Alkhamisi tarehe 5 Septemba 2019
Leo ni Alkhamisi tarehe 5 Muharram 1441 Hijria sawa na Septemba 5 mwaka 2019.
Siku kama hii ya leo miaka 162 iliyopita Auguste Comte mwanafalsafa na mwanahisabati wa Kifaransa alifariki dunia. Comte alizaliwa mwaka 1798. Alishirikiana kwa muda fulani huko Paris na Henri de Saint Simon, mwanafalsafa mashuhuri wa zama hizo na baadaye Comte alianza kufundisha. Auguste Comte alikuwa mwasisi wa mfumo wa elimu jamii. Comte ameandika vitabu kadhaa kikiwemo kile cha The Positive Philosophy of Auguste Comte.
Miaka 132 iliyopita mwafaka na tarehe 5 mwezi Septemba mwaka 1887, mto mkubwa wa Huang He huko China ulianza kufurika maji. Mafuriko hayo makubwa yalisababishwa na kujaa maji katika mto huo kwa zaidi ya mwezi mmoja. Zaidi ya watu laki tisa walipoteza maisha katika mafuriko hayo na taathira zake mbaya. Aidha miji kadhaa, mamia ya vijiji na mashamba mengi yaliharibiwa baada ya kukumbwa na mafuriko ya mto Huang He huko China.
Miaka 114 iliyopita katika siku kama ya leo yaani tarehe 5 Septemba mwaka 1905, mkataba wa Portsmouth ulitiwa saini na hivyo kuhitimisha vita kati ya Russia na Japan. Februari 8 mwaka 1904, vikosi vya majeshi ya Japan vilifanya mashambulio ya kushtukiza dhidi ya meli za kivita za Russia na kuyadhibiti maeneo ya Manchuria ambayo yalikuwa chini ya mamlaka ya Russia. Russia ilipata vipigo mfululizo katika vita hivyo. Hatimaye kwa upatanishi wa Marekani, katika siku kama ya leo pande mbili zilitia saini mkataba wa Portsmouth na huo ukawa mwisho wa vita kati ya Japan na Russia.
Siku kama ya leo miaka 38 iliyopita Ayatullah Ali Quddusi Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Mapinduzi ya Kislamu nchini Iran aliuawa shahidi katika mlipuko wa bomu uliotekelezwa na kundi la kigaidi la MKO. Shahidi Quddusi alipata elimu kwa wasomi kama Ayatullah Burujerdi, Allama Tabatabai na Imam Ruhullah Khomeini MA na kufikia daraja ya Ijtihad. Shahidi Quddusi alishiriki vilivyo katika masuala ya kidini na mfano wa wazi wa mchango wake ni kuasisi shule ya mafunzo ya kidini ya Haqqani. Mwaka 1341 Hijria Shamsia alisimama kupambana na utawala dhalimu wa Shah na akatiwa jela kwa kipindi fulani. Ayatullah Quddusi alisabilia miaka ya mwishoni mwa umri wake kwa juhudi za kuimarisha mfumo mchanga wakati huo wa Kiislamu hapa nchini na hatimaye aliuawa shahidi na magaidi wa kundi la MKO katika siku kama hii ya leo.
Siku kama ya leo miaka 26 iliyopita inayosadifiana na tarehe 5 Septemba 1993, moja kati ya misikiti mikubwa katika ulimwengu wa Kiislamu ulifunguliwa rasmi huko Casablanca nchini Morocco. Msikiti huo umejengwa mwa mtindo wa kisasa na una minara inayoakisi usanifu majengo wa hali ya juu wa Kiislamu. Eneo la uwanja wa msikiti huo lina uwezo wa kuchukua waumini 75,000. Eneo la ndani la msikiti huo limepambwa kiufundi. Pembeni ya msikiti huo kumejengwa maktaba moja kubwa na Chuo Kikuu cha Kidini. Msikiti huo unahesabiwa kuwa moja kati ya misikiti mikubwa na maridadi sana katika ulimwengu wa Kiislamu.