Jul 10, 2019 10:37 UTC

Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur’ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SW, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu. Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur’ani.

Hii ni darsa ya 835 na sura tunayoizungumzia hivi sasa ni ya 38 ya S’aad. Tunaianza darsa yetu kwa aya ya 79 hadi 81 ambazo zinasema:

قَالَ رَبِّ فَأَنظِرْنِي إِلَىٰ يَوْمِ يُبْعَثُونَ

Akasema: Mola wangu Mlezi! Nipe muhula mpaka siku watakapo fufuliwa viumbe.

قَالَ فَإِنَّكَ مِنَ الْمُنظَرِينَ

Mwenyezi Mungu akasema: Basi hakika wewe umekwisha kuwa miongoni mwa walio pewa muhula,

إِلَىٰ يَوْمِ الْوَقْتِ الْمَعْلُومِ

Mpaka siku ya wakati maalumu.

Katika darsa iliyopita tulisema kuwa, baada ya Allah kutoa amri  kwa malaika ya kumsujudia Adam, Iblisi alikataa kutii amri hiyo na kutokuwa tayari kuonyesha unyenyekevu mbele ya Adam. Lakini ubaya wa kosa la Iblisi haukuwa wa kukataa kusujudu tu, bali ni kwamba, badala ya kutubia na kuonyesha majuto kwa kitendo alichofanya cha kuasi kutii amri ya Allah, alitaka athibitishe kuwa yeye ni mbora kuliko Adam na kwa njia hiyo kuhalalisha na kutetea kitendo alichofanya. Na hiyo ndiyo sababu iliyomfanya alaaniwe na kuwekwa mbali na rehma za Mwenyezi Mungu. Aya tulizosoma zinasema: Wakati alipotimuliwa na kuwekwa mbali na rehma za Allah, Iblisi alimwomba Mola ampe muhula mpaka Siku ya Kiyama na kumrefushia umri wake hadi wakati huo. Lakini ombi hilo la shetani la kutaka apatiwe muhula halikuwa la kutaka kusawazisha kitendo kiovu alichofanya huko nyuma, bali ni kwa ajili ya kuwapotosha wanadamu, ili kulipiza kisasi. Kwa hakika, kosa jengine alilofanya Iblisi ni kwamba, badala ya kujitambua yeye mwenyewe kuwa ndiye mkosa, alimbebesha lawama Adam na kusema: Huyu Adam ndiye aliyesababisha mimi kulaaniwa na kuwekwa mbali na rehma za Mwenyezi Mungu! Muhula huo alioomba apatiwe Iblisi, ulikubaliwa kwa hekima ya Mola; lakini si mpaka Siku ya Kiyama, bali ni kwa muda maalumu ambao anaujua Yeye Allah. Muda huo unaweza ukawa ni siku kitakapomalizika kipindi cha kuishi wanadamu katika sayari ya dunia, au siku Hujja wa Mwenyezi Mungu, Imam wa Zama, Imam Mahdi (as) atakapotawala ulimwengu mzima, au siku nyingine ambayo Allah pekee ndiye mwenye kuijua. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba, badala ya kuomba msamaha kwa Allah, kiburi na ghururi ya Iblisi vilimfanya aombe kupatiwa muhula wa kulipiza kisasi kwa Adam na kizazi chake. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa, ni rahisi na sahali kwa Mwenyezi Mungu kuwarefushia umri baadhi ya viumbe. Humpa umri mrefu yeyote anayeona kuna maslaha ya kumfanyia hivyo; awe ni mtenda mema au mabaya. Aya hizi aidha zinatuelimisha kwamba, kasoro ya Iblisi haikuwa ni kukosa utambuzi sahihi wa kumjua Allah na Siku ya Kiyama, bali ilitokana na upotofu wake, moyo wa kiburi, kujikweza na hulka ya ukaidi aliyokuwa nayo. Hulka hiyo ndiyo iliyomfanya Iblisi apinge na kukaidi kutekeleza amri ya Allah.

Darsa yetu ya leo inahitimshwa na aya ya 82 na 83 ambazo zinasema:

قَالَ فَبِعِزَّتِكَ لَأُغْوِيَنَّهُمْ أَجْمَعِينَ

Akasema (Iblisi): Naapa kwa utukufu wako, bila ya shaka nitawapoteza wote,

إِلَّا عِبَادَكَ مِنْهُمُ الْمُخْلَصِينَ

Isipokuwa wale waja wako miongoni mwao waliosafishwa.

Tumesema kuwa shetani alimwomba Allah amrefushie umri wake; na Allah SW akamkubalia ombi lake hilo kwa ajili ya muda maalumu ambao ni Yeye Mola ndiye aujuaye. Lakini baada ya Allah kumpa muhula huo, shetani alitamka kwamba lengo la kuomba apewe muhula huo ni kutaka awaghilibu na kuwapotosha wanadamu, jambo ambalo aliapa kuwa atahakikisha analifanikisha; badala ya kutaka apewe muhula ili kujirekebisha na kusawazisha kosa alilofanya. Ajabu ni kwamba, shetani ameiapia izza na utukufu wa Allah SW kwa ajili ya kuwapotosha wanadamu. Hii Iblisi kudai kwamba anaweza kuwapotosha wanadamu wote, huo kwa kweli ni upeo wa juu kabisa wa kuonyesha kiburi kwa Allah SW na kuamini kwake kwamba, mwanadamu ni kiumbe dhaifu na asiye na uwezo wowote. Ilhali kwa mujibu wa aya za Qur'ani ni watu wanaomfuata shetani tu ndio watakaopotea; na kimsingi, shetani hawezi kumteza nguvu na kumlazimisha mtu amfuate. Na sababu ni kuwa wanadamu wana hiari ya kuamua na wanao uwezo wa kukabiliana na wasiwasi wa shetani. Ni kama inavyoeleza aya ya 20 ya Suratu-Saba'a kwamba, baadhi ya waumini hawamfuati shetani. Na yeye shetani mwenyewe pia, baada ya madai yake ya ujumla kwamba atawapotosha wanadamu wote, alikiri kwamba, hawezi kuwaathiri wala kuwa na ushawishi juu yao waja wa kweli na wenye ikhlasi kwa Allah. Ni wazi kwamba Mitume na Maimamu ni waja wa Mwenyezi Mungu wenye ikhlasi iliyokamilika; wao wamekingika na kufanya aina yoyote ya makosa na madhambi; na kwa istilahi ya kidini, ni waja maasumu. Kwa upande wa watu wengine, nao pia watasalimika na wasiwasi na ushawishi wa shetani kulingana na kiwango cha ikhlasi waliyo nayo na kadiri watakavyozivua nyoyo zao na mapenzi ya dunia. Ama kuhusu hekima ya Allah ya kumpa Iblisi muhula aliotaka kwa ajili ya kuwapotosha watu, kuna rai kadhaa zilizotolewa kuhusiana na suala hilo. Lakini kwa ujumla tunaweza kusema kuwa, Mwenyezi Mungu SW amemuumba mwanadamu na maumbile ya kuwa na mamlaka na hiari ya kuamua; na sharti la hiari hiyo ni kuwepo njia tofauti mbele ya kiumbe huyo, na yeye kuweza kwa hiari yake kuchagua anayopenda kufuata. Kwa upande mwingine, kwa vile Allah SW ametaka mwanadamu afikie kwenye ukamilifu wa kiutu; sharti la kufikia ukamilifu huo ni kufanya juhudi na jitihada na kuwa na muqawama na istiqama. Kama ilivyo katika kuufikia utukukaji na ukamilifu wa kielimu, ambapo ni lazima mtu aache kupenda raha, na awe tayari kuvumilia baadhi ya tabu; sharti la kujengeka na kukamilika kimaanawi ni kuwa na istikama ya kudhibiti ghariza za maovu na maasi. Tuelewe pia kwamba, wasiwasi wa shetani huwa daima unazichochea ghariza na matamanio ya kinafsi ya mtu. Na tab’an baadhi ya watu wenye nafsi dhaifu, husalimu amri kwa adui mwenye kutia wasiwasi, yaani shetani, na si hasha baadhi ya watu wakamfuata na kujiunga na jeshi lake. Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba, mwanadamu, katika maisha yake yote, anakabiliwa na hatari ya wasiwasi wa shetani na wala asijihisi kuwa yuko salama na balaa la wasiwasi huo. Kwa sababu Iblisi ameapa kuwa atahakikisha anawapoteza wanadamu wote. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa, baadhi ya wakati, dhambi moja kubwa huwa utangulizi wa madhambi mengine makubwa zaidi. Shetani alifanya dhambi moja ambayo ni kukataa kumsujudia Adam, lakini dhambi hiyo ikawa utangulizi wa dhambi kubwa zaidi, ambayo ni kutaka kuwapotosha na kuwatia wasiwasi wanadamu katika zama zote za historia. Wa aidha aya hizi zinatuelimisha kwamba, kuutakasa moyo na mapenzi ya asiyekuwa Allah na kuwa na ikhlasi katika amali, ndilo sharti la kunusurika na mtego wa Iblisi na kumkinga mtu na wasiwasi wa shetani. Wapenzi wasikilizaji, darsa ya 835 ya Qur’ani imefikia tamati. Tunamwomba Allah atulinde na vitimbi vya wasiwasi wa shetani na atuwezeshe kumfanya adui kama yeye alivyo adui kwetu. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh…/

 

Tags