Jan 31, 2021 02:53 UTC
  • Jumapili, Januari 31, 2021

Leo ni Jumapili tarehe 17 Mfunguo Tisa Jamadithani 1442 Hijria mwafaka na tarehe 31 Januari 2021 Miladia.

Siku kama ya leo tarehe 12 Bahman kwa mujibu wa kalenda ya Hijria Shamsia mwafaka na tarehe 31 Januari miaka 42 iliyopita, Imam Khomein (MA) muasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, alirejea nchini na kupokelewa kwa nderemo na shangwe kubwa na wananchi baada ya kuishi uhamishoni kwa kipindi cha miaka 15. Imam Khomeini alirejea hapa nchini akitokea uhamishoni Ufaransa huku harakati za wananchi zikiwa zimepamba moto kuelekea ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu. Inapaswa kufahamika kuwa, kurejea nchini Imam kutoka uhamishoni kulitengeneza historia mpya ya taifa hili. Kadhalika ujio huo ni nukta muhimu mno ya kipindi cha kukaribia ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu. Mapokezi hayo makubwa ya wananchi wa Iran kwa Imam Khomeini hayajawahi kushuhudiwa mfano wake katika historia ya sasa ya dunia. Baada ya kutoa hotuba fupi katika uwanja wa ndege wa Mehrabad, Imam Khomein alielekea moja kwa moja kwenye makaburi ya mashahidi waliouawa katika harakati za Mapinduzi ya Kiislamu kwa ajili ya kutoa heshima kwa mashahidi hao ambako pia alitoa hotuba katika umati mkubwa wa wananchi. Kwa mara nyingine Imam aliitaja serikali ya Shapour Bakhtiar kuwa kibaraka wa Shah sanjari na kutangaza kuunda serikali mpya kwa msaada wa wananchi. Siku kumi baada ya kurejea nchini Imam, Mapinduzi ya Kiislamu yalipata ushindi kamili na kipindi hicho cha siku kumi za baina ya kurejea Imam nchini hadi kupata ushindi kamili Mapinduzi ya Kiislamu, kinajulikana hapa nchini kama "Alfajiri Kumi".

Imam Ruhullah Khomeini akirejea Iran kutoka uhamishoni

##########

Siku kama ya leo miaka 918 iliyopita, yaani tarehe 17 Jamadithani mwaka 524 Hijiria, alifariki dunia Bari'i Baghdadi, mwanafasihi na malenga mashuhuri wa Kiarabu. Baghdadi alizaliwa mwaka 443 Hijiria na kuanza kusomea elimu ya nahau na lugha kutoka kwa maulama wakubwa wa kipindi chake. Moja ya athari mashuhuri za Bari'i Baghdadi ni kitabu cha mashairi kilichopewa jina lake. Malenga na mshairi huyo aliaga dunia akiwa na umri wa miaka 81 hali akiwa ni kipofu.

Bari'i Baghdadi

##########

Siku kama ya leo miaka 171 iliyopita, ilianzishwa harakati kubwa ya uasi wananchi wa China iliyokuwa ikijulikana kwa jina la Taiping. Harakati hiyo ilitokana na hali mbaya na umasikini uliokuwa ukiwasumbua wananchi wa nchi hiyo na hasa matabaka ya watu wa vijijini, iliyosababishwa na ukoloni wa kigeni na utawala wa familia isiyofaa ya Manchu. Lengo kuu la harakati hiyo iliyodumu kwa muda wa miaka 14 lilikuwa ni kuwepo usawa katika kugawana ardhi kati ya wanawake na wanaume.

Uasi wa Taiping

##########

Na siku kama ya leo miaka 422 iliyopita, ilianzishwa kampuni ya kwanza ya Uingereza ya India Mashariki nchini India kwa amri ya Malkia Elizabeth wa Kwanza wa Uingereza. Kampuni hiyo iliimarisha ukoloni wa Uingereza katika maeneo yenye utajiri huko kusini mwa Asia na baada ya hapo shughuli za ukoloni zikaimarika zaidi katika mataifa ya kusini mwa Asia kupitia kampuni hiyo. Baada ya kuasisiwa kampuni hiyo, nchi nyingine kama vile Uholanzi, Ureno na Ufaransa zilielekeza nguvu zao katika bara Hindi kwa lengo la kuhudumia ukoloni wao. Baada ya karne 3 za kuanzishwa shirika hilo, ushawishi na kuimarika utawala wa Uingereza nchini India vilisababisha nchi hiyo kutangazwa kuwa sehemu ya Uingereza na Malkia Viktoria akavikwa taji la kuwa mtawala wa India na Uingereza.

Kampuni ya India Mashariki nchini India 

 

Tags