Feb 05, 2016 07:19 UTC
  • Hadithi ya Uongofu (30)

Assalaamu Alaykum wapenzi wasikilizaji na karibuni katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Hadithi ya Uongofu. Kama mnakumbuka, kipindi chetu cha wiki iliyopita kilijadili na kuzungumzia suala la kutatua shida za watu na jinsi jambo hilo lilivyotiliwa mkazo katika Uislamu.

Juma hili sehemu hii ya 30 ya mfululizo huu itaashiria baadhi ya misdaqi na mifano ya wazi ya kutatua shida ya mtu na kumkidhia haja yake na kuelezea athari zinazopatikana kwa kufanya amali hiyo inayopendwa na Mwenyezi Mungu na Mtume Wake. Ni matumaini yangu kuwa mtakuwa nami hadi mwisho wa kipindi hiki.
Hapana shaka kuwa, mahitaji ya kimsingi kabisa ya kimaada ya mwanadamu hapa duniani ni maji na chakula.
Imekuja katika hadithi kwamba, mtu kumpatia msaada mwenzake kwa mambo haya mawili yaani maji na chakula ni katika msaada wenye thamani kubwa mno. Kwani bila ya maji na chakula maisha ya mwanadamu yapo hatarini. Imam Ja'afar Swadiq (a.s) anasema kuwa:
Yeyote atakayempa chakula muumini na akamshibisha, hakuna anayetambua ujira wa hilo bighairi ya Mwenyezi Mungu, sio Malaika wala Nabii Mursali.
Imam Sajjad as amesema kuwa, yeyote ambaye atampa chakula mwenye njaa, Mwenyezi Mungu atamlisha matunda ya peponi na mtu ambaye atampatia maji muumini mwenye kiu, basi Mwenyezi Mungu Mtukufu atamnywesha kinywaji cha peponi.
Mavazi au nguo nayo ni katika mambo ya dharura katika maisha ya mwanadamu. Nguo mbali na kumsitiri mtu, humkinga na baridi na nguo anazovaa mtu huwa sababu ya shakhsia na heshima katika jamii anayoishi. Ni kwa kuzingatia ukweli huo ndio maana watu ambao wanafanya hima kwa ajili ya kukidhi na kudhamini mahitaji ya kimsingi ya maisha ya kimaada wana nafasi maalumu mbele ya Mwenyezi Mungu SWT.
Imam Ali bin Hussein Zeinul Abidin (a.s) anasema kuwa: Mtu yeyote ambaye atampatia chakula mtu mwenye njaa, Allah atamlisha matunda ya peponi na yeyote ambaye atampa maji mwenye kiu Mwenyezi Mungu atamnywesha maji matamu kutoka katika chemchemi ya peponi na kila ambaye atampa nguo na kumsitiri mtu ambaye hana nguo, Allah atamvisha mtu huyo nguo ya kijani kutoka peponi."
Amali nyingine njema na stahiki katika Uislamu ni watu kukopeshana. Kukopesha ni katika mifano ya wazi kabisa ya kutatua shida na haja za watu. Kuhusiana na utukufu wa amali hii inayopendwa na Mwenyezi Mungu Mtume s.a.w amesema: Mtu ambaye atamkopesha ndugu yake Mwislamu, basi Mwenyezi Mungu atampatia mkabala wa kila dirihamu moja aliyoikopesha mambo mema sawa na uzito wa mlima Uhud, mlima Ridhwan na mlima Sinai na endapo atakuwa mwenye subira wakati wa kufuatilia kwa ajili ya kurejeshewa deni lake, basi Mwenyezi Mungu atampitisha katika njia ya Sirat kwa kasi kama umeme bila ya hesabu wala adhabu."
Kwa hakika hadithi hii inaonesha fadhila kubwa za mtu kumkopesha ndugu yake Mwislamu ambaye ana shida na amekwama katika jambo fulani. Aidha Mtume (saw) anazungumzia kitendo cha mtu mwenye uwezo ambaye anajiwa na ndugu yake Mwislamu ili amkopeshe, lakini licha ya kuwa na uwezo wa kufanya hivyo huamua kutomtekelezea shida yake nduguye.
Anasema. Amtu ambaye atajiwa na nduguye Mwislamu na hali ya kuwa ni mwenye shida lakini licha ya kuwa na uwezo wa kumtekelezea shida hiyo akakataa kufanya hivyo, Mwenyezi Mungu humharamishia mtu huyo harufu ya pepo.
Misdaqi na mfano mwingine muhimu wa kutatua shida za watu ni kulipa madeni ya wengine. Kwa maana kwamba, kuna ndugu Mwislamu mwenye deni ambapo kutokana na mazonge na ugumu wa maisha alionayo ameshindwa kulipa madeni deni alilonalo, wewe ukaja na kumlipia deni hilo au madeni yake. Kitendo hiki nacho ni miongoni mwa amali zinazopendwa na Mwenyezi Mungu.
Imam Ja'afar Swadiq (a.s) anasema: "Amali zinazopendwa zaidi mbele ya Mwenyezi Mungu ni kumfurahisha muumini kwa kumshibisha au kumtatulia shida yake au kumlipia deni lake."
Inasimuliwa kwamba, siku moja Imam Hussein (a.s) alikwenda kumtembelea mgonjwa aliyejulikana kwa jina la Usama bin Zeid. Usama alikuwa na ghamu na huzuni sana. Imam akamuuliza kwa nini ni mwenye huzuni na ghamu kiasi hicho? Usama akamjibu Imam kwa kusema:
Nina deni la dirihamu elfu 60 ambalo nilimkopa mtu na ndilo ambalo limezizonga na kunifanya niingiwe na huzuni. Imam Hussein (a.s) akamwambia, usihuzunike! Mimi nitalipa deni lako hilo. Usama akasema: Nahofia na kuchelea kuaga dunia kabla sijalipa madeni yangu. Imam akasema: Mimi ninakuhakikishia kwamba, nitalipa madeni yako yote kabla hujaaga dunia. Kama alivyokuwa ameahidi, Imam Hussein (a.s) alilipa madeni ya Usama kabla ya kufariki kwake dunia.
Na hadi hapa wapenzi wasikilizaji ndio tunafikia tamati ya kipindi chetu kwa juma hili. Tunamuomba Mwenyezi Mungub atujaalie kuwa miongoni mwa wanaofanya hima na idili kwa ajili ya kushughulikia na kutatua matatizo ya watu na tunapokopeshwa basi tuwe waaminifu na kulipa madeni kwa wakati.
Wassalaamu Alaykumu Warahmatullahi Wabarakaatuh.