Jumatano tarehe 16 Oktoba 2019
Leo ni Jumatano tarehe 17 Safar 1441 Hijria inayosadifiana na tarehe 16 Oktoba 2019.
Siku kama ya leo miaka 545 iliyopita, alizaliwa Muhammad Mustafa Imad, maarufu kwa jina la Abus-Su’ud, faqihi na mfasiri wa Kiislamu katika kijiji cha Mudares, karibu na mji wa Istanbul, Uturuki. Baada ya kukamilisha masomo yake Abus-Suud alianza kufundisha sambamba na kujishughulisha na kazi ya ukadhhi mjini Istanbul. Aliendelea na kazi hiyo hadi mwishoni mwa uhai wake. Msomi huyo alifanya jitihada kubwa za kuhakikisha kwamba sheria za utawala wa Kiothmani (Ottoman Empire) zinaoana na sheria za Kiislamu. Mbali na kujua lugha ya Kituruki, msomi huyo pia alikuwa hodari katika lugha za Kifarsi na Kiarabu na aliandika mashairi kwa kutumia lugha hizo. Miongoni mwa vitabu vya Abus-Suud ni pamoja na 'Tafsiru Abis-Suud' 'Dua Nameh' 'Qanun Nameh' na 'Mafrudhaat.'
Siku kama ya leo miaka 226 iliyopita, yaani tarehe 16 Oktoba mwaka 1793, alinyongwa kwa kukatwa kichwa na shoka, malikia wa Ufaransa Marie Antoinette kwa amri ya Baraza la Katiba la nchi hiyo na pia amri ya Maximilien Robespierre. Louis wa 16 aliyekuwa mume wa Antoinette miezi 10 kabla ya hapo alikumbwa tayari amepatwa na hatma hiyo hiyo iliyomkuta mke wake. Marie Antoinette alikuwa binti wa Maria Theresa Walburga, mtawala wa Austria na Ufaransa. Antoinette aliolewa na Louis, mrithi wa kiti cha ufalme wa Ufaransa, mnamo mwaka 1770 akiwa na umri wa miaka 14. Hatua ya Louis ya kumuoa mwanamke huyo ilikuwa ni na nia ya kuzikurubisha pamoja nchi za Austria na Ufaransa ambazo wakati huo zilikuwa zikishindana barani Ulaya. Hata hivyo Wafaransa wengi hawakuridhia ndoa hiyo kiasi cha kuwafanya kuendelea kumwita ‘Muaustria’ hata kipindi alipokuwa tayari ni malikia wa Ufaransa.
Siku kama ya leo miaka 186 iliyopita, alizaliwa Sheikh Abdul Rahim Sultanul-Qurrai Tabrizi, qaari mkubwa wa Qur’ani Tukufu na mmoja wa walimu mashuhuri wa taaluma ya qiraa, huko mjini Tabriz, kaskazini magharibi mwa Iran. Baada ya kujifunza taaluma hiyo kutoka kwa baba yake, Sultanul-Qurrai Tabrizi alifahamiana na Sheikh Shamil Daghestani na kushirikiana naye. Wakati Sheikh Shamil Daghestani alipoandaa jeshi kwa ajili ya kupambana na Warusi, Sultanul-Qurrai alifanya safari kuelekea Daghestani ili kushiriki katika harakati hiyo. Baadaye alirejea Tabriz na kuanzisha chuo cha kisomo cha Qur’ani na ni wakati huo ndipo alipopewa lakabu ya Sultanul-Qurrai. Miongoni mwa athari zake ni pamoja na ‘Risala katika Elimu ya Tajwidi’ Sultanul-Qurrai alifariki dunia mwaka 1336 Hijiria mjini Tabriz.
Siku kama ya leo miaka 165 iliyopita alizaliwa Oscar Wilde mwandishi mashuhuri Dublin huko Ireland. Oscar Wilde alipata elimu ya msingi katika mji wa Skyline kaskazini mwa Ireland na akajiunga na chuo kikuu cha Trinity na baadaye Oxford. Oscar Wilde alipata umaarufu baada ya kuandika mfululizo wa vitabu vya kisa cha Mwanamfalme Mwenye Furaha (The Happy Prince).
Siku kama ya leo miaka 74 iliyopita liliasisiwa Shirika la Chakula Duniani (FAO). Hati ya kuasisiwa shirika hilo ilipasishwa Oktoba 16 mwaka 1945 katika mji wa Québec nchini Canada. Lengo ya kuasisiwa shirika la FAO ni kuzisaidia nchi wanachama kukusanya taarifa, ripoti na takwimu zinazohusiana na chakula, kilimo, utunzaji wa misitu na uvuvi na kufanya tathmini kuhusu uzalishaji wa chakula, ugavi wake na juhudi za kuboresha uzalishaji, masoko ya chakula, kulinda maliasili, kupanga sera zinazohusiana na kilimo na chakula na kadhalika. Siku hii pia inatambuliwa kuwa ni Siku ya Kimataifa ya Chakula.
Miaka 73 iliyopita katika siku kama ya leo, mwafaka na tarehe 16 Oktoba 1946, kwa mujibu wa hukumu iliyotolewa na Mahakama ya Nuremberg walinyongwa viongozi 10 wa Ujerumani ya utawala wa Kinazi baada ya kupatikana na hatia za kutenda jinai za kivita. Herman Goering aliyekuwa Kamanda Mkuu wa kikosi cha Jeshi la Anga la Ujerumani na msaidizi wa dikteta Adolphe Hitler ambaye alikuwa amehukumiwa adhabu ya kifo, pia aliamua kujinyonga yakiwa yamebakia masaa machache kabla ya kutekelezwa hukumu hiyo ya kifo. Hali kadhalika mahakama hiyo iliwahukumu adhabu ya kifungo cha muda mrefu viongozi wengine 9 wa Ujerumani ya Wanazi na wengine watatu hawakupatikana na hatia. Mahakama ya Nuremberg iliyoundwa na wawakilishi wa Marekani, Urusi ya zamani, Uingereza na Ufaransa kwa shabaha ya kuwahukumu maafisa 22 wa Manazi wa Ujerumani kwa tuhuma za kufanya jinai za kivita ilikamilisha shughuli zake tarehe 30 Septemba mwaka 1946.
Na siku kama ya leo tarehe 25 Mehr miaka 41 iliyopita, kulitokea maafa makubwa kwenye Msikiti Mkuu wa Kerman, huko magharibi mwa Iran baada ya vikosi vya polisi na askari usalama wa utawala wa mfalme Muhammad Reza Pahlavi kuwashambulia kwa risasi wananchi waliokusanyika kwenye eneo hilo la msikitini kwa shabaha ya kuadhimisha 40 ya mashahidi waliouawa tarehe 17 Shahrivar mjini Tehran. Shambulio hilo la askari usalama wa Shah liliamsha hasira na wimbi jipya la harakati za wananchi za kupinga utawala kibaraka wa Mfalme Muhammad Reza Pahlavi.