Jul 10, 2019 10:40 UTC

Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur’ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SW, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu. Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur’ani.

Hii ni darsa ya 836 na sura tunayoizungumzia hivi sasa ni ya 38 ya S’aad. Tunaianza darsa yetu kwa aya ya 84 na 85 ambazo zinasema:

قَالَ فَالْحَقُّ وَالْحَقَّ أَقُولُ

Akasema: Ni haki! Na haki ndio niisemayo.

 لَأَمْلَأَنَّ جَهَنَّمَ مِنكَ وَمِمَّن تَبِعَكَ مِنْهُمْ أَجْمَعِينَ

Bila ya shaka nitaijaza Jahannamu kwa wewe na kwa hao wote wenye kukufuata miongoni mwao.

Katika darsa iliyopita tulisema, wakati Iblisi alipolaaniwa na kuwekwa mbali na rehma za Mwenyezi Mungu, aliapa na kutangaza kuwa, kwa muda wote atapokuwa hai atahakikisha anawapoteza wanandamu ili kulipiza kisasi kwao. Katika aya hizi tulizosoma, Allah SW anamjibu Iblisi kwa kusema: La haki ni kwamba, wale tu wataokufuata wewe na kughilibiwa na wasiwasi wako ndio watakaopotea. Wao, wataingia motoni Siku ya Kiyama. Lakini wale ambao, kwa kutumia akili zao na maumbile safi waliyojaaliwa na Mola wao, wataepuka kutekwa na wasiwasi wako; na badala ya kukufuata wewe wakawafuata Mitume wa haki na mafundisho yao, hao hawatokuwa pamoja na wewe Siku ya Kiyama, na wataepukana na adhabu ya moto. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba, Mwenyezi Mungu Mtukufu, Yeye mwenyewe ni haki, na maneno yake pia ni haki; na kimsingi, kuwa haki kwa kitu chochote kile kunatokana na Yeye. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa, Siku ya Kiyama kila kundi la watu litafufuliwa na kiongozi wake wa fikra liliyokuwa likifuata. Watu wema watafufuliwa na viongozi wema waliowafuata, na watu wabaya watakuwa pamoja na viongozi wao wabaya waliowafuata.

Darsa yetu ya leo inahitimishwa na aya ya 86 hadi 88 ambazo zinasema:

قُلْ مَا أَسْأَلُكُمْ عَلَيْهِ مِنْ أَجْرٍ وَمَا أَنَا مِنَ الْمُتَكَلِّفِينَ

Sema (Ewe Mtume): Sikuombeni ujira juu ya haya, wala mimi si katika wanaojifanya.

إِنْ هُوَ إِلَّا ذِكْرٌ لِّلْعَالَمِينَ

Hayakuwa haya ila ni mawaidha kwa walimwengu wote.

وَلَتَعْلَمُنَّ نَبَأَهُ بَعْدَ حِينٍ

Na bila ya shaka mtajua khabari zake baada ya muda. 

Aya hizi ni za sehemu ya mwisho ya Suratu-S'aad na zinatilia mkazo nukta muhimu kadhaa na za msingi kuhusu lengo la kubaathiwa na kupewa Utume Nabii Muhammad SAW na kuteremshwa Qur'ani tukufu. Kwa mujibu wa aya hizi, kinyume na wale wanaojidai kuwa Mitume, ambao wanafanya hivyo kwa sababu ya tamaa za kimaada na malengo ya kidunia, Mitume wote wa haki, akiwemo Bwana Mtume Muhammad SAW walitangaza bayana kuwa, hawatarajii chochote kwa watu; si kusifiwa na kushukuriwa kwa maneno, si kutunukiwa na kulipwa malipo yoyote ya kimaada na kimaanawi na wala si kutaka mali, cheo au kitu kingine chochote kile. Wao walikuwa wakijitambulisha kuwa ni wasita na waunganishi wa kufikisha ujumbe wa Mwenyezi Mungu kwa watu, na wala hakuna hata moja kati ya yaliyomo kwenye ujumbe huo linalotokana na wao. Ni kinyume na wanavyoitakidi baadhi ya watu wanaodai kwamba, Mitume walikuwa watu wema na wazuri tu waliokuwa wakitumia jina la Mwenyezi Mungu kuwalingania watu mambo mema, ili kwa njia hiyo wawashajiishe na kuwatia raghaba ya kufanya mambo hayo. Ukweli ni kwamba, tabia na maneno ya Mitume kwa watu wa zama zao yalikuwa ya namna ambayo, hata wapinzani wao pia hawakuweza kuwatia ila wala kuwatoa kasoro yoyote ya kitabia na matendo katika maisha yao. Kwani laiti kama wangegundua kitu kama hicho, hakuna shaka wangelikikuza na kukieneza hadharani kwa watu dhidi yao. Mitume, si tu hawakuwa wakitafuta maslahi ya kimaada, bali katika tablighi na utangazaji wao wa dini ya Allah, walifanyiwa udhia na maudhi mengi, hata baadhi yao wakalazimika kuyatoa mhanga maisha yao katika njia hiyo. Kwa hivyo aya tulizosoma zinasema: Lengo la Mitume na Vitabu vya mbinguni walivyokuja navyo, ni kuwatoa watu kwenye giza la dhulma na mghafala. Mighafala ambayo inatokana na nyoyo zao kutekwa na dunia na mambo ya kidunia na kuwafanya waghafilike na ulimwengu wa baada ya kifo na Kiyama; na au kwa kuikana na kuikadhibisha haki, kuwa sababu ya kutumbukia kwenye lindi la shirki na ukafiri. Aya ya mwisho ya Suratu-S'aad inawahutubu wapinzani kwamba: Kama hamuyaamini na hamuyapi uzito maneno ya haki, karibuni hivi utakuthibitikieni ukweli wake; lakini litakapothibiti hilo hakutakuwa na faida yoyote tena kwenu, kwa sababu hamtopata njia wala fursa ya kuyafidia na kuyarekebisha mliyoyatanguliza huko nyuma. Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba, watu wanaofanya tablighi na ufikishaji wito wa dini inapasa, kama walivyokuwa Mitume, wasiwe na matarajio ya kunufaika kimaada wala kupata chochote kwa watu; na hilo ni sharti la lazima kwa ajili ya kufanikiwa katika kufikisha ujumbe wa haki. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa, kutumia fasaha ya kupindukia katika maneno na kuwa na madoido na urasimu mwingi katika mwenendo, muamala na uchanganyikaji na watu kunaviza na kukwamisha mafanikio ya tablighi ya dini. Dini inatakiwa itangazwe kwa lugha nyepesi, wadhiha na inayoeleweka na kila mtu, na kwa namna iliyo rahisi kutekelezeka; vyenginevyo, tutawataabisha watu na kuwafanya wakirihike na kuiacha. Aya hizi aidha zinatuelimisha kwamba, ujumbe wa Bwana Mtume Muhammad SAW na Kitabu cha Qur'ani alichokuja nacho ni kwa ajili ya ulimwengu mzima na mataifa yote, wala hauhusiani na kaumu maalumu ya Waarabu au watu walioishi katika zama zake tu. Kadhalika aya hizi zinatutaka tuelewe kuwa, Qur'ani tukufu ni kitabu cha mawaidha na maonyo kwa ajili ya kuwazindua na kuwatahadharisha watu. Vile vile tunajielimisha kutokana na aya hizi kwamba, ukweli wa Qur'ani na mafundisho ya Bwana Mtume SAW utakuja kuwabainikia walimwengu katika siku za usoni japokuwa leo hii baadhi ya watu hawayakubali mafundisho hayo matukufu. Wapenzi wasikilizaji, darsa ya 836 ya Qur'ani imefikia tamati na ndiyo inayotuhitimishia pia tarjumi na maelezo ya sura yetu hii ya S'aad. Inshallah tuwe tumeelimika na kunufaika na yote tuliyojifunza katika sura hii. Tunamwomba Allah aijaalie Qur'ani ije iwe muombezi wetu Siku ya Kiyama, isije ikawa shahidi wa kushuhudia dhidi yetu. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh…/

Tags