Jumanne, tarehe 8 Septemba, 2020
Leo ni Jumanne tarehe 19 Muharram 1442 Hijria inayosadifiana na Septemba 8 mwaka 2020.
Tarehe 8 Septemba ilitangazwa na Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa kuwa ni Siku ya Kimataifa ya Kupambana na Ujinga. Kujua kusoma na kuandika ni miongoni mwa vielelezo cha ustawi katika jamii ya mwanadamu na ujinga husababisha umaskini na kubakia nyuma kimaendeleo. Kwa mujibu wa ripoti za Umoja wa Mataifa mkakati wa kupambana na kutojua kusoma na kuandika haukuwa wa kuridhisha katika baadhi ya nchi na hadi sasa idadi kubwa ya watu hawajapata neema hiyo.
Nchini Iran baada tu ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu na kwa mujibu wa mafundisho ya Uislamu kulifanyika jitihada kubwa za kupambana na ujinga wa kutojua kusoma na kuandika kwa kadiri kwamba Disemba mwaka 1979 Imam Ruhullah Khomeini alitoa amri ya kuasisiwa Harakati ya Kupamgana na Ujinga. Taasisi hiyo imechukua hatua kubwa hapa nchini.

Tarehe 19 Muharram mwaka 61 Hijria msafara wa mateka wa Karbala uliokuwa na familia ya mjukuu wa Mtume, Imam Hussein (as) na mashahidi wengine waliouawa na utawala wa Yazid bin Muawiya katika medani ya Karbala uliondoka Kufa nchini Iraq ukielekea Damascus, makao makuu ya serikali ya bani Umayyah. Msafara huo hususan Imam Zainul Abidin na Bibi Zainab binti Ali bin Abi Twalib (as) ulifichua na kuanika maovu ya Yazid bin Muawiyyah na kuwafanya watu wa Kufa wajute sana kwa kumuacha peke yake mjukuu wa Mtume (saw), Imam Hussein katika mapambano ya Karbala. Watu wa mji wa Kufa walisikitika sana kutokana na kumwacha peke yake mjukuu huyo wa Mtume na wasiwasi ulizuka juu ya uwezekano wa kuanza harakati ya wananchi dhidi ya utawala wa Yazid mjini humo. Kwa msingi huo mtawala wa Kufa, Ubaidullah bin Ziyad, alikhitari kutuma wajukuu hao wa Mtume wetu Muhammad (saw) huko Sham kwa mtawala dhalimu Yazid bin Muawiyyah wakitanguliwa na kichwa kilichotenganishwa na mwili cha Bwana wa Vijana wa Peponi, Imam Hussein (as).

Miaka 257 iliyopita katika siku kama ya leo, baada ya mapigano ya muda mrefu na kwa mujibu wa makubaliano ya Paris, Canada iliondoka chini ya udhibiti wa Ufaransa na kudhibitiwa rasmi na Uingereza. Hata hivyo mivutano baina ya Wacanada wenye asili ya Ufaransa na Waingereza waliokuwa wakiishi Canada iliendelea kwa muda mrefu. Licha ya Canada kujitangazia uhuru na mamlaka ya kujitawala mwaka 1867 lakini nchi hiyo inafuata Uingereza katika mfumo wake wa kisiasa.

Katika siku kama ya leo miaka 79 iliyopita, wanajeshi wa Ujerumani ya Kinazi waliuzingira mji wa Leningrad, Saint Petersburg ya sasa. Hata hivyo mji huo haukutekwa na jeshi la Kinazi licha ya matarajio ya Adolf Hitler na makamanda wake. Wakazi wa Leningrad waliendeleza mapambano ya ukombozi hadi Januari mwaka 1944 wakati walipofanikiwa kujiondoa katika mzingiro wa wanajeshi wa Ujerumani.

Siku kama ya leo miaka 66 iliyopita, kulitiwa saini mkataba wa ulinzi wa mataifa ya Asia ya kusini mashariki (SEATO) katika mji mkuu wa Ufilipino, Manila. Mkataba huo ulitiwa saini na nchi za Marekani, Uingereza, Australia, Pakistan, Thailand, Ufaransa, New Zealand na Ufilipino. Kwa mujibu wa mkataba huo, nchi mwanachama itakapokabiliwa na mashambulio ya kijeshi kutoka nje, uasi na vitisho vya ndani, basi nchi wanachama zinapaswa kuisaidia nchi hiyo kijeshi au kwa kutumia wenzo wa vikwazo.
