata wanaume nchini. Mbali na hayo ni kwamba, wakati mwingine asilimia kubwa ya ufaulu wa wanafunzi katika shule za kawaida na vyuo vikuu huhodhiwa na wanafunzi wa kike kuliko wa kiume.

Jamii ya wanawake nchini Iran chini ya mfumo bora wa Uislamu

Suala hilo linashuhudiwa mara nyingi katika sekta tofauti za maisha ya wananchi wa Iran kama ambavyo hata uadilifu wa kijamii upande wa kijinsia umeongezeka kwa kiasi kikubwa hapa nchini. Tukiwa tunakamilisha suala la nafasi chanya ya mwanamke katika mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu, hii leo tumekusudia kuzungumzia taathira ya wanawake katika jamii salama nchini hapa, hivyo endeleeni kuwa nami hadi mwisho wa kipindi.

****

Ndugu wasikilizaji, kama tulivyoashiria katika vipindi vilivyopita, katika kuinua hadhi ya mwanamke Imam Khomeini (MA) aliitangaza siku ya kuzaliwa Bibi Fatwimat Zahra (as) kuwa siku ya mwanamke nchini hapa ili kumtangaza Bibi Fatwimah (binti ya Mtume Muhammad saw) kuwa kiigizo chema na halisi kwa wanawake wa Iran. Kama ambavyo pia katika nyuga za kifamilia, malezi bora ya watoto yameshika nafasi ya kwanza kwenye uwanja wa mabadiliko ya kifikra na kiutamaduni ambapo Bibi Fatwimah pamoja na mume wake, Ali Bin Abi Twalib (as) walikuwa na umuhimu katika kutengeneza malezi bora yaliyobakia milele kwenye nyuga za kiakhlaqi, kisiasa na kijamii.

Bibi Fatwimat Zahra (as) kiigizo chema cha wanawake duniani

Katika moja ya jumbe zake kwa mnasaba wa kuzaliwa Bibi Fatwimat Zahra (as), Imam Khomeini sambamba na kutoa pongezi kwa mnasaba wa siku hiyo kwa watu wote hususan wanawake wa Iran alisema: “Ninatoa mkono wa kheri na fanaka kwa watu watukufu wa Iran hususan wanawake. Siku ya mwanamke ni siku yenye baraka, ni siku ambayo amezaliwa mtu mwenye nuru na ambaye anaakisi fadhila za ubinaadamu na thamani kubwa za khalifa wa Mwenyezi Mungu ulimwenguni. Ni siku yenye fahari ya kuzaliwa mwanamke ambaye ameleta miujiza ya kihistoria na fakhari duniani. Mwanamke ambaye ndani ya chumba kidogo na nyumba isiyo na thamani yoyote ya kimaada alilea watu ambao mwanga wao uliangaza kutoka ardhini hadi mbinguni. Rehema na amani ya Mwenyezi Mungu iwe juu ya nyumba hii isiyo na thamani ya kimaada (ya kawaida kabisa) ambayo inaakisi mwanga wa utukufu wa Mwenyezi Mungu na eneo la malezi ya kizazi bora cha wanadamu.” Hotuba yake ya tarehe 25/1/1361.

*****

Kama kwanza ndio unafungulia redio yako, kipindi kilicho hewani ni sehemu 25 ya mfululizo wa vipindi vinavyozungumzia nadharia na mitazamo ya Mwasisi wa Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran yaani Imam Khomeini (MA), kinachokujieni kupitia Idhaa ya Kiswahili Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Kadhalika akiashiria nafasi muhimu ya wanawake katika ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu na kufelisha njama za madola ya kibeberu na kuporomoka misingi ya ufisadi wao katika jamii, aliitaja siku ya mwanamke kuwa fursa bora ya kuifanya jamii yote ya mwanadamu kuweza kujifakharisha na kuinuliwa thamani ya mwanamke na maendeleo yake katika mfumo wa Kiislamu kwa kusema: “Mwamko wa Kiislamu na kwa baraka ya Uislamu umeleta mabadiliko katika nafsi ya mwanaume na mwanamke ndani ya jamii kiasi kwamba hakujawahi kushuhudiwa mfano wake katika kipindi cha miaka 100 iliyopita. Nyinyi watu wa Iran mmeona kwamba wanawake watukufu na waliojitolea wa nchi hii walikuwa bega kwa bega na wanaume na kuweza kuvunja nguzo za utawala wa kifalme na kwa hakika sisi sote tumetegemea mwamko na hatua yao hiyo. Na baada ya kuyashinda madola ya kibeberu na matawi yao ya uharibifu, tunaweza kuzungumzia haki ya mwanamke na maendeleo yake ndani ya Jamhuri ya Kiislamu.” Ujumbe wa Imam kwa mnasaba wa siku ya mwanamke tarehe 15/2/1359.

Hakuna ubora kati ya mwanamke na mwanamume ispokuwa kwa uchaji-Mungu pekee

Katika sehemu nyingine Imam Khomeini anasema: “Ninajifakharisha kwa wanawake wa Iran ambao ndani yao kumepatikana mabadiliko ambayo yamesambaratisha njama za kishetani na wamethibitisha kwamba wanawake watukufu wa Kiislamu hawajapotea na kwamba njama hizo chafu za Magharibi na Wamagharibi kamwe hazitowadhuru.” Ujumbe wake katika siku ya mwanamke tarehe 5/2/1360.

******

Aidha Imam Khomeini (MA) alisema kuwa usalama na ufisadi wa jamii unatokana na usalama na ufisadi wa wanawake na kwamba mwanamke ni kiumbe pekee ambaye anaweza kuipotosha au kuongoza jamii kuelekea kwenye matukufu ya kibinaadamu. Katika uwanja huo anasema: “Nafasi ya wanawake duniani ni ya kipekee. Usalama na upotofu wa jamii fulani unatokana na usalama na upotofu wa wanawake ndani ya jamii hiyo. Mwanamke ni kiumbe pekee ambaye anaweza kulea katika jamii watu wema na walio na thamani za juu kiutu na pia anaweza kuiongoza jamii hiyo kinyume na hali hiyo.” Ujumbe wake kwa mnasaba wa siku ya mwanamke tarehe 25/1/1361. Katika sehemu nyingine Imam anazungumzia nafasi ya wanawake katika kulea  jamii iliyo salama na watu bora wa jamii kwa kusema: “Mlezi wa wanadamu ni mwanamke. Ubora na ufisadi wa nchi mbalimbali unategemea mwanamke ambaye malezi yake yanaweza kumrekebisha mwanadamu, kama ambavyo malezi yake sahihi yanaimarisha nchi. Chanzo cha utukufu wote kinatoka kwa mwanamke na kwa hakika mwanamke anatakiwa kuwa chimbuko la mema yote.” Ujumbe wake kwa mnasaba wa siku ya mwanamke tarehe 26/2/1358. Mbali na hayo Imam Khomeini (MA) aliifananisha nafasi chanya ya kimalezi ya mwanamke kuwa ni sawa na Qur’ani na kuhusiana na hilo aliamini kwamba iwapo nafasi ya kumrekebisha mwanadamu ya wanawake ndani ya jamii itapokonywa kutoka kwa viumbe hao (wanawake), basi jamii itaelekea kwenye mporomoko na maangamizi.

Wanawake na wanaume wote ni sawa ispokuwa kwa uchaji-Mungu wao

Kuhusiana na hilo anasema: “Wanaume wanayo haki ya kuwasimamia watu, lakini wanawake wanayo haki zaidi yao. Wanawake wanalea na kukuza wanaume mashujaa. Qur’an Tukufu ni mrekebishaji wa mwanadamu na mwanamke pia ni mrekebishaji wa mwanadamu. Jukumu la wanawake ni kulea na kuwajenga wanadamu, hivyo iwapo mataifa yatapokonywa nafasi hiyo ya malezi na ujenzi wa mwaadamu, ni wazi kuwa matifa hayo yatakumbwa na mporomoko wa maadili na upotovu. Ni wanawake ndio wanaoyafanya mataifa kuwa yenye nguvu na shujaa.” Hotuba yake mbele ya wanawake wa mji wa Qum tarehe 12/11/1358.

*****

Kadhalika Imam Khomeini aliitaja ndoa kuwa uwanja wa kuzuia upotovu katika jamii ya mwanadamu na sababu ya kupatikana jamii salama. Pia aliitaja ndoa kuwa inayokinga matamanio na ghariza na kuyafanya maisha kwenda sawa na mafundisho ya Mitume wa Mwenyezi Mungu na hivyo kupatikana saada ya dunia na mafanikio ya Akhera kwa kusema: “Lengo la ndoa ni kuzuia upotovu katika jamii. Kwa kuyawekea mipaka matamanio jumla, Mitume wa Mwenyezi Mungu walitangaza idara hiyo (yaani ndoa) kuwa eneo la kuzuia ufisadi na machafu. Sio msingi wa matamanio kwa sababu hilo ni jambo la kimaumbile linalopaswa kuchukua mkondo wake wa kawaida, lakini linapasa kuwekewa mipaka. Iwapo malezi na mafunzo yalifundishwa na Mitume yatatekelezwa ipaswavyo, ni wazi kuwa dunia ya mwanadamu itarekebika na kupatikana mfumo mmoja na hivyo ukiukaji huu, ukatili na tofauti mbalimbali za kimatabaka hazitakuwepo na wakati huohuo kujidhaminia maisha mazuri na ya kudumu milele. Fanyeni juhudi za kutoa mafunzo na kuwalea wanadamu ili wapate kutoka katika mipaka ya unyama na kustawi kibinadamu na kiutu.” Hotuba yake mbele ya wanawake tarehe 16/4/1358.

Wapenzi wasikilizaji sehemu ya 25 ya kipindi hiki cha Katika Maktaba ya Imam Khomeini (MA) ambacho kinakujieni kwa mnasaba wa kutimia miaka 40 ya Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran na kupitia Idhaa ya Kiswahili, Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, inaishia hapa kwa leo. Mimi ni Sudi Jafar, kwaherini.  

 

 

Tags