Mchango wa Maulamaa wa Kishia Katika Uislamu (9)
Assalaam Aalaykum wapenzi wasikilizaji popote pale mlipo na karibuni katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Mchango wa Maulamaa wa Kishia Katika Uislamu ambacho huwatambulisha na kuwazungumzia Maulamaa wakubwa wa Kishia, mchango wao katika Uislamu pamoja na vitabu na athari zao.
Kipindi chetu kilichopita kiliendelea kumtambulisha Muhammad bin Muhammad bin Nu’man mashuhuri kwa jina la Sheikh Mufid, mmoja wa Maulamaa na wanazuoni mashuhuri mno katika ulimwengu wa Kishia. Tulieleza jinsi Sheikh Mufid alivyoandaa mpango na mkakati jumla kwa ajili ya Ijtihadi na kunyambua sheria na hukumu za dini kutoka katika vyanzo vyake vikuu.
Kadhalika tulibainisha kwamba, Sheikh Mufid akiwa na lengo la kujibu shubha na mambo tata, mbali na kuandika makala na vitabu, alikuwa akiandaa vikao vya midahalo na mijadala na kufanya majadiliano na maulamaa wa mapote na makundi ya itikadi mbalimbali. Sehemu ya 9 ya mfululizo huu juma pia itaendelea kumzungumzia mwanazuoni huyu. Tafadhalini kuweni nami hadi mwisho wa kipindi.

Utendaji wa Sheikh Mufid katika elimu ya fikihi na teolojia unahesabiwa kuwa ni utendaji wa muelekeo wa kutumia akili. Mwanazuoni huyu alifanya juhudi kubwa katika kufundisha masomo ya dini katika uga wa fikihi, Usul, teolojia, historia na tafsiri na kuzibainisha elimu hizo kwa mtazamo wa akili na kuyatetea hayo kupitia akili.
Katika kipindi chetu kilichopita tuliashiria zama za ghaiba na kipindi cha kabla ya Sheikh Mufid ambapo fikra za watu wa hadithi zilikuwa zimetawala anga ya elimu za Kiislamu. Waliokuwa wakiitwa Ahlul Hadith au watu wa hadithi ni watu ambao hawakuwa wakiamini suala la kutumia akili katika masuala ya teolojia na fikihi na walifanya hima na juhudi zao zote kwa ajili ya kunukuu hadithi na kuishia katika kuzigawa katika mafungu tu kulingana na maudhui zake. Kwa mintarafu hiyo kuliibuka makundi katika zama hizo ambayo yalichupa mipaka katika uwanja huo, ambayo yalikuwa yakijiepusha kwa nguvu zao zote, nafasi na mchango wa aina yoyote ile wa akili katika kufahamu hadithi na maarifa ya Kiislamu. Harakati hii iliyokuwa dhidi ya akili ilipelekea kuibuka upotofu na hali ya ufahamu wa kijuujuu wa dini.
Sheikh Mufid akiwa alimu, mwanazuoni mkubwa na mujtahidi aliyekuwa na mtazamo mpana na wa kisomi, aliendesha harakati zisizo choka za kukabiliana na fikra za upotoshaji mambo. Alitilia mkazo juu ya nafasi na kutumiwa akili katika kujenga hoja katika fikihi na teolojia.
Sheikh Mufid alikuwa akiamini kuwa, hadithi zilizonukuliwa ni lazima zitiwe katika mizani ya akili. Hii ni kutokana na kuwa, kwanza walionukuu hadithi wakati mwingine walikuwa wakikumbwa na mghafala au kukosea hususan kundi ambalo lilikuwa likijulikana kwa jina la Ahlul Hadith “Watu wa Hadithi” wao walikubali hadithi yoyote ya Maasumina (as) bila ya kuzingatia usahihi na uongo wake na kuifanya kuwa msingi wa amali na matendo yao.
Kwa hakika Sheikh Mufid alikuwa akiamini kwamba, madhali hadithi fulani ya Maasumu (as) haijathibiti ukweli wake kupitia mbinu za kiakili, basi haipasi kuichukua na kuifanyia kazi hadithi husika. Kadhalika baada ya kufahamika usahihi na uongo wa hadithi, itibari ya hadithi hiyo inapimwa kwa kigezo cha akili na katika hatua inayofuata ni lazima kupata msaada wa akili katika kufahamu usahihi wa hadithi yenyewe. Kwa hakika Sheikh Mufid alikuwa akithamini mno suala la kufahamu kwa njia sahihi riwaya na hadithi na alikuwa akiamini kwamba, kuna haja ya kuweko aina ya mtazamo wa kiuhakiki sambamba na tafakuri na akili ili njia ya ufahamu usio sahihi wa hadithi ifungwe na kubatilishwa. Kwa msingi huo, mwanazuoni huyu alikuwa akitetea kwa nguvu zake zote nafasi na mchango chanya wa akili katika ‘kunakili’ na ‘kufahamu’ hadithi.
Sehemu muhimu ya maisha ya mwanazuoni huyu wa fikihi mwenye uwezo mkubwa inahusiana na masuala ya elimu ya fikihi. Fikihi ni elimu ambayo inatoa na kuleta hukumu na sheria za kivitendo za Uislamu kutoka katika vyanzo vya kidini na kwa kutumia hoja madhubuti. Baadhi ya wasomi wanamtambua Sheikh Mufid kama mwanafakihi wa kwanza aliyezungumzia nafasi na mchango wa akili katika elimu ya fikihi.
Tukirejea vitabu vya hadithi tunaona ni kwa namna gani Ahlul Baiti (as) walivyokuwa wakiwashajiisha daima Mashia wao kutumia akili na walikuwa wakiwafundisha mbinu za kunyambua hukumu na sheria kutoka katika Qur’ani na hadithi za Bwana MtumeMuhammad (saw) kulingana na zama na mazingira ya wafuasi wao hao.
Lakini kama tulivyotangulia kusema, baada ya Imam Mahdi (atfs), Imam wa kumi na mbili na Imam wa zama hizi kughibu na kwenda ghaiba na mpaka mwishoni mwa karne ya nne Hijria, kutokana na fikra za watu wa hadithi kutawala katika jamii, hakukuweko na suala la uchambuzi na tathmini ya kiakili na suala la uchambuaji wa hukumu kiijtihadi.
Kabla ya Sheikh Mufid, kuna baadhi ya maulamaa na wanazuoni akiwemo Ibn Abi Aqil na Ibn Junaid Askafi walikuwa na hali ya muelekeo wa utumiaji akili katika Ijtihadi, lakini Sheikh Mufid katika zama zake alikuja na suala linalojulikana kama “muelekeo wa utumiaji akili” kwa upana wa hali ya juu na kubainisha kwamba, akili inapaswa kurejewa na kutambulika kama moja ya vyanzo vya kutumia kwa ajili ya kunyambua na kutoa hukumu na sheria katika vyanzo vyake yaani Qurani na hadithi.
Sheikh Mufid ameandika katika moja ya vitabu vyake kwamba: Ikiwa katika zama za ghaiba ya Imam Mahdi (atfs) kutaibuka mivutano kuhusiana na jambo fulani baina ya Mashia ambapo katika Qur’ani na hadithi hakuna agizo na amri ya wazi na bayana, nini cha kufanya?
Sheikh Mufid anajibu swali hili kwa kuandika: Mtu ambaye amekabiliwa na jambo fulani ambalo hafahamu hukumu yake na akataka kulifahamu hilo, anapaswa kuwarejea Maulamaa wa Kishia na kama hakupata jibu, katika mazingira kama haya inafahamika kwamba, akili inapaswa kuwa hakimu kuhusiana na suala hilo.
Historia inaonyesha kuwa, Sheikh Mufid alifanikiwa kuandika makala na vitabu mbalimbali vya midahalo visivyo na mithili. Ndio maana maulama wengi watajika katika ulimwengu wa Kishia akiwemo Allamah Hilli, msomi na alimu mkubwa wa fikihi, anamtaja Sheikh Mufid kama Ustadh na mwalimu wa wanazuoni wote wa fikihi na teolojia.
Kwa leo mpenzi msikilizaji sina budi kukomea hapa, hata hivyo usikose kuwa nami wiki ijayo katika sehemu nyingine ya mfululizo huu ambapo tutazungumzia zaidi taathira ya Sheikh Mufid katika harakati ya Kishia.
Basi hadi tutakapokutana tena wiki ijayo ninakuageni nikikutakieni kila la kheri.
Wassalaamu Alaykum Warahamtullahi Wabarakaatuh….