Jumatatu tarehe 7 Septemba 2020
Leo ni Jumatatu tarehe 18 Muharram 1442 Hijria sawa na Septemba 7 mwaka 2020.
Siku kama ya leo miaka 198 iliyopita, nchi ya Brazil ilipata uhuru kutoka kwa mkoloni Mreno. Ureno ilianza kuikoloni Brazil mwaka 1494, na mbali na kuwatumikisha watu wa jamii ya Wahindi Wekundu wa nchi hiyo, ilichukua mamilioni ya Waafrika kwa ajili ya kuwatumikisha kama watumwa katika shughuli za kilimo.
Siku kama ya leo, miaka 149 iliyopita alizaliwa Allamah Haidar Qali Sardor Kabuli, alimu mkubwa na mtaalamu wa fiqhi huko Kabul, Afghanistan. Akiwa kijana mdogo Allamah Sardor Kabuli alipata kusoma kwa wasomi wakubwa wa enzi hizo kama vile, Mirza Hussein Nuri na Sayyid Swafiyyud-Din Hassan bin Hadi Kadhimi, sanjari na kustafidi na elimu kutoka kwa maulama na maraajii watajika kama vile, Sayyid Hassan Sadr naHaji Sheikh Abbas Qumi, ambapo pia alipata ijaza (idhini) ya kunakili na kuandika riwaya na hadithi. Mwaka 1310 Hijiria, Allamah Haidar Qali Sardor Kabuli alielekea mjini Kermanshah, Iran na kujishughulisha na ufundishaji kwa wakazi wa mji huo sanjari na kuandika vitabu kadhaa. Aidha msomi huyo alipata kusomea lugha kadhaa za dunia, kama vile Kiarabu, Kingereza, Kiebrania na Urdu. Kitabu cha ‘Tarjama ya Injili ya Barnaba’ na ‘Hadithi 40 katika fadhila za Amirul-Muuminin’ ni miongoni mwa athari za msomi huyo. Allamah Haidar Qali Sardor Kabuli alifariki dunia mwaka 1372 Hijiria, akiwa na umri wa miaka 79 na kuzikwa mjini Najaf, Iraq.
Siku kama ya leo miaka 133 iliyopita alizaliwa Ayatullah Sayyid Ahmad Khansari, faqihi na marjaa mkubwa wa Kiislamu. Akiwa na miaka 20, Ayatullah Ahmad Khansari alielekea mjini Najaf, Iraq na kustafidi na elimu kutoka kwa wasomi wakubwa kama vile Muhaqqiq Khorasani, Sayyid Muhammad Kadhim Yazdi, Shariat Isfahani na Muhaqqiq Naaini. Ayatullah Sayyid Ahmad Khansari alielekea mjini Arak, Iran katika kipindi cha kuasisiwa chuo cha hauza cha mji huo na kujishughulisha na ukufunzi. Baadaye msomi huyo alishirikiana na Ayatullah Sheikh Abdul-Karim Hairi katika shughuli za tablighi na baada ya kuasisiwa hauza ya Qum, chini ya usimamizi wa Ayatullah Hairi Yazdi, Ayatullah Ahmad Khansari alikuwa imamu wa swala ya jamaa katika chuo cha Faiziya mjini humo. Mwaka 1370 Hijiria, Ayatullah Ahmad Khansari alielekea mjini Tehran na kuwa imamu wa swala ya jamaa katika msikiti maarufu wa ‘Sayyid Azizullah’. Hadi mwisho wa uhai wake msomi huyo alisalia mjini Tehran na baada ya kufariki dunia akazikwa mjini Qum.
Siku kama ya leo miaka 121 iliyopita harakati ya kihistoria ya Wanamasumbwi nchini Uchina ilikandamizwa na kuzimwa. Wanamasumbwi lilikuwa jina walilopewa wanajeshi wa China waliosimama kupambana na ubeberu wa nchi za kigeni hususan za Magharibi ulioambatana na harakati za wamishonari wa Kikristo ndani ya China. Miongoni mwa hatua zilizochukuliwa na wanamasumbwi hao ni kuteka balozi za nchi za Magharibi katika mji wa Beijing na kupambana vikali na shughuli za wahubiri wa Kikristo kutoka Ulaya. Harakati ya Wanamasumbwi wa Kichina ilikandamizwa na majeshi ya Ulaya, Marekani na Japan na serikali ya China ikalazimika kulipa gharama kubwa kwa nchi hizo.
Siku kama ya leo miaka 42 iliyopita, wanajeshi wa utawala wa kidikteta wa Pahlavi walishambulia maandamano makubwa ya wananchi wa mji wa Tehran na kuua raia wengi. Wananchi Waislamu wakazi wa Tehran siku hiyo walianza kuandamana tangu asubuhi, hayo yakiwa maandamano ya siku kadhaa mfululizo kuwahi kufanywa na wakazi wa mji wa Tehran dhidi ya utawala wa kibaraka wa Pahlavi. Wakati huo, utawala wa kijeshi ulikuwa umetangazwa katika mji wa Tehran, lakini wananchi Waislamu bila ya kuzingatia hali hiyo, wakamiminika mitaani wakipiga nara dhidi ya utawala wa Shah. Wakati huo huo walinzi maalumu wa Shah walifanya mashambulizi na katika muda mfupi wakawaua shahidi wananchi zaidi ya elfu nne wa Tehran waliokuwa wakipigania haki zao.
Siku kama ya leo miaka 23 iliyopita alifariki dunia dikteta wa zamani wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo au Zaire ya zamani, Jenerali Mobutu Sese Seko. Mobutu alizaliwa mwaka 1930 nchini Congo na mwaka 1950 alijiunga na harakati ya ukombozi ya Patrice Lumumba. Baada ya uhuru wa Congo, Jenerali Mobutu alishika uongozi wa jeshi la nchi hiyo na mwaka 1960 alikuwa waziri mkuu akiwa na umri wa miaka 30. Tarehe 25 Novemba mwaka 1965 Mobutu alipindua serikali na kushika hatamu za nchi hiyo aliyeitawala kidikteta. Tarehe 16 Mei 1997 Mobutu alilazimika kukimbia nchi hiyo na kwenda Morocco ambako alifia na kuacha nyuma faili jesi la ukatili na mauaji.