Jumanne, Julai 14, 2020
Leo ni Jumanne tarehe 22 Dhulqaada 1441 Hijria inayosadifiana na Julai 14 mwaka 2020.
Miaka 905 iliyopita katika siku kama ya leo kazi ya kuandika tafsiri mashuhuri ya Majmaul Bayan ilimalizika. Kitabu hicho kiliandikwa na Sheikh Tabarsi mmoja wa wafasiri wakubwa wa Qur'ani Tukufu na miongoni mwa maulamaa mashuhuri wa Iran aliyekuwa mashuhuri kwa jina la Aminul Islam kutokana na uaminifu na uchamungu wake. Kitabu hicho ni miongoni mwa tafsiri mashuhuri za Qur'ani kutokana na mbinu yake ya kuvutia katika mtazamo wa fasihi. Tafsiri hiyo imechapishwa mara kadhaa katika nchi za Iran, Lebanon na Misri.
Siku kama ya leo miaka 231 iliyopita, gereza la kihistoria la Bastille lilitekwa na wakazi wa Paris katika kipindi cha mapinduzi ya Ufaransa na sehemu kubwa ya gereza hilo kuharibiwa. Jela hiyo ilijengwa mwaka 1369 kwa lengo la matumizi ya kijeshi. Hata hivyo baada ya kupita miaka kadhaa iligeuka na kuwa gereza la kutisha ambapo ndani yake walizuiliwa wafungwa wengi wa kisiasa hususan watu waliokuwa wakiendesha harakati za kudai jamhuri nchini humo. Gereza la Bastille lilidhihirisha udikteta wa wafalme wa Ufaransa.
Katika siku kama ya leo miaka 159 iliyopita ilitengenezwa bunduki ya kwanza ya rashasha. Bunduki hiyo ilitengenezwa na msomi wa Kimarekani Dr. Richard J. Gatling kwa kutumia uzoefu wa wavumbuzi wa kabla yake wa silaha. Bunduki iliyotengezwa na Gatling haikuwa ya utomatiki lakini baadaye teknolojia ya kutengeneza silaha hiyo ilikamilishwa zaidi na hii leo bunduki ya rashasha inatambuliwa kuwa silaha muhimu sana katika medani za vita.
Siku kama ya leo miaka 81 iliyopita inayosadifiana na tarehe 24 Tir 1318 Hijria Shamsia, alizaliwa Ayatullahil Udhma Sayyid Ali Khamenei Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu katika mji wa Mash'had ulioko kaskazini mashariki mwa Iran. Baada ya kumaliza masomo katika shule ya sekondari, alijikita zaidi katika masomo ya kidini kutoka kwa baba yake, na kupiga hatua kubwa ya kielimu katika kipindi kifupi. Ayatullah Khamenei alielekea mjini Qum kwa masomo ya juu ya kidini, na kupata fursa ya kunufaika na elimu kutoka kwa maulamaa wakubwa katika mji huo, kama vile Imam Khomeini MA, Ayatullahil Udhma Burujerdi na Allamah Tabatabai katika masomo ya fiqh, usulul na falsafa. Akiwa bado kijana, licha ya kuendelea na masomo, lakini alikuwa mstari wa mbele katika harakati za mapinduzi dhidi ya utawala wa kibaraka wa Shah hapa nchini, na mara kadhaa alitiwa mbaroni, kutumikia vifungo na hata kubaidishwa. Mara baada ya kufariki dunia Imam Khomeini MA mwaka 1368 Hijria Shamsia, Baraza la Wanachuoni linalomchagua Kiongozi Muadhamu, lilimchagua Ayatullah Khamenei wakati huo akiwa rais wa nchi, kuwa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu.
Miaka 62 iliyopita katika siku kama ya leo, Jenerali Abdul Karim Qassim alifanya mapinduzi nchini Iraq na kuuondoa madarakani utawala wa Kifalme na kisha kuanzisha mfumo wa utawala wa serikali ya jamhuri. Faisal II mwana wa mfalme na Waziri Mkuu wa Iraq waliuawa katika tukio hilo la mapinduzi. Aidha wafuasi wa utawala wa Kifalme walikandamizwa na kusambaratishwa kabisa. Baada ya mapinduzi hayo, Abdul Karim Qassim aliyekuwa na mirengo ya utaifa alishika hatamu za uongozi nchini Iraq hadi mwaka 1963, wakati alipokuja kuondolewa madarakani kwa njia ya mapinduzi pia na Abdul Salam Arif aliyekuwa muitifaki wake mkubwa na wa karibu.
Siku kama ya leo miaka 10 iliyopita inayosadifiana na tarehe 24 Tir 1389 Hijria Shamsia, kwa akali watu 27 waliuawa na wengine 169 kujeruhiwa, kwenye milipuko miwili ya mabomu iliyotokea katika mji wa Zahedan, ulioko kusini mashariki mwa Iran. Milipuko hiyo ilitokea mkabala na Msikiti Mkuu wa Zahedan, wakati wa kufanyika sherehe za kuadhimisha siku ya kuzaliwa Imam Hussein bin Ali bin Abi Talib AS mmoja kati ya wajukuu wa Mtume Mtukufu Muhammad SAW. Kikundi cha kigaidi kilichojiita Jundullah, ndicho kilichotekeleza shambulio hilo la kigaidi.