Feb 05, 2016 07:17 UTC
  • Hadithi ya Uongofu (29)

Ni matumaini yangu kuwa, hamjambo wapenzi wasikilizaji na karibuni katika sehemu nyingine ya kipindi cha Hadithi ya Uongofu. Kipindi hiki kama tulivyotangulia kusema hapo kabla, hujadili maudhui mbalimbali na kunukuu baadhi ya hadithi zinazohusiana na maudhui hizo.

Kwa hakika dini tukufu ya Kiislamu imelipa umuhimu mkubwa na wa hali ya juu, suala la kujipamba na sifa nzuri za kimaadili na kiakhlaqi kama kusaidia watu, kuwa mkarimu, kufanya juhudi kwa ajili ya kutatua matatizo ya wengine na kukidhi hawaiji na shida za watu. Kipindi chetu cha juma hili ambacho ni sehemu ya 29 ya mfululizo huu kitazungumzia sifa na tabia hii njema na ya kupendeza. Ni matumaini yangu kuwa, mtakuwa nami hadi mwisho wa kipindi hiki kusikiliza yale niliyokuandalieni kwa leo.
Kila Mwislamu anapenda kufahamu ibada bora kabisa ili kwa kuzitekeleza ibada hizo apate njia ya karibu kabisa ya kupata radhi za Mwenyezi Mungu. Tab'an, Mwenyezi Mungu ni mpole na Mwenye huruma na kabla hata ya waja wake, ni mwenye kupenda amali zao njema na kujikurubisha kwao kwake.
Imepokewa katika riwaya na hadithi kutoka kwa Bwana Mtume (s.a.w) na Ahlul-Bayt wake watoharifu (a.s) kwamba, kukidhi shida na haja za waumini ni miongoni mwa amali njema na zenye thamani ya hali ya juu. Amali hii imetajwa katika baadhi ya riwaya kwamba, ni zaidi ya kuwakomboa watumwa elfu moja katika njia ya Mwenyezi Mungu na ni bora kuliko kuwatayarisha na kuwapeleka katika medani ya vita wapiganaji elfu moja.
Imam Ja'afar Swadiq (a.s) amesema: Mtu ambaye atachukua hatua kwa ajili ya kukidhi haja ya muumini ili kutaka ujira wa Mwenyezi Mungu na akafanikiwa kutekeleza hilo, basi Mwenyezi Mungu Mtukufu atamuandikia ujira na thawabu za sawa na kuhiji na kufanya Umra, thawabu za kufunga Saumu miezi miwili na kukaa itikafu katika miezi mitukufu katika Masjid al-Haram huko Makka. Na mtu ambaye amenuia kufanya hivyo lakini hakufanikiwa kutekeleza nia yake hiyo ya kukidhi na kutekeleza haja na shida ya nduguye muumini, Mwenyezi Mungu humuandikia thawabu za Hija moja maqbuul. Hivyo basi kimbilieni kufanya wema na hisani."
Pamoja na hayo nukta ya kuzingatiwa hapa katika hili ni kwamba, kufanya amali hiyo ya wema na hisani licha ya thamani yote iliyonayo, katu jambo hilo haliwezi kuchukua nafasi ya jukumu na wadhifa mwingine wa kidini. Na hakuna mtu anayeweza kuacha kutekeleza mambo ya wajibu katika dini kama Swala na mengineyo kwa kusingizio cha kumhudumia kiumbe. Kwa hakika katika dini tukufu ya Kiislamu kila amali ina thamani kwa nafasi yake na analopaswa kuzingatia mwanadamu ni kutekeleza yale ambayo yana kipaumbele kulingana na mafundisho ya Uislamu.
Imam Ja'afar Swadiq (a.s) amenukuliwa akisema kuwa: Amali bora kabisa ni maarifa na kumtambua Muumba wa ulimwengu. Kisha Swala, Zaka, Saumu, Hija; na maarifa juu yetu sisi Ahlul Bayt (a.s) ndio amali iliyo bora zaidi. Kisha kuwafanyia wema na hisani ndugu katika dini ni katika amali bora kabisa."
Kwa hakika mtu ambaye anatatua shida na kukidhi mahitaji na hawaiji za watu, mbali na kupata radhi za Mwenyezi Mungu huwafurahisha pia waja wa Allah na wakati huo huo hupata utukufu na ubora duniani na akhera. Mtume (s.a.w) amesema: Mtu bora miongoni mwa watu ni yule ambaye ana faida na manufaa kwa watu wengine."
Nabii Issa Masih (a.s) naye amesema akiwa mtoto kwamba:
"Na amenijaalia ni mwenye kubarikiwa popote pale niwapo". Katika kufasiri aya hiyo ya 31 ya Surat Maryam, Imam Ja'afar Swadiq amesema: Kubarikiwa hapa ina maana ya mwenye kuwanufaisha watu wengine. Ndio maana huku kuwanufaisha watu wengine hupelekea mtu kuwa mwenye kubarikiwa.
Katika Uislamu kutatua shida ya Mwislamu imetambuliwa kuwa amali na kitendo ambacho kina msingi wa kumfurahisha Mwenyezi Mungu na vile vile Mtume wake (s.a.w). Imekuja katika hadithi mashuhuri kwamba, Mwenyezi Mungu ana nafasi katika nyoyo zenye imani. Aidha katika upande mwingine imepokea katika Hadith al-Qudsi kutoka kwa Mwenyezi Mungu ya kwamba amesema: Watu ni familia yangu, hivyo wapendwa zaidi kwangu miongoni mwao ni wenye huruma zaidi kwa familia yangu na ambao wanafanya hima na idili zaidi kwa ajili ya kutatua shida na hawaiji za watu."
Kwa hakika hadithi hizi mbili zinabainisha nukta muhimu mno nayo ni kwamba, kila mtu ambaye analeta furaha na nishati katika nyoyo za watu, Mwenyezi Mungu hufurahi na kumridhia na anakuwa ametoa zawadi ya amali nzuri kabisa mbele ya Mwenyezi Mungu.
Mtume (s.a.w) amesema: Kila mtu ambaye atamfurahisha muumini, amenifurahisha mimi, na kila mwenye kunifurahisha mimi amemfurahisha Mwenyezi Mungu."
Kwa hakika kumfurahisha Mwenyezi Mungu ambako kuna maana ya kumridhisha Mwenyezi Mungu na kupata radhi zake, hupelekea mtu kupata rehma maalumu za Mwenyezi Mungu. Tab'an, wanadamu wote wananufaika na ujazi na neema za Mwenyezi Mungu, lakini kuna baadhi ya watu kutokana na ustahiki wao wanaouonesha kutokana na kutenda amali njema, hujumuishwa katika rehma maalumu za Mwenyezi Mungu. Mtume (s.a.w) amesema:
Mtu ambaye atamuonyesha na kumrimu ndugu yake Mwislamu kwa neno zuri na la heshima na akamtatulia shida zake, basi huwa chini ya kivuli cha rehma za Mwenyezi Mungu madhali angali katika hali ya kufanya amali hiyo."
Miongoni mwa athari za kuwasaidia watu wengine na kushughulikia shida na matatizo yao ni mja kusamehewa dhambi zake. Hapana shaka kuwa, katika kipindi chote cha maisha hapa duniani sote wakati fulani huteleza na kutenda dhambi. Kufanya toba na kujutia dhambi ni njia bora kabisa ya mja kusamehewa na kufutiwa dhambi zake. Pamoja na hayo, kutenda wema na hisani, nayo ni amali yenye taathira katika kusamehewa dhambi za mtu.
Mwenyezi Mungu anasema katika aya ya 14 ya Surat Hud:
"Hakika mema huondoa maovu."
Je kwa kuzingatia aya hiyo na hadithi zilizotangulia, kuna wema na jema gani bora zaidi ya kusaidia waja wa Mwenyezi Mungu?
Imam Ali bin Abi Twalib (a.s) anasema:
Kafara ya dhambi kubwa ni kuitikia mayowe ya wenye shida na matatizona kutatua shida za waliokwama (katika mambo yao).
Imam Ja'afar Swadiq (a.s) amesema kuwa: Shindaneni katika kufanya amali njema na kuweni ni waja wa hilo. Hakika peponi kuna mlango ambao jina lake ni "Maarufu" ambao haingii kupitia mlango huo isipokuwa watu waliofanya wema na hisani.
Wapenzi wasikilizaji, muda wa kipindi chetu cha leo umefikia tamati hivyo sina budi kukomea hapa, nikitaraji kuwa mtakuwa nami wiki ijayo katika sehemu nyingine ya kipindi chetu hiki cha Hadithi ya Uongofu.
Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.