May 24, 2020 02:54 UTC
  • Jumapili 24, Mei, 2020

Leo ni Jumapili tarehe Mosi Shawwal 1441 Hijria, inayosadifiana na Juni 24 Mei, 2020 Miladia.

Leo tarehe Mosi Shawwal 1441 Hijiria, inasadifiana na sikukuu ya Idul-Fitr. Idul Fitri ni moja ya sikukuu kubwa katika dini tukufu ya Kiislamu. Baada ya kukamilisha ibada ya funga, kuomba na kujipinda kwa ibada katika mwezi mtukufu wa Ramadhani, Waislamu hufanya sherehe katika siku hii kubwa wakimshukuru Mola Manani kwa kuwawezesha kukamilisha ibada hiyo. Iddi al Fitr ni kuuaga mwezi mtukufu wa Ramadhani ambao ni mwezi wa ibada na kutakasa nafsi. Katika hii ni haramu kufunga saumu yoyote na Waislamu baada ya juhudi za mwezi mzima za kupambana na nafsi na kuchuma matunda ya ucha-Mungu hukusanyika pamoja na kuswali Swala ya Idul Fitr. Kwa mnasaba wa siku hii adhimu, Redio Tehran inatoa mkono wa pongezi, heri na fanaka kwa Waislamu wote duniani.

Siku kama ya leo miaka 1188 iliyopita yaani tarehe Mosi Shawwal mwaka 253, Hijria alifariki dunia mpokezi mashuhuri wa Hadithi wa Ahlusunna, Imam Muhammad Ismail Bukhari. Abu Abdullah Muhammad Ismail aliyekuwa mashuhuri kwa jina la Imam Bukhari ni miongoni mwa wanazuoni wakubwa wa Hadithi wanaoaminiwa na Ahlusunna. Alisafiri sana kwa ajili ya kutafuta Hadithi za Mtume (saw). Kitabu mashuhuri zaidi cha mwanazuoni huyo ni kile cha ‘Jamius Swahih’ maarufu kama Sahihi Bukhari. Vitabu vingine mashuhuri vya mwanazuoni huyo ni ‘Al-Adabul Mufrad’, ‘Al-Jaamiul-Kabiir’ na ‘Tarikhul-Kabir an Taraajam Rijaal-Sanad.’

Muhammad bin Ismail Bukhari

Siku kama ya leo miaka 872 iliyopita, sawa na tarehe Mosi Shawwal mwaka 569 Hijiria alifariki dunia Said Bin Mubarak maarufu kwa jina la Ibn Dahhan, mfasiri, mwanafasihi na malenga wa Kiislamu. Ibn Dahhan alizaliwa mjini Baghdad na baada ya kumaliza masomo yake ya awali, alianza kusoma lugha sambamba na kupokea hadithi kutoka kwa wanazuoni wakubwa wa zama zake. Mtaalamu huyo mkubwa wa lugha alitilia maanani taaluma ya fasihi hususan katika kusoma mashairi na hivyo kuwa mfano wa kuigwa na wanafunzi wake katika usomaji mashairi. Aidha alilipa umuhimu mkubwa suala la kuhuisha baadhi ya vitabu vilivyosahaulika kiasi kwamba mwishoni alipoteza uwezo wake wa kuona katika kazi hiyo.

Ibn Dahhan

Siku kama ya leo miaka 835 iliyopita, yaani sawa na tarehe Mosi Shawwal, alifariki dunia Abu Abdallah Muhammad bin Omar Razi mashuhuri kwa jina la ‘Fakhrurazi’ msomi na mwanazuoni mashuhuri wa Kiislamu. Fakhrurazi alizaliwa mwaka 543 Hijiria mjini Rey karibu na mji wa Tehran na kutokana na maandalizi yake makubwa aliweza kukwea daraja za elimu mbalimbali kama vile fiqhi, tafsiri ya Qur’an, theolojia, falsafa na mantiki. Aidha msomi huyo mkubwa alitabahari katika taaluma ya midahalo na kutoa mawaidha ambapo alipata kutoa mawaidha na kufanya midahalo na wasomi wa miji tofauti. Mbali na hayo ni kwamba darsa zake zilijaa wasomi na wanafunzi hususan katika mji wa Herat. Fakhrurazi ameandika vitabu vingi ikiwa ni pamoja na ‘Tafsirul-Kabiir’, ‘Asraarut-Tanziil’ ‘Nihaayatul-Uquul’ na ‘Sirajul-Quluub’.

Abu Abdallah Muhammad bin Omar Razi

Siku kama ya leo miaka 477 iliyopita sawa na tarehe 24 Mei 1543 Miladia, alifariki dunia mnajimu na mwanahesabati mashuhuri wa Poland, Nicolaus Copernicus akiwa na umri wa miaka 70. Alizaliwa mwaka 1473 ambapo awali alijifunza elimu ya nujumu na baadaye tiba, na baada ya kukamilisha masomo alianza kufundisha hesabati huko Roma. Hata hivyo Copernicus aliendelea kudurusu na kufanya utafiti wa elimu ya nujumu na mwaka 1503 alivumbua nadharia ya harakati ya dunia kuzunguka jua na vilevile dunia kujizunguka yenyewe katika kila baada ya masaa 24. Nicolaus Copernicus alifariki dunia tarehe 24 Mei 1543 siku chache tu baada ya kuchapisha kitabu cha On the Revolutions of the Celestial Spheres kinachofafanua nadharia zake. Inafaa kuashirikia hapa kuwa, karne kadhaa kabla ya Corpenicus, mnajimu na msomi maarufu Muirani, Abu Raihan Biruni alikuwa tayari ameshavumbua ukweli kuwa sayari ya dunia huzunguka jua. Katika moja ya vitabu vyake, Corpenicus ameashiria ukweli huo.

Nicolaus Copernicus

Siku kama ya leo miaka 198 iliyopita yaani sawa na tarehe 24 Mei, 1822, nchi ya Ecuador ilipata uhuru wake kutoka kwa mkoloni Muhispania. Ecuador ni moja ya nchi za Amerika ya Kusini ambayo kupitia uongozi wa Simón Bolívar mwanamapinduzi maarufu wa Venezuela, ilifanikiwa kuwa huru na kujiunga na umoja wa Colombia Kubwa. Hata hivyo umoja huo ulisambaratika haraka na kuzipelekea nchi wanachama wa umoja huo ikiwemo Ecuador kuasisi mfumo wa jamhuri.

Ecuador

Siku kama ya leo miaka 27 iliyopita, sawa na tarehe 24 Mei 1993 Miladia, nchi ya Eritrea iliyoko kaskazini mashariki mwa bara la Afrika ilipata uhuru kutoka kwa Ethiopia. Mwaka 1936 Italia iliikalia kwa mabavu Eritrea iliyokuwa ikihesabiwa katika zama hizo kuwa sehemu ya ardhi ya Ethiopia. Mwaka 1953, Italia iliirejeshea Ethiopia ardhi hiyo. Hata hivyo wananchi wengi wa nchi hiyo waliokuwa wakitaka uhuru walianzisha harakati za ukombozi dhidi ya serikali ya Ethiopia. Mwaka 1991, Harakati ya Ukombozi wa Eritrea ikisaidiana na wanamapinduzi wa Ethiopia ilihitimisha utawala wa kidikteta wa Mengistu Haile Mariam, na wakakubaliana kuanishwa mustakbali wa Eritrea mwaka 1993 kupitia kura ya maoni. Washiriki wengi wa kura hiyo ya maoni walipiga kura ya kutaka kujitawala Eritrea. 

Bendera ya Eritrea

Siku kama ya leo miaka 20 iliyopita, sawa a tarehe 24 Mei mwaka 2000, vikosi vya utawala dhalimu wa Israel vililazimika kuondoka kwa madhila katika eneo la kusini mwa Lebanon baada ya kulikalia kwa mabavu kwa muda wa miaka 22. Majeshi hayo yaliondoka baada ya kushindwa kukabiliana na mapambano ya wananchi wa kusini mwa Lebanon. Mwaka 1982, majeshi ya utawala wa Kizayuni wa Israel yalishambulia Lebanon na kusonga mbele hadi katika mji mkuu wa nchi hiyo Beirut. Hata hivyo kutokana na wananchi hao kuathirika na mafundisho ya kutokubali dhulma hasa baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran, nchini Lebanon kulianzishwa harakati za mapambano ya Kiislamu dhidi ya majeshi vamizi ya utawala haramu wa Israel. Harakati ya Mapamabno ya Kiislamu ya Hizbullah ilikuwa na nafasi muhimu na ya kuzingatiwa katika kukombolewa eneo la kusini mwa Lebanon kutoka katika makucha ya utawala dhalimu wa Israel.

Bendera ya Harakati ya Hizbullah ya Lebanon