Dec 23, 2019 07:21 UTC
  • Ulimwengu wa Michezo, Dec 23

Ufuatao ni mkusanyiko wa baadhi ya matukio muhimu ya michezo yaliyojiri ndani ya siku saba zilizopita kitaifa na kimataifa....

Iran Bingwa wa Ndondi

Timu ya taifa ya ndondi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa mara ya kwanza imetwaa ubingwa wa Mashindano ya Masumbwi ya Asia. Timu hiyo ya ngumi ya Iran imetwaa taji la masumbwi mtindo wa Muay Thai kwa kuzoa medali 15 za dhahabu, 10 za fedha na 8 za shaba, katika mashindano hayo ya kikanda yaliyofanyika mjini Abu Dhabi katika Umoja wa Falme za Kiarabu kuanzia Disemba 17 hadi 21. Kila alipotunukiwa mwamasumbwi Muiran medali ya dhahabu, wimbo wa taifa wa Iran ulihinikiza ukumbini. Mashindano hayo ya masumbwi mtindo wa Muay Thai ambayo asili yake ni nchini Thailand yamesimamiwa na Shirikisho la Vyama vya Muay Thai Duniani (IFMA).

Mwanamasumbwi Muirani akikabiliana na hasimu

Kazakhstan imeibuka ya pili kwa kuzoa medali 14 za dhahabu, tatu za fedha na shaba 5, huku Thailand ikifunga orodha ya tatu bora kwa kujikusanyia medali 9 za dhahabu na shaba 4. Wanamasumbwi 600 kutoka nchi 35 duniani wameshiriki mashindano hayo yanayofahamika kama Asian Muay Thai Championships.

 Rais wa IOC amshukuru Rais Rouhani

Rais wa Kamati ya Kimataifa ya Olimpiki (IOC), ameipongeza serikali ya Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa kuunga mkono Michezo ya Olimpiki. Thomas Bach amempa kongole hizo Dakta Rouhani katika barua aliyomuandikia, ambapo pia amewatakia kila la kheri wanamichezo wa Iran watakaoshiriki michezo ya olimpiki ijayo. Katika barua hiyo, Rais wa IOC amemhutubu Dakta Rouhani kwa kumuambia, "Tafadhali pokea shukrani zangu za dhati, kutokana na serikali yako kuunga mkono kikamilifu Michezo ya Olimpiki, kwa kudhamini Azimio la Olimpiki la Umoja wa Mataifa.

Rais Hassan Rouhani wa Iran

Azimio hilo lenye anuani inayosema "Kuunda Dunia Bora na Yenye Amani Kupitia Michezo na Olimpiki" lilipasishwa kwa kishindo katika Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa na hivyo kuweka msingi wa Michezo ya Olimpiki ya 2020 jijini Tokyo nchini Japan.

Waziri wa Michezo wa IRAN akosoa vikwazo batili vya Marekani

Katika hatua nyingine, Masoud Soltanifar, Waziri wa Michezo na Vijana wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amelaani vikali vikwazo vya kidhalimu ya Marekani dhidi ya taifa hili na kubainisha kuwa, vikwazo hivyo vimelifanya Shirikisho la Soka Duniani FIFA lishindwe kuipa Iran ushuru wake. Soltanifar alisema hayo Jumapili katika mazungumzo yake na Spika wa Bunge la Iran, Ali Larijani katika ufunguzi wa Maonyesho ya Spoti hapa jijini Tehran na kufafanua kuwa, "Kwa bahati mbaya kutokana na vikwazo hivyo visivyo vya kiuadilifu, FIFA haiwezi kuipa Iran mapato yake bila idhini ya Wizara ya Fedha ya Marekani.

Masoud Soltanifar, Waziri wa Michezo na Vijana wa Iran

Kutokana na hili, Shirikisho la Soka ya Iran lililazimika kuiomba mkopo kampuni ya hapa nchini, ili iweze kumlipa kocha wa zamani wa timu ya taifa ya soka hapa nchini, Marc Wilmots. Amesema Wilmots pamoja na Andrea Stramaccioni ni miongoni mwa makocha wa kigeni ambao Iran imeshindwa kuwalipa kutokana na vikwazo hivyo ya Marekani, ambavyo vimelenga moja kwa moja soka ya Iran na tabaka la vijana.

Soka: Uganda yatwaa taji la CECAFA (Chalenji)

Timu ya taifa ya soka ya Uganda 'The Cranes' ndio mabingwa wapya wa Kombe la Mataifa ya Afrika Mashariki na Kati (CECAFA Senior Challenge Cup) mwaka huu 2019. Hii ni baada ya kuichabanga Eritrea mabao 3-0, kwenye mchuano wa fainali uliopigwa Disemba 19 jijini Kampala.  Magoli ya Uganda yalifungwa na Bright Anukani dakika ya 32, Mustafa Kizza dakika ya 68 na Joel Madondo dakika ya 88.

Wakati huohuo, timu ya taifa ya soka ya Tanzania Bara 'Kilimanjaro Stars' wamemaliza nafasi ya nne baada ya kupoteza kwa magoli 2-1 katika mchezo wa kutafuta mshindi wa tatu dhidi ya Harambee Stars ya Kenya. Kocha wa Tanzania bara Juma Mgunda baada ya kurejea Tanzania akitokea Uganda katika michuano ya CECAFA, ameeleza sababu za kikosi chake kufanya vibaya katika michuano hiyo kinyume na matarajio ya Watanzania. Timu ya taifa ya soka ya wanaume ya Eritrea iliwashangaza wengi baada ya kuitandika Harambee Stars, katika mchuano wa nusu fainali. Itakumbukwa kuwa, bingwa mtetezi wa kombe hilo la Chaleji ni Kenya ambayo ilitwaa ushindi mwaka 2017 kwa kuifunga Zanzibar Heroes katika fainali iliyoisha kwa sare ya mabao 2 – 2, kabla ya kuibuka kidedea kwa penati 3 – 2. 

CECAFA yapata rais mpya

Wakati huohuo, Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Wallace Karia amechaguliwa kuwa Rais mpya wa Baraza la Vyama na Mashirikisho ya Soka Afrika Mashariki na Kati CECAFA kwa kipindi cha miaka minne ijayo. Karia amechaguliwa katika nafasi hiyo kwenye Mkutano Mkuu wa CECAFA uliofanyika nchini Uganda, ambapo atakuwa akisaidiana na Makamu wa Rais wawili ambao ni Francis Amin kutoka Sudan Kusini na Esayas Jiro wa Ethiopia. Pia katika mkutano huo imeshuhudiwa aliyekuwa Katibu Mkuu wa CECAFA, Nicholas Musonye wa Kenya akiachia ngazi katika nafasi yake hiyo baada ya kuhudumu kwa miaka 20. Karia ameeleza kuwa ataboresha mashindano mbalimbali yanayoandaliwa na CECAFA.

Dondoo za Hapa na Pale

Klabu ya Mpira wa Kikapu ya Patriots ya Rwanda imefuzu Ligi ya Basketball Africa (BAL) msimu wa 2020 baada ya kushinda michezo yao yote tisa ya kufuzu. Mabingwa hao wa Rwanda walikamilisha kampeni yao kwa ushindi wa vikapu 94-63 dhidi ya GNBC ya Madagascar katika mchezo wa fainali wa raundi ya pili wa kufuzu huko Kigali Arena Jumapili.

Kwengineko klabu ya soka ya Uingereza ya Liverpool ni moto wa kuotea mbali katika kandanda. Hivyo ndivyo unavyowza kusema kwa kifupi, baada ya klabu hiyo kutwaa taji la Klabu Bingwa Duniani. Katika mchezo wa fainali wa michuano hiyo uliopigwa usiku wa December 21 nchini Qatar, Wekundu hao ambao kwa asasa wapo kileleni lwa jedwali la Ligi Kuu ya Soka ya Uingereza waliizaba Flamengo ya Brazil bao moja la uchungu bila jibu. Mchezo huo uliolazimika kuchezwa kwa dakika 120 baada ya 90 kumalizika kwa 0-0, uliamuliwa na mchezaji wa Kibrazil Robert Firmino aliyowafunga Flamengo dakika ya 99 na kuipa Ubingwa wa Dunia Liverpool kwa ushindi wa 1-0.

Mbali na hayo, klabu ya Lazio imetwaa ubingwa wa Italian Super Cup baada ya kuiachachafya mabao 3-1 klabu ya Juventus, ambao ni mabingwa watetezi wa Ligi Kuu ya Italia ya Serie A. Katika kitumutimu hicho kilichopigwa mjini Riyadh, Lazio walionyesha azma ya kutwaa kombe hilo baada ya kipenga cha kuanza ngoma kupulizwa. Bao la dakika ya 16 ya mchezo lililotiwa kimyani na Luis Alberto liliiweka kifua mbele timu hiyo. Dakika chache kabla ya kwenda mapumzikoni, straika wa Argentina, Paulo Dybala alifanya mambo kuwa sawa bin sawa. Hata hivyo Lazio walirejea uwanjani kwa kasi isiyo ya kawaida katika kipindi cha pili na kufanikiwa kupata mabao mawili yaliyofungwa na Senad Lulic (73) na Danilo Cataldi katika dakika za lala salama.

Na kwa kutamatisha, klabu ya ligi kuu ya Uingereza, Arsenal imemtangaza Mikel Arteta kuwa kocha mpya wa timu hiyo ya EPL. Gunners ambao mnamo Novemba 29 walimtimua aliyekuwa mkufunzi wao Unai Emery, wamekuwa wakinolewa na Fredrik Ljungberg kama mwalimu wa muda. Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Arsenal mwalimu huyo wa soka mwenye umri wa miaka 37 raia wa Uhispania ambaye pia alikuwa mchezaji wa timu hiyo kati ya 2011 hadi 2016, amesaini mkataba wa kukinoa kikosi hicho kwa muda wa miaka mitatu na nusu. Wakati huohuo, klabu ya Everton imempa kibarua cha kuikarabati timu hiyo ya EPL, Carlo Ancelloti. Ancelloti Jumapili hii amerithi rasmi mikoba ya Marco Silva ambaye alipigwa kalamu nyekundu mwezi huu kwa kuiendesha ndivyo sivyo klabu hiyo. Kocha huyo amesaini mkataba wa miaka minne na nusu na klabu hiyo ya Ligi Kuu ya Soka ya Uingereza.

……………………..TAMATI…………….….

 

Tags