Aug 19, 2020 02:25 UTC
  • Jumatano tarehe 19 Agosti 2020

Leo ni Jumatano tarehe 29 Dhulhija 1441 Hijria sawa na 19 Agosti mwaka 2020.

Miaka 358 iliyopita katika siku kama ya leo, alifariki dunia Blaise Pascal, mwandishi, mwanahesabati na mvumbuzi wa calculator au kikokotoo wa Kifaransa. Alizaliwa Juni mwaka 1623 na tangu utotoni Pascal alivutiwa mno na somo la hisabati. Vilevile urafiki uliokuwepo kati ya baba yake Pascal na msomi mmoja maarufu wa zama hizo ulisaidia mno katika kuchanua kipawa na kugunduliwa uwezo wa kijana huyo katika taaluma ya hisabati. Mwishoni mwa umri wake Blaise Pascal alijielekeza mno katika masuala ya dini na kuandika vitabu kadhaa katika uwanja huo. 

Blaise Pascal

Siku kama hii ya leo miaka 201 iliyopita aliaga dunia mvumbuzi na mhandisi wa Kiingereza James Watt. Msomi huyo alipendelea na kuvutiwa mno na utafiti kuhusu masuala ya kisayansi. Katika utafiti wake Watt alifanikiwa kuvumbua nishati ya mvuke na kuzusha mapinduzi makubwa katika sekta ya viwanda hususan usafirishaji wa nchi kavu na baharini.

James Watt

Siku kama ya leo miaka 32 iliyopita Marekani ilikiri kwamba ilifanya makosa kuishambulia ndege ya abiri ya Iran hapo tarehe 3 Julai mwaka 1988. Siku hiyo ndege ya abiria aina ya Airbus ya shirika la ndege ya Iran iliyokuwa ikitoka Bandar Abbas kusini mwa Iran na kuelekea Dubai Umoja wa Falme za Kiarabu ilishambuliwa kwa makombora mawili kwenye maji ya Ghuba ya Uajemi. Manowari ya kijeshi ya Marekani USS Vincennes ilifyatua makombora hayo na kuuaa shahidi watu 298 waliokuwemo. Shambulio hilo lilionyesha wazi unyama wa serikali ya Marekani na ukatili wake hata kwa wanawake na watoto wadogo waliokuwemo ndani ya ndege hiyo. Viongozi wa Marekani walizidisha ukatili wao pale walipomzawadia medali ya ushujaa nahodha wa meli hiyo kutokana na kitendo hicho kilichoonekana na serikali ya Washington kuwa eti ni cha kishujaa.

Ndege ya abiria ya Iran ilitunguliwa kwa kombora la Marekani

Siku kama ya leo miaka 29 iliyopita, makamanda wa ngazi za juu wa jeshi la Urusi ya zamani wakiongozwa na Gennady Ivanovich Yanayev walifanya mapinduzi dhidi ya rais wa mwisho wa Muungano wa Sovieti, Mikhail Gorbachev. Wanajeshi hao walitaka kukomeshwa marekebisho ya Gorbachev na kuzuia mpango wa kugawanywa Urusi ya zamani. Wakati wa mapinduzi hayo Mikhail Gorbachev alikuwa katika Peninsula ya Crimea huko kaskazni mwa Bahari Nyeusi. Hata hivyo Boris Yeltsin ambaye wakati huo alikuwa kiongozi wa Federesheni ya Urusi na ambaye alikuwa akiungwa mkono na Magharibi, alizima mapinduzi hayo kwa msaada wa wananchi na baadhi ya watu wenye ushawishi serikalini. Kushindwa kwa mapinduzi hayo kulizidisha uwezo na satua ya Boris Yeltsin na kuharakisha mwenendo wa kusambaratika Urusi ya zamani hapo mwaka 1991.

Gennady Ivanovich Yanayev

 

Tags