Aug 08, 2020 04:23 UTC
  • Jumamosi, 08 Agosti, 2020

Leo ni Jumamosi tarehe 18 Mfunguo Tatu Dhul-Hija 1441 Hijria mwafaka na tarehe 8 Agosti 2020 Miladia.

Siku kama ya leo miaka 2353 iliyopita sawa na tarehe 8 Agosti 333 kabla ya kuzaliwa Nabii Issa Masih AS, ilianza kazi ya ujenzi wa mji wa Alexandria nchini Misri, ambao leo hii unahesabiwa kuwa moja kati ya bandari muhimu kusini mwa Bahari ya Mediterranean. Ujenzi huo ulifanyika kwa amri ya Alexander Macedon huko kaskazini mwa Misri.***

Alexandria

 

Siku kama hii ya leo miaka 1431 iliyopita Mtume Muhammad (SAW) akiwa katika safari yake ya mwisho ya Hija, kwa amri ya Mwenyezi Mungu alimtangaza Imam Ali bin Abi Twalib AS kuwa kiongozi wa Waislamu wote baada yake. Hatua hiyo ya Mtume Mtukufu ilifanyika katika eneo linalojulikana kwa jina la Ghadir Khum katika makutano ya njia ya Makka na Madina. Siku hiyo Mtume SAW alitoa hotuba mbele ya hadhara kubwa ya Waislamu kisha akashika mkono wa Ali bin Abi Twalib na kusema: "Kila mtu ambaye mimi ni kiongozi wake basi huyu Ali pia ni kiongozi wake. Mwenyezi Mungu ampende atakayempenda, na amfanyie uadui atakayemfanyia uadui." Mtume SAW pia aliwausia Waislamu kushikamana na Qur'ani na Ahlubaiti wake na akasema viwili hivyo havitatengana hadi vitakapomkuta yeye katika Hodhi ya Kauthar, Siku ya Kiyama. ***

Tukio la Ghadir

 

Katika siku kama ya leo miaka 769, alifariki dunia Nasiruddin Tusi, mwanafalsafa, mtaalamu wa hesabati na nujumu na msomi mkubwa wa Kiislamu huko katika mji wa Tus, kaskazini mashariki mwa Iran. Nasiruddin Tusi aliishi katika kipindi cha Hulagu Khan Mongol na aliasisi kituo kikubwa na cha kwanza cha sayansi ya nujumu huko Maraghe kaskazini magharibi mwa Iran. Nasiruddin Tusi ameandika vitabu zaidi ya 80 kwa lugha za Kiarabu na Kifarsi. Vitabu muhimu zaidi vya msomi huyo ni pamoja na ‘Asasul-Iqtibaas’, ‘Akhlaaq Naaswiri’, ‘Awsaful-Ashraaf’ na ‘Sharhul Ishaarat. ***

Nasiruddin Tusi

 

Tarehe 18 Dhulhija miaka 227 iliyopita alizaliwa faqihi na msomi mkubwa wa Kiislamu, Sheikh Murtadha Ansari katika mji Dezful nchini Iran na baada ya kupata elimu ya msingi kwa baba yake alielekea katika miji mitakatifu ya Karbala na Najaf huko Iraq kwa ajili ya elimu ya juu. Miaka kadhaa baadaye Sheikh Ansari alitambuliwa kuwa miongoni mwa wanazuoni na walimu mashuhuri wa zama hizo. Msomi huyo wa Kiislamu ameandika vitabu vingi vikiwemo vile vya Rasaail na Makaasib ambavyo vingali vinatumiwa hadi sasa kufundishia katika vyuo vikuu vya kidini. ***

Sheikh Murtadha Ansari

 

Na miaka 22 iliyopita katika siku kama ya leo inayosadifiana na tarehe 8 Agosti 1998, wanamgambo wa kundi la Taliban nchini Afghanistan waliuteka na kuukalia kwa mabavu mji wa Mazar Sharif ulioko kaskazini mwa nchi hiyo. Baada ya kukaliwa kwa mabavu mji huo, wanamgambo wa Taleban waliushambulia ubalozi mdogo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika mji huo na kuwauwa shahidi wanadiplomasia 8 wa Kiirani na mwandishi mmoja wa habari. Kundi la Taliban liliasisiwa mwaka 1994 kwa ufadhili na usaidizi wa Marekani na Pakistan na kufanikiwa kuikalia sehemu kubwa ya ardhi ya Afghanistan.***

Mazar Sharif

 

Tags