Ulimwengu wa Spoti, Sep 23
Mkusanyiko wa matukio ya spoti kitaifa na kimataifa ndani ya siku saba zilizopita...
Voliboli: Iran yatwaa ubingwa wa Asia
Timu ya taifa ya voliboli ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imetwaa ubingwa katika Mashindano ya Mabingwa wa Voliboli Asia. Timu hiyo ya Iran iliichachafya Australia seti 3-0 za (25-14, 25-17, 25-21) katika mchuano wa kusisimua wa fainali siku ya Jumamosi, uliopigwa katika ukumbi wa ndani wa Uwanja wa Azadi hapa Tehran.
Japan imetwaa medali ya shaba baada ya kuizaba Korea Kusini seti 3-1 (25-23,25-17, 23-25, 25-22) katika mchuano wa kutafuta mshindi wa tatu. Rais Hassan Rouhani ameongoza msururu wa viongozi wa na wananchi wa taifa hili katika kutuma salamu za pongezi kwa timu hiyo. Dakta Rouhani amesema katika waraka kwa timu hiyo ya voliboli ya Iran kuwa: Ushindi huu ni ukurasa mwingine wa dhahabu katika fahari ya michezo ya Iran. Wiki iliyopita Australia waliibamiza Iran seti 3-1 (25–22, 23–25, 21–25, 21–25). Kabla ya hapo, Iran ilikuwa imeiadhibu vikali Qatar kwa kuilaza (25-18, 25-15, 25-17). Aidha timu hiyo ya voliboli ya Iran iliinyoa bila maji Sri Lanka katika mechi yake ya kwanza, kwa kuitandika seti 3-0. Iran, Australia, China na India zimesonga mbele katika Michuano ya Kufuzu Olimpiki ya Asia 2020.
Debi la Tehran; Persepolis yapata ushindi hafifu dhidi ya Esteqlal
Watani wa jadi wa soka hapa nchini, klabu ya Esteqlal na Persepolis kwa mara nyingine tena zilishuka dimbani siku ya Jumapili kuvaana katika mchuano wa kusisimua wa Ligi Kuu ya Soka ya Iran. Katika debi hilo la 90 la Tehran au ukipenda Sarkhobi, au debi la wekundu na buluu., klabu ya Persepolis au ukipenda Wekundu wa Tehran walipata ushindi hafifu wa bao 1-0 na kujikusanyia alama tatu zilizoifanya ikwee hadi katika nafasi ya pili kwenye jedwali la Ligi Kuu ya Soka nchini. Persepoli imevuna ushindi huo kutokana na goli la kujifunga The Blues.
Masaibu ya Esteqlal yalianza mapema, baada ya kiiungo wa kati wa klabu hiyo, Ali Karimi kupoteza penati kunako dakika ya 28. Zimwi la mababu zake lilienda kumuandama mchezaji huyo hadi kipindi cha mwisho, ambapo alipigwa kadi nyekundu katika dakika za majeruhi. Akizungumza baada ya mchuano huo wa Ligi ya Wataalamu ya Iran, kocha wa Persepolis, Gabriel Calderon alisema, "Mwanzo ningependa kuwapongeza vijana wangu kwa mchezo mzuri. Pili nampongeza Alireza Beiranvand kwa kuokoa mkwaju wa penati katika kipindi cha kwanza, naamini huyu ni kipa bora Zaidi barani Asia.nadhani tulistahiki kushindi mechi hii muhimu katika soka la Iran."
Kwa kichapo cha Jumapili, The Blues ya Tehran haina budi kutosheka na nafasi ya 15 ikiwa na alama 2 katika mechi nne ilizocheza kufikia sasa. Klabu ya Padideh ipo kileleni mwa msimamo wa ligi kwa sasa mbele ya Persepolis yenye alama 9, huku tofauti ya magoli ikiweka mwanya baina ya timu mbili hizo. Katika debi la 89 kati ya Persepolis na Esteqlal mnamo Machi mwaka huu, Wekundu wa Tehran walipata ushindi mwingine hafifu wa bao 1-0 The Blues.
Soka; Tanzania yalazwa nyumbani na Sudan
Timu ya taifa ya soka ya Tanzania (Taifa Stars) imejiweka katika mazingira magumu ya kutinga fainali za Michuano ya Mataifa ya Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (CHAN) mwakani nchini Cameroon. Hii ni baada ya kukubali kichapo cha bao 1-0 iliposhuka dimbani katika Uwanja wa Taifa wa Dar es Salaam siku ya Jumapili kugaragazana na Sudan. Huo ulikuwa mchezo wa kwanza wa Raundi ya pili na ya mwisho ya mchujo kwa ukanda wa Afrika Mashariki na Kati. Katika mchezo huo wa aina yake, bao lililofifiza matumaini ya Tanzania lilifungwa na Yasir Mozamil kunako dakika ya 60 akimalizia mpira uliourudi baada ya kugonga mwamba kufuatia krosi ya Ranadan Agab aliyefanikiwa kumtoka beki wa kulia, Boniphace Maganga.
Sasa Tanzania wanatakiwa kwenda kushinda mabao 2-0 ugenini kwenye mchezo wa marudiano ambao Sudan wameomba ufanyike mjini Kampala, Uganda Oktoba 18 kwa sababu ya machafuko yanayoendelea nchini mwao. Mara ya mwisho Taifa Stars kufuzu fainali za CHAN ilikuwa mwaka 2009.
Kwengineko, Rising Stars ya Kenya imechukua uongozi wa Kundi B kwenye mashindano ya soka ya wachezaji wasiozidi umri wa miaka 20 baada ya kuitandika bila huruma Zanzibar mabao 5-0 katika Uwanja wa Njeru nchini Uganda, siku ya Jumapili. Vijana wa kocha Stanley Okumbi sasa wako juu ya jedwali kwa alama tatu, sawa na Tanzania bara, ambayo pia ilianza kampeni yake kwa kishindo ilipoilipua Ethiopia mabao 4-0 mapema katika uwanja huu. Katika siku ya kwanza ya mashindano haya Septemba 21, wenyeji Uganda Hippos walikabwa na Eritrea 1-1 uwanjani Pece. Nayo Burundi ilitoka sare ya 3-3 dhidi ya Sudan Kusini katika mechi ya Kundi C. Ratiba ya leo: Burundi na Sudan Kusini zitavaana saa nane mchana, Eritrea na Sudan nazo pia zitapambana saa nane mchana na Djibouti na Uganda wakikutana saa kumi jioni.
Ligi ya Premia
Na tunafunga kipindi kwa kutupia jicho baadhi ya matokeo muhimu ya Ligi Kuu ya Soka ya Uingereza. Siku ya Jumapili klabu ya Manchester United ilishindwa kufurukuta na kuishia kuchabangwa mabao 2-0 na West Ham. Magoli ya Andriy Yarmolenko (44) Aaron Cresswell (84) yalitosha kulizamisha jahazi la Mashetani Wekundu ugenini katika Uwanja wa London. Kichapo hicho kimevunja msururu wa ushindi wa vijana hao wa Ole Gunnar Solskjaer.
Wakati Red Divils wakishuhudia kichapo hicho, klabu ya Arsenal nayo ilikuwa ikikabiliwa na kibarua cha ziada, katika mchuano wake na Aston Villa. Ingawaje Gunners ikiwa wachezaji 10 waliibuka washindi katika mechi hiyo, lakini haikuwa mteremko. Wageni Aston Villa walitangulia kuona lango la wenyeji Arsenal katika Uwanja wa Emirates, kupitia goli la John McGinn dakika 20 baada ya kuanza mchezo. Nicolas Pepe ilijibu mapigo kupitia mkwaju wa penati katika dakika ya 59, kabla ya Wesley kuwarejesha wageni kifua mbele tena. Hata hivyo magoli ya dakika za lala za salama ya Calum Chambers and Pierre-Emerick Aubameyang yaliihakikishia Wabeba Bundi alama tatu muhimu.
Mchuano mwingine uliovutia katika Ligi ya EPL ni ule kati ya klabu ya Manchester City na Watford, ambapo City ilivuna ushindi wa kishindo baada ya kuinyeshea mvua ya mabao klabu ya Watford. Man City ambao ni mabingwa watetezi licha ya Watford kuwa na historia ya kuwasumbua vigogo lakini walikutana na kipigo cha msimu. City akiupigia nyumbani aliifunga Watford magoli 8-0, magoli ambayo ni mara chache yanafungwa katika EPL kwenye mechi moja. hali ilikuwa mbaya zaidi kwa Watford kwani ndani ya dakika 18 za kwanza tayari walikuwa wameshalishwa magoli 5-0. Magoli ya Man City yalifungwa na David Silva dakika ya 1, Sergio Aguero dakika ya 7 kwa penati, Riyad Mahrez dakika ya 12, Bernaldo Silva aliyefungwa harttrick dakika ya 15, 48 na 60, Nicolaos Otamendi dakika ya 18 na goli la mwisho la Man City likafungwa na Kelvin De Bruyne dakika ya 85 ya mchezo.
Kwengineko, Liverpool iliibamiza Chelsea mabao 2-1, wakati ambapo Crustal Palace walikuwa wanalazimishwa sare ya 1-1 na Wanderers. Kwa ushindi huo Liverpool inasalia kileleni mwa jedwali la ligi wakiwa na alama 18, wakifuatiwa na City 13 huku Leicester ikifunga orodha ya tatu bora kwa pointi 11. Gunners pia wana alama 11 wakiwa katika nafasi ya nne, alama sawa na West Ham katika nafasi ya tano.
……………………..TAMATI………………