Mar 13, 2020 02:49 UTC
  • Ijumaa tarehe 13 Machi 2020

Leo ni Ijumaa tarehe 18 mwezi wa Rajab 1441 Hijria inayosadifiana na tarehe 13 Machi mwaka 2020.

Siku kama ya leo miaka 1431 iliyopita alifariki dunia mtoto mdogo wa Mtume wetu Muhammad (saw), Ibrahim akiwa na umri wa miezi 18 tu. Ibrahim ambaye alifariki dunia kutokana na maradhi alikuwa mtoto wa kiume pekee wa Mtume ambaye hakuzaliwa na Bibi Khadija (as). Mama yake alikuwa Maria al Qibtiyya ambaye alitumwa na mfalme wa Misri ya wakati huo kuwa hadimu na mtumishi wa Mtume na aliolewa na mtukufu huyo baada ya kusilimu. Kifo cha Ibrahim kilimhuzunisha sana Mtume (saw) kwa sababu mtukufu huyo alikuwa akimpenda sana mtoto huyo. 

Kaburi la Ibrahim, mtoto wa Mtume wetu Muhammad (saw), Baqii- Madina

Tarehe 18 Rajab miaka 1014 iliyopita alifariki dunia Ibn Samh huko katika mji wa mjini Andalucia. Msomi huyo wa Kiislamu alikuwa mtaalamu wa hesabu, nyota na tabibu. Alizaliwa katika mji wa Cordoba, Andalucia mnamo mwaka 370 Hijiria. Msomi huyu wa Kiislamu alifanya utalii na utafiti mwingi katika elimu za hesabu na nyota, sambamba na kuwalea wanafunzi wa zama zake. Kuna vitabu kadhaa vilivyoandikwa na Ibn Samh kwa lugha ya Kiarabu na miongoni mwavyo ni pamoja na kitabu kiitwacho "Al Madkhalu Ila al Handasah", "Al Muamalat" na "Kitabuz Zayj."

Siku kama ya leo miaka 287 iliyopita, yaani 13 Machi, 1733 alizaliwa Joseph Priestley, mkemia na mwanafizikia wa Uingereza. Msomi huyo aliishi katika kipindi kilichokuwa maarufu kama zama za dhahabu za kemia na elimu hiyo ilikuwa imepiga hatua. Katika uchunguzi na utafiti wake, Priestley alivumbua uvutaji pumzi katika mimea na gesi za oksijeni na haidrojeni. Joseph Priestley alifariki dunia mwaka 1804.

Joseph Priestley

Siku kama ya leo miaka 72 iliyopita sawa na tarahe 13 Machi 1948, Wazayuni waliokuwa na mfungamano na kundi la kigaidi la Haganah walishambulia kitongoji cha Wapalestina cha Husseiniyah katika eneo la kaskazini mwa Jalilah. Wazayuni hao licha ya kuwaua shahidi zaidi ya Wapalestina 60, waliharibu nyumba zao kadhaa. Hali kadhalika katika siku hiyo hiyo, wanajeshi wa Israel walizilipua kwa mabomu nyumba za Wapalestina katika eneo la 'Qatmuun' lililoko Baitul Muqaddas. Mauaji ya Waislamu wa Palestina yaliyofanywa na makundi ya kigaidi ya Israel yalitekelezwa kwa lengo la kutaka kutangaza uwepo wa utawala huo bandia kwenye ardhi zinazokaliwa kwa mabavu za Palestina baada ya kuondoka vikosi vya majeshi ya Uingereza katika eneo hilo.

Siku kama ya leo miaka 58 iliyopita sawa na tarehe 23 Esfand 1340 Hijria Shamsia, alifariki dunia Ayatullah Sayyid Abul Qassim Kashani, mwanachuoni na shakhsia maarufu wa kisiasa katika historia ya Iran. Ayatullah Kashani alifanikiwa kupata daraja la ijtihadi akiwa bado barobaro huko Najaf nchini Iraq lakini baadaye alifukuzwa nchini humo kutokana na misimamo yake ya kupinga ukoloni wa Uingereza. Aliporejea nchini Iran, Ayatullah Kashani aliendelea na misimamo yake ya kupambana na ukoloni wa Uingereza na kufungwa jela mara kadhaa. Baada ya kutoka jela wananchi wa Tehran walimchagua kuwa mwakilishi katika bunge la Taifa.

Ayatullah Sayyid Abul Qassim Kashani